HABARI ZETU
www.hakileo.blogspot.comWanawake wa Zimbabwe wakisubiri kupiga kura Julai 31, 2013
Makundi ya wanawake nchini Zimbabwe yamekasirishwa na uamuzi wa rais Robert Mugabe wa kuteuwa wanawake watatu pekee katika baraza lake la mawaziri 26.
Akitetea uamuzi wake, bw.Mugabe alisema ni sharti wanawake wafanye vyema zaidi katika chaguzi ili waweze kupewa viti vya uwaziri.
Wanawake nchini humo wanasema usawa wa kijinsia nchini upo mbali sana kufikiwa. Ni asili mia 12 tu ya wanawake kwenye baraza la mawaziri ikilinganishwa na idadi ya wanawake nchini humo ambayo ni asili mia 52 kwa mujibu wa hesabu ya idadi ya watu iliyofanywa mwaka jana.
Baada ya kuwaapisha mawaziri Jumanne rais Robert Mugabe aliwaambia waandishi habari kuwa hakuna la kustaajabia kwamba wanawake ni wachache kwenye baraza hilo. Alisema elimu ni kwa wote sasa.Na kwamba si muhimu tena kutoa kipaumbele kwa maswala ya wanawake kwa sababu hali ni sawa kwa wote kushindana. Na inafaa wanawake wapambane na wenzao wa kiume bila kutegemea kupendelewa kwa namna yoyote.
Katiba mpya ya Zimbabwe iliyoidhinishwa mapema mwaka huu inaelezea vipengele vya kisheria vinavyolinda wanawake ikiwemo kuwa na haki sawa katika ajira na uwakilishi sawa katika ofisi zote za umma, ambapo inategemewa kwamba usawa huo ni pamoja na uwakilishi kwenye baraza la mawaziri.
Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC ambayo Zimbabwe ni mwanachama ina sheria inayosema wanawake wawe na uwakilishi wa kisiasa kwa asili mia 50 ifikapo mwaka wa 2015. Wanawake wengi nchini humo wasomi, watetezi wa haki za kirai na wafanyabiashara wanasema wanatumaini serikali itatii katiba na kuwapa nafasi sawa na wenzao wa kiume