Watu wawili wameuawa katika mashambulizi ya guruneti mjini Kigali Rwanda.
Mwathiriwa wa kwanza alifariki katika shambulizi la kwanza lililotokea Ijumaa katika soko moja mjini humo.
Guruneti lengine lililipuliwa katika eneo hilohilo Jumamosi na kumuua mtu wa pili huku wengine wanane wakijeruhiwa.Shambulizi hili pia liliwajeruhi watu 14 kwa mujibu wa taarifa za polisi.
Polisi wamewakamata watu watatu kuhusiana na mashambulizi hayo.
Hakuna aliyekiri kufanya mashambulizi hayo, ambayo yametokea kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa wabunge siku ya Jumatatu.
"Sidhani kama mashambulizi haya yataathiri uchaguzi kwa njia yoyote,tumedhibiti hali," alinukuliwa akisema msemaji wa polisi.
Mwaka jana watu 22 walipatikana na hatia ya kufanya mashambulizi mabaya ya guruneti nchini humo ikiwemo waliokuwa wanajeshi wa serikali waliosemekana kuwa na uhusiano na kundi la waasi la FDLR.
Baadhi ya viongozi wa kundi hilo wanadaiwa kuhusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.