|
Hali tete inayotikisa taifa sasa katika masuala ya kidini
imewafanya baadhi ya wasomaji wa safu hii kuomba mwandishi airudie kwa
madhumuni ya kuweka msisitizo. Kwa mara ya kwanza uchambuzi huu
ulichapishwa na gazeti hili tarehe 21/11/201. Endelea:
NILIMSIKIA Rais Jakaya Kikwete akitoa hotuba ya ufunguzi wa Bunge la
10. Kuna jambo lilinigusa. Nadhani anataka kutuletea matatizo kwa
kujadili – kwa staili aliyochagua – suala la udini.
Alisema katika kampeni za mwaka huu kumeibuka nyufa za udini na kwamba
yuko tayari kuchukua hatua za haraka kuziba nyufa hizi. Ni hoja nzito,
lakini inazua maswali.
Alipoingia yeye hakukuwa na kelele za udini. Ni kitu gani kinamfanya
yeye aone udini katika siasa baada ya miaka yake mitano Ikulu? Kama
kweli kuna udini, anawezaje kujivua lawama za serikali yake kujenga
mazingira ya kuasisi udini huo?
Mwaka 2005, wakati chati yake kisiasa ikiwa juu, aliyekuwa Askofu
Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Dk. Methodius Kilaini,
alitamka kwamba Kikwete ni chaguo la Mungu.
Wengi tunajua kuwa Askofu Kilaini ni rafiki binafsi wa Rais Kikwete
kwa muda mrefu. Tunajua pia kwamba urafiki huo ulijengwa na Kikwete
kimkakati, na askofu akajikuta ameingizwa katika mtandao wa Kikwete bila
kujua na bila kutaka.
Kwanini, kwa kauli hiyo, iliyotolewa na askofu Mkatoliki, Watanzania
hawakumtuhumu Kikwete wala Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuendekeza
udini, wala hawakumtuhumu Askofu Kilaini kwa kuingiza dini katika siasa?
Ikumbukwe kuwa Rais Kikwete alitumia vema kauli hiyo na nyingine, na
hata baadhi ya makada na wapiga debe wake walitumia mazingira hayo
kujinasibu na ‘misingi na malezi mazuri aliyopewa na Wakatoliki.’ Mbona
hakuna aliyenyoosha mkono kusema hapa kuna harufu ya udini?
Nasema hivi nikijua kwa dhati kuwa timu ya mtandao wa kampeni ilitumia
nguvu nyingi sana kushawishi maaskofu wa madhehebu kadhaa ya dini
yamuunge mkono. Namjua hata aliyetumwa kujenga mazingira mazuri kwa
baadhi ya maaskofu Wakatoliki ‘wasimpige mawe’ Kikwete kabla hata
hajajitokeza kugombea.
Walifanya hivyo wakitambua kuwa nguvu ya kanisa ni kubwa na kwamba
kama ingetumika dhidi yao wasingepata watakacho. Bahati nzuri, kwa nguvu
ya ushawishi waliotumia, kanisa halikumpiga vita. Kwanini hakuna
aliyezuka kuzungumzia udini katika siasa za Kikwete?
Ikumbukwe pia, Kikwete ndiye aliyenadi sera za CCM, ikiwamo ya
kuwaahidi Waislamu kuwapatia ufumbuzi wa suala la Kadhi Mkuu, ambalo
limeleta sokomoko kwa miaka mitano yote. Mbona Watanzania hawakusema
Kikwete anaendekeza udini katika siasa?
Ninachokumbuka haraka haraka, mwanzoni kabisa mwa utawala wa Rais
Kikwete, yupo Mtanzania mmoja, Nathaniel Limu, aliandika kuhoji uteuzi
wa viongozi waandamizi ndani ya serikali ya Kikwete, ambao wengi
walikuwa Waislamu.
Kutokana na ukali wa mwandishi Limu, timu ya Rais Kikwete, kupitia kwa
swahiba wake, Rostam Azizi, ilimuomba aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa
Habari Corporation, Salva Rweyemamu kujibu hoja za Limu.
Makala zote mbili, ya Limu na ya Rweyemamu ziliandikwa katika gazeti
hili; moja ikikosoa uteuzi wa Rais Kikwete na kuuita wa kidini, na
nyingine ikijibu na kutetea uteuzi huo kwamba ulizingatia sifa za
walioteuliwa, na hata kuorodhesha majina na nafasi za vigogo Wakristo
serikalini. Kwanini Kikwete hakujitokeza kukemea udini?
Yapo magazeti pia ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakiandika habari na
makala za udini, na yakihusisha dini za watu na uongozi wa vyama kadhaa
vya siasa, hata kwa kuvitaja majina. Serikali iliyosajili magazeti hayo
haijawahi kuvichukulia hatua kwa miaka mitano.
Na hata katika kampeni za mwaka huu, magazeti hayo yaliendelea
kuandika habari zinazowataja baadhi ya wagombea kuwa ni makafiri, na
kwamba wasichaguliwe. Kwanini serikali imekaa kimya hadi baada ya
uchaguzi?
Si hilo tu. Hata katika baadhi ya nyumba za ibada, wamesikika viongozi
wa kidini wakiwaomba wafuasi wa madhehebu yao wasiwachague makafiri. Na
wengine walidiriki kumpigia debe Rais Kikwete katika nyumba hizo hizo
za ibada. Kwanini hakujitokeza kukemea kauli hizo wakati ule?
Inafahamika pia kwamba miongoni mwa mbinu chafu za kampeni za chama
chake mwaka huu, ni matumizi ya ujumbe mfupi wa simu za mkononi, dhidi
ya mgombea urais kupitia CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, kwa misingi kwamba
ni kafiri.
Rais Kikwete alishindwa kuwazuia wanachama wake kufanya kampeni hizo.
Na walipogundua kwamba kampeni ya kidini dhidi ya Dk. Slaa ingeweza
kuwafanya waamini wa upande mwingine nao wajihami, wakaanza propaganda
za kumshutumu kwamba anatumia makanisa kufanya kampeni!
Kilichomzuia kuwazuia wafuasi wake kufanya kampeni za kidini kwa
kutumia sms ni kitu gani? Mbona hakujitokeza kukemea baadhi ya misikiti
na makanisa wakati wa kampeni? Anapata wapi leo nguvu ya kukemea matawi
wakati amepalilia mizizi ya tatizo hilo hilo?
Lakini pia anaposema kwamba uchaguzi huu umefanyika kwa misingi ya
udini, anataka kusema kwamba hizo kura milioni tano alizotangazwa kupata
ni za watu wa imani moja (Waislamu) pekee? Anataka kusema kwamba kama
Wakristo wangepiga kura za udini Dk. Slaa angepata kura milioni mbili
zilizotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)?
Au anataka kusema kwamba anajua zaidi, kwamba Wakristo walimchagua
Mkristo, na Waislamu walimchagua Mwislamu, lakini kura zilizopigwa sizo
zilizotangazwa?
Ipo pia hoja iliyotolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible
Fellowship. Mwaka 2000 alimpigia debe mgombea urais kupitia TLP,
akimpinga rais aliyekuwa madarakani, Benjamin Mkapa.
Mbona hakuna aliyehoji udini katika siasa? Ni kitu gani kinawafanya
watawala wafikirie kwamba kwa kuwa mwaka huu Askofu Kakobe ameendelea
kuwapinga, alipinga dini zao si udhaifu wao wa uongozi?
Kama ambavyo baadhi ya watu wamejadili, watawala wamekuwa na tabia ya
kuchomeka hoja za ajabu ajabu kama nia ya kuwaondoa Watanzania katika
mijadala mizito ya kitaifa.
Na sote tumeshuhudia mbinu yao hii katika kampeni za uchaguzi mwaka
huu. Hata baadhi ya vyombo vya habari vilivyomuunga mkono Rais Kikwete
na CCM, jambo ambalo si kosa kisera vilishindwa kumjenga mtu wao,
vikaishia kutafuta namna ya kubomoa washindani wake, hasa Dk. Slaa.
Lakini havikujua kwamba udhahifu wa kiuongozi wa Rais Kikwete wa miaka
mitano iliyopita, usingeweza kuboreshwa au kutetewa kwa mashabulizi
dhidi ya washindani wake.
Na tayari baadhi yetu tunajua mikakati yao ya kipropaganda ya kutumia
mashambulizi dhidi ya kina Dk. Slaa na wenzao kuelekea 2015. Tunasubiri
kuona ufundi utakaozitengeneza!
Lakini mwandishi mmoja, Richard Mgamba, amehoji: “Tanzania kuna udini
upi? Nani mdini? Ukiomba Mahakama ya Kadhi kosa, ukiomba OIC dhambi;
askofu akikosoa serikali tayari kuna udini. Hivi kweli nchi hii kuna
udini au ni uoga wa viongozi wetu? Huko mtaani mbona tunaishi salama
Wapagani, Waislamu na Wakristo? Huo udini wanauona watu wa usalama tu na
bwana mkubwa? Jamani tusiingie kwenye mitego ya kipuuzi.
Udini kama ungekuwepo hapa, leo hii huko mitaani kwetu kungekuwa
hakukaliki. Kama kuna Mkristo fulani mwendawazimu haina maana Wakristo
wote wanafikiria hivyo, na pia kama kuna Mwislamu mmoja kichaa, haina
maana Waislamu wote wako hivyo.
“CCM inadai ina wanachama milioni 5 nchi nzima. Imepata kura milioni
5.8 mwaka huu. Ina maana imepigiwa kura na wasio na vyama laki nane.
Mwaka 2005 ilipata kura milioni 8.9, sasa ina maana hizo kura
zilizopotea milioni 3.1 ni za Wakristo?
“Hivi mbona hatujiulizi uhalali wa watu milioni 19.5 kujiandikisha
kupiga kura, kisha wanaojitokeza ni milioni 8.5 tu, hao milioni kumi na
moja wako wapi? Hawa wote walikufa, au walisafiri au waliamua kutokupiga
kura ghafla?”
Sasa Rais Kikwete atuambie. Amechaguliwa na Waislamu milioni tano? Au
amechaguliwa na wana CCM milioni tano? Au amechaguliwa na Watanzania
milioni tano?
Na huu ndio uongo wa takwimu za watawala. Kama wana CCM ni milioni
tano, na rais anachaguliwa na watu milioni tano, basi amekosa uhalali wa
kutawala Watanzania takriban milioni 45.
Na kama amechaguliwa na Waislamu milioni tano, basi maana yake CCM ni
chama cha watu wa imani moja tu, jambo ambalo si kweli. Na kama miongoni
mwa waliompigia kura Kikwete wamo Wakristo, basi hoja yake ni potofu.
Maana natambua kuwa idadi ya Wakristo nchini inazidi milioni tano.
Vile vile idadi ya Waislamu ni kubwa kuliko milioni tano. Kwa mujibu wa
ensaiklopidia ya Wikipedia, hadi mwaka 2007, idadi ya Waislamu na
Wakristo nchini inazidiana kidogo, na wote wako kati ya asilimia 30 na
40 ya Watanzania wote.
Kama Waislamu wote wangehamasishwa rasmi kumchagua Mwislamu mwenzao,
na kama wangekubali wote, Kikwete na Profesa Lipumba wangegawana kura.
Na kama Wakristo wangekuwa wamehamasishwa rasmi kumchagua Mkristo
mwenzao na wakakubali, kura za Dk. Slaa zingekuwa nyingi kuliko milioni
tano alizopata Kikwete.
Lakini suala la msingi analopaswa kujiuliza Kikwete ni hili. Hoja hii
ya udini aliirithi kutoka kwa Rais Mkapa au imeota mizizi katika miaka
mitano ya utawala wake?
|