|
MITAANI kwetu tumewapachika jina la ‘koko’ mbwa wote wasioonesha
ukali, iwe mchana au usiku, hata wanapobweka hakuna mwenye kuwaogopa.
Kimsingi mbwa wa aina hii hudharauliwa sana mitaani, hawa pia hawana
matunzo mazuri kutoka kwa wamiliki wao, maana kila uchwao huzurura huku
na huko kujitafutia chakula na maji.
Mbwa koko humuogopa mhalifu, akijitutumua huishia kuwasumbua watoto wadogo. Hivi ndivyo ilivyo TAKUKURU.
Taasisi hiyo huwakamata dagaa wa rushwa na kuwaacha papa na nyangumi ambao ndio wanaoitafuna nchi kwa kiasi kikubwa sana.
Leo hii TAKUKURU imegeuka mbwa koko licha ya kupewa meno ya kuwang’ata
wala rushwa, taasisi hii nayo imekuwa miongoni mwa watuhumiwa wa
kupokea rushwa.
Rushwa wanayoipata au uoga walionao dhidi ya Papa na Nyangumi
vinaiondolea hadhi taasisi hii inayotumia mamilioni ya fedha za walipa
kodi kujiendesha.
Juzi nimesikia TAKUKURU imewatia mbaroni walimu wawili Faustin Robert
na Josephat Mwasote wa Shule ya Sekondari ya Forest iliyopo mkoani Mbeya
kwa tuhuma ya kudai na kupokea rushwa ya shilingi mia tano (500) kutoka
kwa wanafunzi wao.
Kamanda wa TAKUKURU mkoani humo, Daniel Mtuka, alisema walimu hao
wanatuhumiwa kwa kuunda mtandao au mradi wa kuvuna fedha kutoka kwa
wanafunzi wanaofanya makosa.
Mwanafunzi anayefanya kosa hutakiwa kupewa adhabu ya viboko au
nyingine yoyote lakini kama akitoa sh 500 adhabu husika humuepuka.
‘Kwenye udhia tumbukiza rupia’ ndivyo walivyofanya walimu.
Mwanafunzi asiyetoa kiasi hicho cha fedha hupewa adhabu kali
zinazotolewa katika chumba maalumu walichokipachika jina la
‘Guantanamo.’
Guantanamo ni jela ya Marekani iliyopo nchini Cuba inayosifika kwa
mateso makali kwa kila wafungwa au mahabusu waofikishwa hapo.
Binafsi nimesikitishwa na kitendo cha walimu wale, maana walichokuwa
wakikifanya ni kinyume cha maadili ya taaluma yao, pia ni kosa la jinai.
Walimu wale wanajenga taifa a wala rushwa, mwanafunzi aliyelelewa
katika maadili ya kutoa rushwa ili asamehewe au apate huduma fulani
kamwe hataichukia rushwa. Huyu atakuwa mtoa na mpokea rushwa jasiri.
Pamoja na kulaani walichokifanya walimu hao bado nina shaka na uwezo
wa TAKUKURU katika utendaji kazi, hawa ni wepesi zaidi kuwashughulikia
wanyonge kuliko vigogo wanaoiba kwa kutumia kalamu.
TAKUKURU ilipoomba ipewe meno na baadaye ilipopewa nilitarajia
ingewang’ata watoa na wapokea rushwa wote bila kujali wadhifa au uwezo
wa kifedha wa mhusika.
Kwa bahati mbaya baadhi ya watendaji wa TAKUKURU wamekuwa sehemu ya
kupokea au kulazimisha rushwa. Wameigeuza ofisi ya umma kuwa mradi
binafsi.
Hawa wanafurahia zaidi wanaposikia tajiri au kigogo fulani kakumbwa na
tuhumu za kutoa au kupokea rushwa, wakifika huko hudai wapewe chochote
kwa lengo la kutolifikisha suala husika katika ngazi za kisheria.
Kilio cha TAKUKURU huko nyuma kilikuwa meno lakini baada ya kupewa
hawaonekani kuyafanyia kazi hasa kwa matajiri, vigogo wa serikalini na
taasisi za umma.
Najiuliza, yako wapi meno waliyopatiwa? Hivi waliotoa meno kwa TAKUKURU waliyachunguza meno yao kama ni mazima au yameoza?
Najua meno yaliyooza kamwe hayawezi kuwa na ufanisi unaotakiwa. Kama
TAKUKURU walipewa meno ya aina hiyo kwanini viongozi wake waliyakubali
ilhali wakijua hayataweza kuwasaidia?
Chombo hiki sasa kinataka kiwe na mahakama yake itakayoshughulikia
masuala ya rushwa, hoja hii wanaishibisha kuwa mahakama za kawaida
zimekuwa kikwazo kwao.
Wanadai zinachelewesha kesi, mimi sikubaliani na hoja ya TAKUKURU,
hawa wakipewa mahakama yao watakuwa wala rushwa zaidi. Watawaonea,
kuwakandamiza watu kama ilivyokuwa ikifanyika huko nyuma kwa polisi.
Polisi walikuwa wanakamata wahalifu, wanachunguza na wanaandaa
mashitaka. Hapa watu walikuwa wakilia zaidi kwa kesi za kubambikiziwa
lakini tangu Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), ikabidhiwe
jukumu la kuandaa mashitaka angalau mambo yamebadilika.
Kwa hali tunayokwenda nayo sina shaka ipo siku TAKUKURU watapigwa mawe
na wananchi kama wataendelea na utaratibu huu wa kuwakamata walimu
wenye kuchukua sh 500 huku wakiwaacha mafisadi wanaokwapua rasilimali za
taifa kwa kutumia kalamu zao.
Mikataba mbalimbali ihusuyo rasilimali za taifa imetawaliwa na rushwa,
TAKUKURU wakipewa kazi ya kuichunguza hutoa majibu ya kutokuwapo na
rushwa, hili si geni, si tumeliona katika Richmond.
Wananchi sasa wana mahakama zao, porojo za serikali pamoja na vyombo
vyake zimewachosha. Wahalifu wakikamatwa mitaani wananchi wameamua
kuwahukumu hata kama ni kinyume cha sheria.
Kwa hali inavyokwenda, kuna kila dalili wananchi wakaanza kuwahukumu
wala rushwa bila ya kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kama
wawafanyavyo vibaka wanaokwapua simu.
Maeneo yaliyokubuhu kwa rushwa yanajulikana, huduma kwenye zahanati,
hospitali na vituo vya afya hazitolewi bure kama inavyotakiwa,
kuunganishiwa umeme inahitajika rushwa, kuajiriwa kunahitaji rushwa.
TAKUKURU hawayaoni maeneo haya?
TAKUKURU ilikuwepo kwenye chaguzi za vyama vya siasa ambako rushwa
zilikuwa nje nje lakini mwisho wa siku waliokamatwa ni ‘dagaa’, tena
wachache. Papa na nyangumi wa kutoa rushwa waliendelea kuogelea kwenye
bahari ya rushwa.
Wananchi wanashangazwa, inakuwaje TAKUKURU inashindwa kesi ilhali
ilishiriki kikamilifu katika ‘mitego’ na hatimaye kuandaa vidhibiti
alivyokamatwa navyo mhusika?
TAKUKURU wenyewe hawaonekani kusikitikia kushindwa kwenye kesi
walizozichunguza, huu ni udhaifu na kama chombo hiki kikiendelea hivi ni
afadhali kivunjwe kiundwe kingine kitakachowajibika ipasavyo. Kwangu
chombo hiki hakina faida.
|