Kulingana na taarifa kutoka ofisi ya rais, imeonya mtu yeyote atakayefanya vitendo vyoyote akitumia jina la waasi la Seleka ataadhibiwa. " Kutoka hii leo kundi la waasi la Seleka halipo tena," Alisema rais Djotodia aliyeapishwa kuwa rais mpya wa nchi hiyo mwezi Agosti m,waka huu katika nchi inayokumbwa na ghasia za mara kwa mara.
Waasi wa Seleka wameshutumiwa kufanya wizi na mauaji baada ya rais wa zamani Francois Bozize alipoondolewa madarakani mwezi Machi.
Wakati huohuo Umoja wa Mataifa umeonya, Jamhuiri ya Afrika ya Kati inaweza kuwa nchi iliofeli katika majukumu yake kutokana na kuyumba kwa uthabiti wa nchi hiyo.
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon
Hata hivyo baada ya kumpindua kutoka madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo Francois Bozize, Rais Djotodia ambaye wakati huo alikuwa mshirika wa kundi la waasi wa Seleka alitambulika na jamii ya kimataifa kuwa ataiendesha nchi hiyo katika kipindi cha mpito kwa miezi 18 hadi wakati kutakapofanyika uchaguzi mkuu.
Rais wa sita wa taifa la Jamhuri ya Afrika ya kati ambalo ni koloni la zamani la Ufaransa, kwa sasa ana changamoto kubwa ya kurejesha usalama nchini humo.
Huku hayo yakiarifiwa miezi sita baada ya Bozize kuondolewa madarakani bado kumekuwa na wingu zito la uhalifu.
Rais akabiliwa na changamoto ya kuimarisha Usalama
Ripoti mbali mbali zimetolewa juu ya kuzidi kwa visa vya ubakaji, kusajili watoto kuwa wanajeshi na hata kuingizwa kwa silaha kinyume na sheria nchini humo hali iliomlazimu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon kusema kwamba nchi hiyo inahitaji dunia kuisaidia na kuiangalia kwa makini.
Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa wapiganaji wa Seleka ambao wengi wao hawajalipwa mishahara yao ya miezi kadhaa wanapaswa kulaumiwa kutokana na ghasia zinazoendelea nchini humo.
Rais mpya wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Michel Djotodia
Kwa upande wake shirika la kimataifa linalotetea haki za binaadamu limesema mwezi wa Julai lilipokea visa takriban 400 vya mauaji ambayo yalitekelezwa na kundi la waasi wa Seleka. Lakini licha ya watu kadhaa kutiwa nguvuni waliotekeleza mauaji hayo wamekwepa bila ya kuadhibiwa.
Nchi hiyo isiokuwa na bandari ilio na idadi ya watu milioni 4.6 na yenye utajiri wa madini ambayo bado hayajavumbuliwa inapakana na mataifa yalioyumba kiusalama kama Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Chad na Sudan Kusini.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP
Mhariri: Sekione kitojo
CHANZO DW SWAHILI.