|
IMENICHUKUA muda mrefu kujipanga ili niweze kujua kuwa nataka
kuandika nini kuhusu watu hawa; Dk. Harrison Mwakyembe, marehemu Daudi
Mwangosi, Danny Mwakiteleko, Absalom Kibanda na Dk. Stephen Ulimboka.
Nakumbuka ni ndani ya miezi saba nilipokuwa miongoni mwa Watanzania
wachache tulioshiriki kumzika mtangazaji wa Televisheni ya Channel Ten,
Daudi Mwangosi huko nyumbani kwao Tukuyu.
Nakumbuka niliposhiriki mazishi ya aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa
magazeti ya New Habari Corporation, Danny Mwakiteleko, aliyekufa kwa
ajali ya gari akitokea kazini majira ya usiku kuelekea nyumbani kwake
jijini Dar es Salaam. Nilishiriki mazishi yake huko Mwakaleli, Tukuyu.
Nakumbuka baada ya mazishi hayo nilipoitwa na kukutana na wazee wa
Kyela ili waweze kutoa dukuduku lao na shaka kubwa ya ugonjwa
uliomkumba, Mbunge wa jimbo hilo, Dk. Harrison Mwakyembe na
kumsababishia madhara makubwa mwilini na hasa ngozi.
Nakumbuka jinsi wazee hao hao walivyotaka baadaye kufahamu nani
aliyeweza kumdhuru kiongozi wa umoja wa madaktari, Dk. Stephen Ulimboka
na kumuumiza vibaya na hatima ya uhai wake iliweza kuokolewa na
madaktari bingwa nchini Afrika Kusini.
Sasa siwezi kusema tena nakumbuka isipokuwa imetokea tena, aliyekuwa
Mhariri Mtendaji wa magazeti ya Tanzania Daima na baadaye kuhamia
Kampuni ya New Habari na kuwa katika nafasi hiyo ya juu kwenye vyombo
vya habari, Absalom Kibanda naye amefanyiwa unyama mkubwa kama Dk.
Ulimboka.
Si kwamba nataka kuwataja Watanzania hao wachache kwa maana ndio
walioweza kuathiriwa zaidi kwenye moja ya majukumu yao ya kutekeleza
wajibu wao isipokuwa nina hoja ya msingi ya kutaka kufahamu, watu hawa
wamewakosea nini Watanzania?
Ukiacha tukio lililomkuta Dk. Ulimboka kama daktari kitaaluma, narudi
nyuma ili kuweza kuona na kushitushwa na matukio ya wana habari
kuvamiwa, kupigwa, kujeruhiwa na wengine kuuawa katika mazingira yenye
utata, hayo yametokea na hali inazidi kutia shaka zaidi.
Naanzia kwa wanahabari kwa wale wasiofahamu Dk. Harrison Mwakyembe
licha ya kuwa kitaaluma ni mwanasheria pia ni mwandishi wa habari
kitaaluma, kwa hali yoyote ile madhara aliyoyapata hayakuweza kufungwa
na kazi yake anayoifanya sasa kama waziri pia wanahabari wanaomfahamu
waliguswa na mkasa uliompata.
Katika mazingira hayo naweza kuyasukuma mawazo yangu na mawazo ya watu
wengine jinsi tasnia ya habari inavyozidi kuzungukwa na maadui, tena
maadui wakubwa na wenye dhamira mbaya hasa wakiwalenga watu ambao si
rahisi kupona kutokana na ujasiri wao mkubwa walionao wa kupigania na
kutetea masilahi ya nchi hii.
Leo hii, ‘Tuendako’ Absalom Kibanda kama ambavyo amekuwa akiwaelimisha
wananchi kupitia safu yake ya Tuendako amelazwa nchini Afrika Kusini
akiendelea kupatiwa matibabu baada ya kuumizwa vibaya na watu
wanaojulikana, wapo na kwa kuwa wapo si kazi ya wanahabari kuwakamata
hiyo ni kazi ya vyombo vya usalama.
Kuna mambo mawili ambayo kama serikali haitaweza kushtuka haraka na
kutokulala usingizi, misingi ya kihabari itakuwa shakani na viongozi wa
madhehebu ya dini nao hawawezi kufanya kazi zao kwa uhuru na haki ya
kuabudu, waandishi wanauawa, viongozi wa dini nao wanauawa, sasa nini
kifanyike?
Ni dhahiri kwamba matukio ya hivi karibuni yanayoendelea kuvaa sura ya
ukatili na uvunjifu wa haki za binadamu kupita kiasi yanazidi kukua na
kutishia usalama wa mamlaka za kidini na taaluma ya uandishi wa habari
nikiamini katika kusema kweli makundi hayo mawili yapo hatarini.
Lazima tujiulize hawa wanaowatuma watu wawaue mapadri, wachungaji na
masheikh wametoka wapi na wanafanya hivyo kwa nia ipi nzuri, kama hata
wao ipo siku hawatakufa na ni kina nani hao wanaokesha kwenye nyumba za
siri wanamua kuwatuma watu wawavamie waandishi wa habari, wanafanya
hivyo kwa kuwa kazi wanayoifanya nao hawawezi kufa?
Ningeweza kupanga vizuri orodha ya wanahabari mmoja baada ya mwingine
waliokumbwa na madhara, kufa wakiwa wanatekeleza majukumu yao, wanafanya
kazi ya kuwafikishia habari wananchi, kosa lao ni nini kwa nini jamii
inawahukumu wanahabari ambao ndio jicho lao?
Kuumizwa, kupigwa na kuuawa kwa wanahabari haiwezi kuwa fimbo ya
mwisho katika ukombozi wa nchi inayoficha maovu yake chini ya uvungu wa
kitanda, watakufa wachache lakini wengi watajitokeza na kuwa mashujaa
wataweza kufichua uoza unaoitafuna nchi hii taratibu.
Ipo haja vyombo vya usalama vikafanya kazi zake usiku na mchana ili
kuweza kufichua aina hii ya ukatili, mauaji na kuvuruga haki za binadamu
wengine bila sababu, ndiyo maana nauliza, hivi watu hawa wamewakosea
nini Watanzania?
Kuumizwa vibaya kwa Kibanda si mwisho wa uhunzi, kuuawa kwa Mwangosi
si mwisho wa uhunzi, ajali ya Mwakiteleko yenye utata si mwisho wa
uhunzi, madhara aliyoyapata Dk Mwakyembe si mwisho wa uhunzi na madhara
wanayoendelea kuyapata wanahabari sehemu mbalimbali kwa nyakati tofauti
si mwisho wa uhunzi, si usiku, si mchana ipo siku nuru ya haki itaangaza
na kuwaaibisha watu wabaya wanaowadhuru wenzao.
Wanahabari hawapaswi kukata tamaa kwa kuwa penye haki Mungu husimama
na penye uovu lazima wafuasi wa shetani wataangamizwa na hawawezi
kufaulu kila siku, zamu yao itafika na huo utakuwa ndio ukombozi wa nchi
hii, kwani damu inayomwagika haina hatia, ni ya watu wanyonge na
itang’arishwa zaidi na wale wote wanaoitakia mema nchi hii. Mungu
ibariki Tanzania.
|