TMF kutoa ruzuku kuchunguza tukio la Kibanda









MFUKO wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) utatoa ruzuku na kuungana na wadau wa habari nchini na nje ya nchi kuchunguza chanzo cha ukatili uliofanywa na watu wasiojulikana dhidi ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri(TEF), Absalom Kibanda.

Mkurugenzi wa TMF, Ernest Sungura amesema kuna kila sababu ya kuchunguza tukio hilo ambalo ni mfululizo wa matukio yanayopunguza uhuru wa vyombo vya habari nchini na kujenga woga kwa waandishi kufanya uandishi wa habari za uchunguzi nchini.

“Kumejitokeza mfululizo wa matukio yanayopunguza uhuru wa vyombo vya habari kufanya kazi zake bila woga. Tulikuwa nchi ya 30 duniani kwa kuwa na uhuru wa vyombo vya habari mwaka mmoja uliopita. Tumeshuka mpaka nchi ya 70 mwaka huu. Matukio ya aina hii yanaendelea kutuweka mahali pabaya, “ alisema Sungura jana.

Alisema TMF ina wajibu wa kuongeza wingi na ubora wa habari za kiuchunguzi kupitia vyombo vya habari ambazo zinahitaji mazingira salama yasiyo na vitisho katika kufanikisha uandishi wa aina hiyo.

“Kwa vyovyote vile na kwa sababu zozote, wanaotoa vitisho kwa waandishi na kuwafanyia vitendo vya kikatili ni maadui wa uandishi wa habari za uchunguzi. Ni kwa msingi huu, TMF iko tayari kutoa ruzuku na kuungana na wadau wengine wa habari kuchunguza kilichompata Kibanda, “ alisisitiza Sungura.

Aidha, alisema TMF katika awamu ijayo, itaandaa mpango mkakati unaolenga kulinda waandishi wa habari wanaofanya uandishi wa habari za uchunguzi ikiwamo kufikiria uwezekano wa kuwawekea bima ya kazi kwenye mazingira hatarishi. Kibanda, ambaye ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited, ni mwandishi ambaye yuko mstari wa mbele kuhimiza uhuru wa vyombo vya habari, uandishi unaozingatia maadili na maendeleo ya tasnia ya habari kwa ujumla.

Mhariri huyo alivamiwa na kushambuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake saa 6.15 usiku wa kuamkia Jumatano iliyopita, maeneo ya Goba Kunguru, Mbezi Juu, kata ya Kawe, Dar es Salaam.

Kwa sasa yuko Afrika Kusini kwa matibabu zaidi. Kwa mujibu wa Katibu wa TEF, Neville Meena, Kibanda alijeruhiwa kichwani kwa kupigwa na kitu ambacho yeye alisema ni nondo huku jicho la kushoto likiathirika kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali, kucha ya kidole cha mkono wa kulia kung’olewa sambamba na meno mawili.

Katibu huyo alisema akiwa kwenye lango, ghafla walitokea watu watatu ambao walivunja kioo cha gari ambako alikoketi, na kumvuta nje na kutekeleza walichokusudia.

Mpaka sasa vyombo vilivyojitokeza kushtushwa na kilichomtokea Kibanda ambavyo TMF itaungana navyo kutafuta mustakabali wa Kibanda ni TEF, MCT, UTPC, MISA-Tan, CPJ, FAIR, AJAAT na Haki za Binadamu.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company