Jumba la Biashara la Westgate la Nchini Kenya lililoshambuliwa na Wanamgambo wa Al Shabab
REUTERS/Thomas Mukoya
Na
Nurdin Selemani RamadhaniShirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya limesema idadi ya watu waliokosekana tangu kutokea kwa shambulizi la kigaidi kwenye Jumba la Biashara la Westgate Jijini Nairobi imesalia kuwa watu thelathini na tisa tofauti na hapo awali ambapo watu sitini na mmoja walikuwa hawajulikani walipo. Shirika hilo limesema idafi hiyo imepungua baada ya watu kumi na nne kupatikana wakiwa hai huku miili mingine saba ya watu waliopoteza maisha kuendelea kuwepo kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti kitu ambacho kimechangia kushuka kwa idadi ya watu waliokuwa hawajulikani walipo.
www.hakileo.blogspot.comWakuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya wamesema hadi kufika sasa hawana taarifa za watu hao thelathini na tisa licha a kwamba usafi wa kuondoa vifusi kwenye mabaki ya jengo la Westgate kufanyika kama ambavyo Jeshi nchini humo limethibitisha.
Taarifa hii ya Shirika la Msalaba Mwekundu inatolewa huku takwimu za Serikali zikiendelea kusalia watu waliopoteza maisha kwenye shambulizi hilo wakiwa ni sabini na saba wakiwemo wanasjeshi sita ambao nao waliuawa kwenye mashambulizi na wanamgambo wa Al Shabab.
Haya yanakuja huku Mkuu wa Usalama wa Taifa nchini Kenya akiendelea kuhojiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi akituhumiwa kushindwa kufanyia kazi taarifa za kijasusi zilizokuwepo juu ya kupangwa kwa Shambulizi la kigaidi katika Jumba la Biashara la Westgate.
Mkuu wa Usalama wa Taifa ameendelea kukabiliwa na hali ngumu ni kwa nini alishindwa kuwa na taarifa za kutosha ambazo zingesaidia kuzuia kutokea kwa shambulizi hilo la kigaidi linalotajwa kupangwa na kutekelezwa na Wanamgambo wa Kundi la Al Shabab wenye uhusiano na Mtandao wa Al Qaeda.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi nchini Kenya imefikia uamuzi huo wa kumhoji Mkuu wa Usalama wa Taifa kutokana na uwepo wa taarifa zilizovuja na kueleza Kitengo cah Usalama wa Taifa kilikuwa na taarifa za kutokea kwa shambulizi hilo tangu mwaka 2011 lakini walishindwa kuchukua hatua madhubuti kulidhibiti.
Taarifa zimeendelea kuzagaa na kuanisha Kundi la Al Shabab lilishatoa tishio la kushambulia Jumba la Biashara la Westgate pamoja na Kanisa la Mtakatifu Bsilica lililopo Jijini Nairobi lakini hakuna hatua za haraka zilizochukuliwa kuhakikisha kitisho hicho kinafanyiwa kazi kwa wakati.
Vyombo vya Habari zimekuwa vikivujisha taarifa zinazoeleza kuwa Usalama wa Taifa wa Kenya ulivyopata taarifa hizo za onyo la kufanyika kwa mashambulizi walichukua hatua za kuifahamisha Marekani na Israel ili kuhakikisha wanawasaidia kuchukua hatua kukabiliana nalo.
Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya Joseph Ole Lenku kwa upande wake amekanusha madai ya kwamba Serikali ilikuwa na taarifa zaidi ya mwaka mmoja kabla ya kutokwa kwa shambulizi hilo na kusema hizo ni taarifa zisizona ukweli wowote na kama wangepata onyo hilo wangelifanyia kazi.
Lenku amewaambia wanahabari Serikali imekuwa makani katika kuhakikisha wanaimarisha hali ya usalama katika nchi yote ya Kenya kwa hiyo wanapopata taarifa kama hizo hawawezi kukaa kimya kwani wanafahamu madhara yanayoweza kutokea ni makubwa.
Katika hatua nyingine Waziri Lenku amekanusha taarifa zilizokuwa zimezagaa ya kwamba zaidi ya watu sabini wamefukiwa kwenye vifusi vilivyochangiwa na kulipuliwa kwa jengo hilo na amesisitiza hakuna mtu mwengine aliyeuawa zaidi ya wale sitini na saba waliotolea maelezo.
Kumekuwa na taarifa na hali ya wasiwasi nchini Kenya kutokana na watu kadhaa kuendelea kusaka ndugu zao ambao hawajulikani walipo huku taarifa ya mwisho ya Shirika la Msalaba Mwekundu likisisitiza watu wanaokadiriwa kufikia sitini hawajulikani walipo.
Serikali nchini Kenya imesisitiza kwenye shambulizi hilo la kigaidi la huko Westgate walifanikiwa kuwaua Wanamgambo watano waliokuwa wamewashikilia mateka na kuwaua wananchi waliokuwa kwenye Jumba hilo.