kwa MUJIBU WA GAZETI LA RAIA MWEMA.
www.hakileo.blogspot.com MBUNGE wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Leticia Mageni Nyerere, anakabiliwa na jaribio la kutapeliwa Sh milioni 315 na Fauzia Jamal Mohamed, mkazi wa Dar es Salaam.
Tayari jaribio hilo la utapeli limeripotiwa Kituo cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam na Fauzia alikamatwa na kufikishwa kituoni hapo kwa mara ya kwanza kwa ajili ya kutoa maelezo ya awali kuhusu tuhuma hizo, Agosti 23, mwaka huu.
Mbunge Leticia anaelezwa kutoa fedha hizo kwa Fauzia Desemba mwaka jana, kupitia kwa mshirika wake wa kibiashara, Lilian Onael Kileo, kwa lengo la kununua moja ya nyumba za serikali zilizoko eneo la Oysterbay, Dar es Salaam.
Lilian amezungumza na gazeti hili na kukiri kupewa fedha hizo na mbunge huyo kwa ajili hiyo. Kwa mujibu wa Lilian, yeye na Fauzia walikuwa na urafiki wa muda mfupi uliotokana na uhusiano wa kibiashara, wote wakijishughulisha na biashara ya udalali ya kuuza na kununua mashamba, viwanja na nyumba, kama ma-Real Estate.
Anasema kutokana na urafiki huo kati yake na Fauzia, Desemba mwaka jana, Fauzia alimdokeza kuhusu kuwepo kwa nyumba ya Serikali iliyokuwa ikiuzwa kupitia kwa Katibu Mkuu wa Hazina katika maeneo ya Oysterbay, kwa thamani ya Sh milioni 400.
Lilian, anasema kwa kuwa hakuwa na kiasi hicho cha fedha, aliamua kuwasiliana na mshirika wake huyo wa kibiashara, mbunge Leticia, na kumjulisha kuhusu ‘dili’ hiyo.
Mbunge Leticia baada ya kupata ‘taarifa njema hizo’ inaelezwa kuwa alikubali kutoa malipo ya awali ya Sh milioni 315.0 kwa ahadi kwamba kiasi kilichobaki cha Sh milioni 85.0 kingeweza kupatikana ndani ya wiki mbili au tatu.
Katika hali inayotia shaka, inaelezwa kwamba
‘dalali huyo wa nyumba ya serikali,’ Fauzia, alimtaka Lilian kupeleka kwake kiasi chote hicho cha fedha kikiwa taslimu, kwa maana ya bila kukipitisha benki, na lakini pia pasipo kuwekeana maandishi mahali popote wakati wa kukabidhiana fedha hizo.
Mbunge Leticia alipoulizwa kuhusu habari hizi, kwanza alionyesha kushituka na kukataa kuingia kwa undani kulielezea suala lenyewe hili, kabla ya kukiri kuwepo kwa jaribio hilo la kupoteza kiasi hicho cha fedha, lakini akisema fedha hizo hazikumfikia mtuhumiwa huyo kutoka mikononi mwake moja kwa moja, bali zilipitia kwa mtu mwingine ambaye aliomba awasiliane naye kwanza kabla ya kusema chochote.
“Hizo fedha zilipitia kwa mtu mwingine, na huyo ndiye aliyetoa ripoti juu ya tukio hilo polisi na kufanikisha kukamatwa kwake. Kwa sasa siwezi kusema chochote, ngoja niwasiliane naye kwanza (Lilian) tushauriane naye, halafu nitakupigia. Leticia hakupiga tena.
Muda mfupi tu baada ya mwandishi wetu kuzungumza na Mbunge Leticia kupitia simu yake ya mkononi, mwandishi wetu alipigiwa simu na Lilian na kusema: “Mheshimiwa amenipigia simu, anasema asingependa kabisa yeye aonekane popote katika suala hili. Unajua huyu ni mwanasiasa na fedha hizi ni nyingi hataki usumbufu.”
Baada ya mwandishi wetu kumwambia kwamba watu hao maarufu ndiyo habari yenyewe kama kweli fedha hizo alitoa yeye, Lilian alijibu: “Sawa, lakini wapo watu wengi maarufu wametapeliwa na mama huyu, naweza kukutafutia watu hao na namba zao za simu kama watakubali kuandikwa, basi uwataje wao.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, amekiri kuwepo kwa shauri hilo katika kituo chake hicho, lakini akasema polisi walikuwa bado wanalifanyia uchunguzi suala hili ili kupata ukweli wake, na kushauri kwamba kama suala hili litaandikwa linaweza kuharibu uchunguzi wao huo.
“Huyu mtu (Fauzia Jamal Mohamed) bado tunamchunguza kama kweli ni tapeli au la kama unavyosema. Kuchapisha habari hizi mapema kabla ya kukamilisha uchunguzi kunaweza kuharibu uchunguzi wetu,” alisema RPC Wambura.
Alipoambiwa kazi za waandishi wa habari za uchunguzi mara nyingi ndizo zimekuwa zikilisaidia polisi na vyombo vingine vya dola katika kufanya uchunguzi wao, na kwa hiyo, kuandikwa kwa habari hizi mapema kunaweza kukaisaidia zaidi polisi, RPC Wambura alisema:
“Najua ninyi waandishi mnaweza kuwa mnajua vitu vingi zaidi kumhusu mtu huyu kuliko sisi. Na ni kweli ninyi ni wadau wetu muhimu katika masuala haya ya uchunguzi, lakini nashauri kama unazo taarifa zozote zinazomhusu mtu huyu kamuone RCO umpatie taarifa hizo ulizonazo.”
Hata hivyo, vyanzo kadhaa vya habari kutoka katika kituo hicho cha Oysterbay, zinasema hadi sasa Fauzia Mohamed hajafikishwa mahakamani kusomewa tuhuma zinazomkabili tangu akamatwe Agosti 23, mwaka huu, kwa madai kwamba jalada lililofunguliwa kituoni hapo dhidi yake ni jalada la uchunguzi kwanza ili kubaini kama kweli malalamiko dhidi yake yana uhalali wowote.
Fauzia Mohamed mwenyewe amezungumza na gazeti hili na kukiri kukamatwa na kufunguliwa kesi katika kituo hicho cha Osterbay. Hata hivyo, alisema waliomfanyia mambo hayo (kumfikisha kituo cha polisi), wana nia ya kumdhalilisha tu, huku pia akiwatupia lawama baadhi ya wanasiasa nchini kwa kuwataja majina yao kwamba wako nyuma ya njama hizo za kumdhalilisha.
“Raia Mwema ni gazeti langu, napenda kulisoma sana linaandika vitu vizuri. Kama ni fedha zao nimeshawalipa. Hata ukitaka TT (hati za kuhamisha fedha benki) nitakuonyesha, ninazo. Hawa ni watu waliopanga kunidhalilisha tu…mimi mtu mzima, siwezi kuwa tapeli mtu…hizi ni njama za wanasiasa huko serikalini wanaotumia madaraka yao vibaya, hawa ni akina (anataja jina la mwanasiasa), wamepanga kunidhalilisha kwa sababu zao tu,” alisema Fauzia Mohamed.
Mama huyo alitimiza ahadi yake kwa kuwasilisha nyaraka zake chumba chetu cha habari zinazothibitisha kupokea kiasi hicho cha fedha cha Sh 315,000,000.00 kutoka kwa Lilian, likini kikielezwa kuwa ni mkopo, pamoja na hati za kibenki (TT) anazodai zilitumika kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti yake kwenda Lilian kwa lengo la kulipa deni.
Nyaraka hizo za kuhamishia fedha, zinaonyesha kwamba Januari 30, mwaka huu, kupitia benki ya CRDB PLC, mwana mama huyo mwenye umri wa miaka 72, akiwa amezaliwa mwaka 1941, alihamisha dola za Kimarekani 50,000, sawa na takriban Sh milioni 80, kwenda kwa Lilian Kileo.
Aidha, nyaraka hizo zinaonyesha kwamba, kupitia benki hiyo hiyo ya CRDB, Agosti Mosi, mwaka huu alihamisha Sh 70,000,000.00 kwenda kwa Lilian, kabla ya kufanya hivyo tena Agosti 6 (Sh 25,000,000.00) na Agosti 12 mwaka huu Sh 60,000,000.00 na hivyo kufanya jumla ya kiasi alicholipa kufikia Sh 235,000,000.00. Alipopigiwa Lilian ili athibitishe malipo hayo, simu yake iliita muda wote bila kupokelewa.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba dola 50,000, sawa na Sh 80,000,000 zinazodaiwa kulipwa Januari 30 mwaka huu, hazikuwa sehemu ya fedha hizo, bali ni fedha alizokuwa akidaiwa na Lilian kutokana na biashara nyingine kabisa tofauti na mauziano ya nyumba hiyo inayodaiwa kuwa ya Serikali.
Hiyo inathibitishwa na ukweli kwamba siku ambayo Fauzia anadai alihamisha kiasi hicho cha fedha ili kulipa deni hilo, ndiyo siku ambayo mkataba wa makubaliano ya kukopeshana kiasi hicho cha Sh milioni 315.0 uliandaliwa na kutiwa sahihi mbele ya mwanasheria wao.
Gazeti hili limefanikiwa kupata mkataba wa kisheria unaoonyesha kwamba Fauzia Jamal Mohamed anadaiwa na Lilian Onael Kileo kiasi cha Sh 315,000,000.
Katika mkataba huo wa Januari 30 mwaka huu, ulioshuhudiwa na kampuni ya uwakili ya Legis Attorneys ya Dar es Salaam, Fauzia aliahidi kulipa deni hilo baada ya miezi sita kuanzi tarehe ya kusainiwa kwa makubaliano hayo. Miezi sita kwa mujibu wa makubaliano hayo, ilimalizika Julai 30, mwaka huu.
Mtandao maarufu wa kijamii nchini, Jamiiforums, umemtaja mama huyo kwamba ameshawaliza wanasiasa wengi maarufu nchini, akiwemo Andrew Chenge. Aidha, mtandao huo unadai kwamba nyumba kadhaa anazozimiliki mama huyo katika maeneo ya Masaki na Oysterbay amezitapeli kutoka mashirika tofauti ya umma nchini, yakiwemo ya NIC, NHC, NSSF, Ushirika na Bandari kwa kutengeneza hati na mikataba feki ya mauzo (Sales Agreements).