|
TUME huru ya uchaguzi nchini Kenya (IEBC), jana ilimtangaza
Uhuru Kenyatta kupitia Muungano wa Jubilee kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu
uliofanyka Jumatatu wiki hii.
Kenyatta ambaye anakuwa rais wa nne wa taifa hilo, alijipatia kura
6,173,433 (50.03%) na kumwangusha hasimu wake wa karibu Waziri Mkuu
anayemaliza muda wake, Raila Odinga aliyejipatia kura 5,340,546
(43.28%) kati ya kura 12,338,667 zilizopigwa.
Tunampongeza Kenyatta kwa kuchaguliwa kuiongoza Kenya katika uchaguzi
uliofanyika kwa hali ya amani, utulivu na uwazi wa hali ya juu, hatua
inayoonesha kuwa Wakenya wameamua kuweka maslahi ya taifa lao mbele
kwanza.
Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba kila mgombea wa kiti hicho
cha urais alikuwa mstari wa mbele kuwasisitiza wafuasi wake kutunza
amani, hata pale zilipojitokeza kasoro ndogo ndogo, lengo ni kutorudia
vurugu za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 ambapo watu zaidi ya
1,300 waliuawa na wengine zaidi ya 600,000 kuachwa bila makazi.
Wakenya wameamua, chaguo lao ni Kenyatta na hata tume huru ya uchaguzi
imejitahidi kwa kila jinsi kuweka imani kwamba kura zao
hazichakachuliki.
Tumeshuhudia jinsi IEBC ilivyojaribu kuhakikisha kila kitu kinakwenda
vizuri na kuondosha malalamiko ya hapa na pale, hasa pale teknolojia
mpya ya kuhesabu kura kwa mashine ilivyogoma na hivyo kulazimika
kuzihesabu upya kwa mikono.
Huu ni mfano wa kuigwa na nchi nyingine za bara hili la Afrika ikiwemo
Tanzania, ambazo nyingi zimekuwa na chaguzi zenye mizengwe ya wizi wa
kura, matumizi makubwa ya vyombo vya dola, ubabe na siasa chafu za
kupakana matope.
Lakini kwa wenzetu Wakenya sera za vyama ndizo zimenadiwa na wagombea
kupigiwa kura kutokana na umahiri wao. Tumeona wagombea urais wote nane
waliojitokeza kila mmoja akinadi sera zake na kueleza nini atafanya
akichaguliwa.
Jambo jema na la kutia moyo ni pale matokeo yalipokuwa yakiendelea
kupatikana, baadhi ya wagombea walijitokeza wazi na kukiri kushindwa na
hivyo kuwapongeza wenzao waliokuwa wakielekea kushinda.
Hata baada ya matokeo ya jumla kutangazwa jana, Raila alimtumia salamu
za pongeza Rais mteule Kenyatta licha ya kwamba muungano wao wa Cord
walikuwa katika hatua za kutafakari kupinga ushindi huo mahakamani.
Aliwasihi wafuasi wake kuwa makini, watulivu na wenye subira wakati
huu wakitafakari ni hatua gani za kuchukua. Huu ni mfano wa kuigwa.
Hongera Kenyatta na Wakenya kwa ujumla.
|