JK usiingizwe mkenge, Muswada huu ni majanga

HABARI ZETU


WWW.HAKILEO.BLOGSPOT.

Rais Jakaya Kikwete 


Posted  Alhamisi,na GAZETI LA MWANANCHI
KWA UFUPI
  • Wakati wote huo, Naibu Spika ambaye alikuwa akiendesha kikao hicho alikaa kimya bila kuwataka wabunge hao wa chama chake kujielekeza katika kujadili Muswada huo.

Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria ya Katiba ulipitishwa Bungeni wiki iliyopita na kinachosubiriwa sasa ni Rais Jakaya Kikwete muda wowote kuutia saini kuwa sheria au kuukataa. Tunatambua fika ukweli kuwa, kwa mara nyingine katika kipindi cha mwaka mmoja, Rais ameingizwa majaribuni katika namna ambayo atapaswa tena kutumia umakini na busara zake ili kukwepa kuingia katika mtego wa kikatiba uliotegwa na wabunge wa chama chake cha CCM.
Tunasema hivyo kwa sababu Muswada huo muhimu kwa mustakabali wa nchi yetu ulipitishwa na Bunge pasipo kujadiliwa. Wabunge wa upinzani waliposusia mjadala wa Muswada huo na kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge kutokana na tofauti zilizojitokeza baina yao na Naibu Spika, Job Ndugai, ilitegemewa kwamba wabunge wa CCM waliobaki Bungeni wangewatendea haki wananchi kwa kuujadili Muswada huo kwa kina na umakini mkubwa kwa kutanguliza mbele masilahi ya taifa letu
.
Lakini kwa mshangao wa wengi, hasa wananchi waliokuwa wakifuatilia matukio hayo katika televisheni, wabunge hao hawakuujadili Muswada huo na badala yake wakajikita katika kuporomosha matusi ya nguoni, kutoa kejeli na kuwapiga vijembe wabunge wa upinzani kutoka vyama vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi waliosusia mjadala huo. Wabunge wa CCM, wakiwamo baadhi ya mawaziri walisimama mmoja baada ya mwingine kutoa kauli za kibabe na kusema Muswada huo lazima upitishwe kutokana na wingi wao katika Bunge hilo.
Wakati wote huo, Naibu Spika ambaye alikuwa akiendesha kikao hicho alikaa kimya bila kuwataka wabunge hao wa chama chake kujielekeza katika kujadili Muswada huo. Hapo ndipo alipoonyesha bayana kukosa busara za kuliongoza Bunge kupata mwafaka wa Muswada huo nyeti. Matokeo yake ni kumwingiza Rais Kikwete kwenye mkenge kwa kumtaka aukubali Muswada huo ili uwe sheria, huku akijua kwamba ulikuwa batili kutokana na kupitishwa kwa hoja ya nguvu.
Sio nia yetu kuorodhesha hapa hoja zote za wabunge wa upinzani ambazo Naibu Spika Ndugai alikataa kuzisikiliza na kusababisha mtafaruku mkubwa Bungeni, hatimaye wabunge wa upinzani wakaususia mjadala wa Muswada huo na kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge. Hata hivyo, moja ya hoja hizo ni umuhimu wa kutoa muda zaidi kwa wananchi wa Zanzibar kutoa maoni yao kuhusu Muswada huo kabla haujapitishwa na Bunge.
Kwa jumla, wananchi wengi wamepaza sauti kupinga mchakato uliotumiwa na wabunge wa CCM kuupitisha Muswada huo. Gazeti hili leo limechapisha habari inayotoa kilio cha wananchi mbalimbali wanaomtaka Rais Kikwete asisaini Muswada huo kutokana na upungufu mkubwa uliomo. Hata hivyo, sisi tunadhani Rais Kikwete atumie busara kama alivyofanya katika suala kama hili mwaka jana. Anaweza kuupitisha kuwa sheria, lakini akairudisha sheria hiyo Bungeni ili ifanyiwe marekebisho makubwa.
Tungependa kulitahadharisha Bunge kwamba kazi ya kutunga Katiba ya nchi sio lelemama. Ni mchakato usiohitaji vitendo vya kupimana nguvu au kutunishiana misuli. Ni kazi inayohitaji maridhiano na ushirikiano miongoni mwa wadau. Inahitaji kuvumiliana, kushauriana na kuelekezana katika hali ya utulivu. Ndio maana kuigeuza kazi hiyo kuwa suala la chama fulani cha siasa ni kukaribisha ‘majanga’ kwa nchi yetu. Kama ambavyo Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekuwa ikisisitiza, wingi wa watoa hoja sio muhimu. Jambo muhimu ni nguvu ya hoja
.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company