|
WAKATI akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani -
DW kuhusu utete wa usalama unaowakumba wanahabari Tanzania, na kutakiwa
ataje hatua za makusudi zinazochukuliwa na serikali kuwaondolea
wanahabari zahama hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanueli Nchimbi,
alitamka kwa kujiamini kwamba serikali inalo jukumu la kuhakikisha
usalama wa kila raia na si kwa wanahabari peke yao.
Nchimbi aliongeza kwamba si kweli kuwa wanahabari ndilo kundi pekee
ambalo usalama wake umegubikwa na utata katika jamii ya Watanzania.
Akasema mtu akitakiwa kutaja matukio yanayodhihirisha kuwa usalama wa
wanahabari umepotea hayawezi kufika hata matukio matano. Kwa mtazamo
wake mpaka sasa wanahabari wako salama! Pengine wafe nusu yao ndipo
atalipa uzito suala hilo!
Lakini hata hivyo Nchimbi hakulitaja kundi lingine katika jamii ya
Watanzania ambalo taaluma yake inalifanya kujikuta limepoteza usalama
wake kama ilivyo kwa wanahabari. Maana kwa kuitia uzito hoja yake ya
kwamba si wanahabari peke yao wanaoonekana kupoteza usalama wao kutokana
na kuihudumia vilivyo taaluma yao, angeongeza walau makundi mawili
yaliyo katika mkumbo mmoja kama mfano. Pengine angesema wahandisi au
wahasibu.
Lakini kushindwa kufanya hivyo ni kama Nchimbi kakiri kwamba usalama wa wanahabari kwa sasa uko hatarini kama inavyojionesha.
DW ilimhoji Nchimbi kufuatia tukio la kinyama la kutekwa na kujeruhiwa
kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Absalom Kibanda, ambaye
pia ni mhariri mtendaji wa Kampuni ya New Habari.
Tukio hilo ambalo Nchimbi anataka kulijengea hoja ili lionekane ni la
kawaida katika jamii ya Watanzania, limekuja baada ya matukio kadhaa ya
mashambulizi yaliyolengwa kwa makusudi kwa wanahabari.
Matukio ya karibuni yakiwa ni pamoja na kuvamiwa kwa ofisi za gazeti
la Mwanahalisi, ambako mhariri mtendaji wa gazeti hilo, Saeed Kubenea,
pamoja na mshauri wa taaluma, Ndimara Tegambwage, walijeruhiwa na watu
wasiojulikana.
Mbali na tukio hilo likafuatia la kushambuliwa kwa mwanahabari, Daudi
Mwangosi na watu wanaojulikana, tena wa vyombo vya usalama wa raia,
ambapo mwanahabari huyo aliyekuwa anatekeleza majukumu yake alipoteza
maisha baada ya kulipuliwa na bomu lililoelekezwa tumboni kwake chini ya
usimamizi wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa Iringa, Michael Kamuhanda.
Baada ya tukio hilo la kijijini Nyololo, Mfindi, Iringa, likafuatia la
mwanahabari Shabani Matutu kuvamiwa nyumbani kwake, Kunduchi Machimbo,
nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, na kikosi cha wanausalama
waliomjeruhi kwa risasi begani kwa visingizio visivyo na mashiko.
Matukio hayo yasiyolenga kwenye kitu kingine zaidi ya uhai wa mtu
tunawezaje kuyachukulia ni ya kawaida tukiwa tumeyafananisha na matukio
ya vibaka?
Tulizoea ujambazi unaolenga kwenye mali, lakini unaolenga tu kwenye
uhai wa mtu tunawezaje kuuita ni wa kawaida? Mali inaweza ikaporwa na
ikapatikana nyingine, lakini uhai unapoporwa unawezaje kupatikana
mwingine? Je, Nchimbi tukubali hii ni kawaida?
Na kwanini ujambazi huu uchague taaluma? Tuuchukulie unakuja kama
ajali, lakini mara zote ajali hizo ziwakute wanahabari tu? Dukuduku
langu lingepungua kama mashambulizi haya ya kinyama yangekuwa
yanaelekezwa kwa watu wa taaluma mbalimbali bila kuiandama moja tu.
La muhimu ninalotaka kukumbusha na kuhoji ni kwamba Waziri Nchimbi
anayo dhamana ya mambo ya ndani ya nchi yetu. Chini yake ndiko kuna
Jeshi la Polisi ambalo lipo kuulinda usalama wa raia, na kwahiyo jeshi
hilo likajulikana kwa kifupi kama Usalama wa Raia.
Kutokana na kuwepo jeshi hilo wananchi wanapaswa kutembea wakijidai
bila hofu wakijivunia uwepo wake. Ndiyo maana wanalipa kodi ili pamoja
na mambo mengine, zihakikishe chombo hicho kinabaki imara kuwahakikishia
usalama wao.
Kwa hiyo kinachotarajiwa na wananchi kutoka kwenye chombo hicho ni
habari za kuyazima matukio yoyote ya uhalifu yanayokuwa yamepangwa
kutekelezwa na wahalifu dhidi ya raia wema na mali zao.
Jambo la kusikitisha ni kwamba mambo yamekuwa kinyume chake katika
siku za karibuni hapa nchini. Uhalifu limegeuka jambo la kawaida hapa
kwetu. Wananchi wanadhurika na wengine kupoteza mali zao au vyote
viwili.
Chombo kilichopaswa kuwahakikishia usalama, wao na mali zao,
kinajigeuza cha kufanya uchunguzi kana kwamba hakihusiki na ulinzi wa
usalama!
Kila baada ya tukio la uhalifu chombo kilichopaswa kuhakikisha uhalifu
hautendeki ndicho kinajipa jukumu la kuchunguza kwanini umetendeka na
umetendekaje. Wakati uhalifu umeishafanyika na madhara yasiyoponyeka
yameishatokea, chombo cha usalama kinahangaika na uchunguzi!
Na yumkini chombo cha kulinda uhalifu usitokee kinapojigeuza cha
kuchunguza, uhalifu unapata mvuto sababu unakuwa hauna kinga, utafanyika
ili baadaye ukachunguzwe.
Swali la muhimu la kujiuliza ni kwamba Jeshi la Polisi ni kwa ajili ya
kuulinda usalama wa raia au ni la kufanya uchunguzi kila baada ya
usalama wa raia kutibuka?
Je, wananchi wanapaswa waishi kwa kuutegemea usalama wao na mali zao
au uchunguzi unaofanyika baada ya kuwa wamedhurika? Tulitegemee Jeshi la
Polisi katika lipi? Kuulinda usalama wetu na mali zetu au kutufanyia
uchunguzi wakati baadhi yetu wamepoteza mali na hata maisha?
Absalom Kibanda ni kijana aliyekuwa buheri wa afya kabla ya usalama
wake kuyeyuka na kujikuta ameangukia mikononi mwa majahili. Kwa sasa
tayari afya yake ni mgogoro, akipona hawezi tena kurudia hali yake ya
kawaida, na si ajabu akawa chongo kulingana na mashambulizi aliyofanyiwa
na majahili hayo. Ni jambo linalouma sana.
Lakini tunaambiwa kwamba polisi wamejipanga kufanya uchunguzi wa “kufa
mtu”! Je, baada ya uchunguzi huo wa nguvu Kibanda atarudia hali yake ya
kawaida? Jicho lake litapona?
Kilichopaswa kufanywa na polisi ni kutumia walau moja ya mia moja ya
nguvu inayotumika kufanya uchunguzi ili kuulinda usalama wake, sio
kufanya uchunguzi wakati kaishapoteza jicho na meno.
Usalama wa raia si kusubiri raia adhurike au afe kusudi Jeshi la
Polisi lionyeshe manjonjo yake katika uchunguzi, kinachopaswa kuangaliwa
ni usalama kwanza. Raia asidhurike wala kufa katika mazingira
yanayoweza kuepusha vitu hivyo.
Mfano, mwandishi mmoja anayeishi nchini Scotland, majuzi tu katueleza
jinsi vyombo vya usalama vya wenzetu vinavyofanya kazi kwa ufasaha.
Vyenyewe vinafanya uchunguzi kabla ya tukio lenye madhara na kuliepusha.
Alieleza jinsi polisi walivyokwenda nyumbani kwake alfajiri na
kujitambulisha kisha wakamweleza kuwa anafuatiliwa na watu wasio wema
kwake ili akachukue tahadhari. Polisi hao hawakutaka mtu huyo adhurike
kwanza ndipo waanze uchunguzi wa nini kimemsibu.
Kwahiyo hata hapa kwetu ningetegemea polisi wamfuate Kibanda, au walau
kumpigia simu, kumweleza kuwa usalama wake ulikuwa hatarini kusudi
achukue tahadhari. Hapo ningeamini kwamba vyombo vyetu vya usalama kweli
viko kazini na vinaitumia kwa umakini intelijensia yake kwa manufaa ya
wananchi. Lakini sio ile intelijensia inayotumika tu kuzuia mikutano ya
hadhara ya vyama vya upinzani.
Nimalizie kwa kukumbusha ya enzi za nyuma. Wakati wanahabari kwa sasa
wanaonekana ni maadui kwa baadhi ya watumishi wa umma hasa walio katika
vyombo vya dola, mfano kama RPC wa Iringa, Michael Kamuhanda, miaka ya
nyuma walikuwa vipenzi vya watu kama hao.
Katika Vita ya Kagera, 1978 – 79, Jenerali David Msuguri, akiwa
brigedia wakati huo, aliwapenda sana waandishi wa habari waliokuwa
wanaripoti mwenendo wa vita kutokea uwanja wa mapambano kiasi cha
kuwaita makomandoo wake.
Hiyo ilitokana na wanahabri kutaka kufika katika kila eneo la tukio
ili wakapate cha kuuhabarisha umma katika uhalisia wake. Wanahabari
walifika hata mahali ambapo askari hawakuona umuhimu wa kufika zaidi ya
kutuma salamu za makombora.
Wanahabari walifanya hivyo kwa kujitoa mhanga mpaka Msuguri akaona
wanafaa kuitwa makomandoo. Walikuwa wanatimiza jukumu lao kwa moyo
mmoja. Ukomandoo huo bado upo na pengine unaongezeka, lakini je, kwanini
kwa sasa hauthaminiwi?
Nakutakia kupona kwa haraka ndugu yangu Komandoo Absalom Kibanda, pole
sana. Wahaya wanasema “Bishanga abashaija”, yaani hayo huwakuta
wanaume.
|