BADO HALI NI TETTE MISRI SASA MAREKANI YA SITISHA MSADA WAKE WAKIJESHI



Na Victor Melkizedeck Abuso

Marekani inasitisha ufadhili wa Dola Bilioni 1 nukta 3 ambao umekuwa ukitoa kwa jeshi la Misri kuliimarisha kifedha na kulinunulia silaha za kisasa pamoja na kufanya mazoezi ya pamoja.
Wizara ya Mambo ya nje imetangaza uamuzi huo umechukuliwa kutokana na kudorora kwa hali ya kisiasa nchini Misri na msaada huo utarejelewa tu baada ya utulivu wa kisiasa kushuhudiwa tena nchini humo.

Marekani ilikuwa imeonya kuichukulia Misri hatua hii baada ya jeshi kuanza kuwasaka wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Mosri na kusababisha vifo vya mamia ya wafuasi wa chama cha Muslim Brotherhood mwezi wa Agosti.

Msemaji wa Wizara hiyo Jen Psaki amesema serikali ya mpito nchini Misri imejulishwa kuhusu hatua hiyo na ushirikiano huo utarudi kama kawaida baada ya kufanyika kwa Uchaguzi utakaokuwa huru na haki nchini humo.

Mbali na msaada huo wa mara ka mara wa kijeshi, Marekani ilikuwa imepanga kutoa msaada wa Dola Milioni 260 na kutoa mkopo wa Dola 300 kwa serikali ya Misri msaada ambao pia umesitishwa.

Mwezi uliopita, rais Barrack Obama akizungumza katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa alikashifu namna Mosri alivyoondolewa madarakani na jeshi na kusisitiza uwepo wa suluhu la kisiasa nchini humo kwa kuwashirikisha washikadau wote.

Wakati hayo yakijiri, Mahakama nchini Misri siku ya Jumatano ilitenga tarehe 4 mwezi wa Novemba kuanza kusikilizwa kwa kesi ya uchochezi na mauaji inayomkabili rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Morsi.

Morsi atafika kizimbani akiandamana na washtakiwa wengine 14 wanaotuhumiwa kuchochea mauaji hayo wakati wa maandamani mwezi Desemba mwaka uliopita, miezi saba kabla ya uongozi wake haujapinduliwa na jeshi.

Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa kushtakiwa kwa Morsi huenda kukasababisha maandamano zaidi nchini humo kipindi hiki hali ya wasiwasi ikiendelea kutanda baada ya watu 57 kuuliwa Jumapili iliyopita wakati wa makabiliano na polisi jijini Cairo.

Upande wa Mashtaka unamtuhumu Morsi kuchochea maaandamano na mauji ya raia wasiokuwa na hatia mwaka uliopita kwa kutumia mamlaka yake vibaya kama kiongozi wa taifa hilo.

Wapinzani wa Morsi walianza kupiga kambi nje ya Ikulu jijini Cairo kumtuhumu kushindwa kutekeleza mabadiliko muhimu aliyowaahidi alipoingia madarakani baada ya mapinduzi dhidi ya rais wa zamani Hosni Mubarak.www.hakileo.blogspot.com
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company