CCM yawavumilia mafisadi lakini si wenye fikra mbadal






BARAZANI KWA AHMED RAJAB

UAMUZI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa kumfukuza chamani Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe samaki, Mansoor Yussuf Himid ni uamuzi uliokuwa ukitarajiwa tangu Ijumaa iliyopita baada ya mwanasiasa huyo kuchambuliwa katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM.


Hata hivyo, wakati mmoja kuna waliodhani kwamba angeweza kunusurika baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, kuwasihi wanachama wenzake wavumiliane alipokihutubia kikao cha Kamati Kuu ya CCM. Hiyo ilikuwa nasaha ya busara.


Lakini kutofuatwa kwa nasaha hiyo kunazusha maswali ambayo majibu yake yanaweza kutuashiria mengi kuhusu majaaliwa ya CCM ikiwa imebaki miaka miwili tu kabla ya uchaguzi mkuu ujao.


Maswali yenyewe yanahusu uhalisi wa msimamo wa Kikwete, nia yake na nguvu zake ndani ya CCM.


Swali la kwanza ni iwapo Kikwete kweli alikuwa na msimamo wa dhati alipowasihi wenzake wavumiliane.Au alikuwa akibabaisha tu?


Ikiwa alikuwa akibabaisha kwa makusudi ni kipi kilichomzuia asionyeshe ujasiri wa kuchukua msimamo madhubuti kwa kuwakemea wale wasiovumilia fikra mbadala ndani ya chama na hivyo kuwa kitisho kwa uhuru wa kufikiri na wa mawazo ndani ya chama?


Swali jengine ni hili: ikiwa alikuwa mkweli na alikuwa na nia ya kutaka pawepo na uvumilivu wa fikra tofauti ndani ya chama chake ilikuwaje hata asisikilizwe na akashindwa? Nani na nani waliomzidi nguvu ndani ya CCM?


Tunavyofahamu ni kwamba Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana,

www.hakileo.blogspot.comaliudhiwa sana na barua aliyoandikiwa karibuni na Mansoor.


Katika barua hiyo inayoelezewa na waliokaribu na Kinana kuwa ni ya usafihi Mansoor alimwambia huyo Katibu Mkuu wa CCM kwamba hakuwa tayari kuubadili msimamo wake kuhusu muundo wa Muungano na kwamba yuko tayari kufukuzwa chamani au hata kunyongwa.


Mansoor pia anatuhumiwa kuwa mfedhuli kwa vile inasemekana kwamba alikuwa akikataa kuhudhuria vikao kadhaa vya CCM vilivyomwita kumjadili.


Chama cha Mapinduzi kilianza mchakato wa kumshughulikia Mansoor katika kipindi cha takriban mwaka sasa tangu pale ilipobainika wazi kwamba mwanasiasa huyo mshupavu ana msimamo unaokinzana na ule wa chama chake kuhusu mustakabali wa Zanzibar.


Mansoor anataka Zanzibar iwe na mamlaka kamili katika Muungano wa aina mpya utaokuwa juu ya msingi wa Mkataba badala ya Katiba.


Wiki iliyopita kikao cha Kamati maalumu ya CCM/Zanzibar, kikiwa chini ya uwenyekiti wa Rais Ali Mohamed Shein ambaye ni makamu mwenyekiti wa CCM, kilipendekeza kwamba Mansoor afukuzwe chamani kwa shtuma za kwamba alikiuka maadili ya chama hicho. Aidha, alishutumiwa kwa kutokuwa mtiifu kwa CCM kwa mwendo, tabia na vitendo.


Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Magharib, Zanzibar, ikaamua kuwa Mansoor afukuzwe kutoka CCM.


Majadiliano yalikuwa makali katika kikao hicho na inasemekana kwamba wajumbe wa kamati hiyo walipapurana. Uhasama huo wa ndani unatishia hadi leo kuigawa CCM/Zanzibar katika mapande mawili. Waliojitolea kumtetea Mansoor walihoji kwamba si yeye pekee aliyekuwa akitoa maoni kuhusu Muungano yenye kupingana na msimamo rasmi wa CCM wa kutaka muundo wa sasa wa Muungano wa serikali mbili uendelee.


Hata hivyo, watetezi wa Mansoor hawakuweza kufua dafu na pendekezo la kumfukuza liliwasilishwa na Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Magharib, Zanzibar, mbele ya Kamati Kuu ya Chama mjini Dodoma.


Huko suala la Mansoor lilijadiliwa lakini mara tu kikao cha Kamati Kuu kikapendekeza kwamba suala hilo liamuliwe na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC). Na Jumatatu mchana ndipo hiyo Halmashauri Kuu ya Taifa ilipoamua kumfukuza Mansoor.


Katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari baada ya uamuzi huo kuchukuliwa Nape Nnauye, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa NEC alisema kwamba baadhi ya shutuma dhidi ya Mansoor ni pamoja na:
Kushindwa kusimamia malengo ya CCM na kutekeleza masharti ya uanachama.
Kushindwa kutekeleza wajibu wa mwanachama na kukiuka maadili ya kiongozi wa CCM.
Kuikana Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010-2015 na kuisaliti CCM.


Habari zilizovuja kutoka vikao vyote vya wiki iliyopita vya CCM huko Dodoma zimezusha tetesi kwamba tayari nyufa za mpasuko ndani ya CCM Taifa zinaonekana kwa wenye kuzitafuta.


Mara baada ya uamuzi huo wa kumfukuza, Mansoor hakutoa tamko rasmi wa akisema kuwa ni mapema kusema lolote kwa sasa. Ni mapema pia kuweza kuagua kwa sasa ni viongozi wangapi wengine wa CCM/Zanzibar wataokuwa na ujasiri kama wa Mansoor wa kujitoa kadamnasi na kutetea mfumo wa Muungano wenye kwenda kinyume cha sera ya CCM.


Kadhalika ni mapema mno kuweza kujua ni lini mpasuko ndani ya CCM/Zanzibar utadhihirika wazi, utadhihiri vipi na utakuwa wa ukubwa gani. Hata hivyo, hakuna anayekataa kwamba hali ya mambo si shuwari ndani ya CCM/Zanzibar, chama ambacho kwa sasa kinaonyesha kuwa mikononi mwa wahafidhina wenye kupinga mageuzi.


Namna wahafidhina hao wanavyokiendesha chama ni kana kwamba bado tungali katika enzi za mfumo unaoruhusu chama kimoja tu halali cha siasa. Ndio maana fikra zenye kuridhia pawepo mageuzi zinapingwa vikali na wenye kuhodhi madaraka ya chama hapa Zanzibar. Wanachochelea ni kupoteza ulwa wao na njia za kujaza matumbo yao. Wanaongozwa na ubinafsi na si uzalendo kama alivyo Mansoor.


Wao wahafidhina hawakumchimba Mansoor kwa sababu tu anataka muundo wa Muungano ubadilike. Pia wanamchimba kwa sababu ni mtetezi wa umoja wa Wazanzibari na wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyozaliwa na Maridhiano.


Yeye mwenyewe ni mmoja wa wajumbe sita wa Kamati ya Maridhiano iliyo chini ya uwenyekiti wa Hassan Nassor Moyo, mmoja wa viongozi wa Zanzibar waliokuwa karibu sana na Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa mwanzo wa Zanzibar.


Wahafidhina wanaipinga serikali hiyo na hawataki kamwe pawepo na mashirikiano au ubia baina ya Chama cha Wananchi (CUF) na CCM. Ni wakali dhidi ya ushirikiano huo kama walivyo wakali dhidi ya muundo wa Muungano utaoipa Zanzibar mamlaka kamili.


Kinachoshangaza ni kwamba viongozi kadhaa wa CCM/Bara wamekuwa wakitoa maoni kuhusu Muungano yanayotafautiana na sera ya CCM. Kuna wenye kutaka pawepo Muungano wenye serikali mbili na kuna hata wenye kutaka pawepo na serikali moja tu ya Jamhuri ya Muunganoya Tanzania. Hakuna hata mmoja wao aliyefukuzwa chamani — hatua ambayo ni adhabu ya mwisho ndani ya CCM. Kwa hakika, hakuna hata mmoja aliyekemewa.


Wazanzibari wanasema kwamba hatua ya kufukuzana CCM ni hatua waliowekewa wanachama kutoka Zanzibar tu. Ni wao tu wanaoshikishwa adabu wakionekana wanakiuka mipaka ya sera za chama chao.


La kushangaza zaidi na kutisha ni kuwaona mafisadi wakivumiliwa ndani ya CCM ingawa wanakwenda kinyume cha maadili asilia ya chama hicho, maadili yenye kupinga rushwa na kila aina ya vitendo vya kifisadi. Imekuwa kama hakuna anayeweza kuwagusa mafisadi hao licha ya hasara walioitia Tanzania ya mabilioni ya dola za Marekani.

-CHANZO http://www.raiamwema.co.tz/
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company