DIWANI WA CCM APIGWA.

na Samwel Mwanga, Shinyanga
DIWANI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Chambo, wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga, Damas Njige, amepigwa na maofisa wa Maliasili wilayani humo, kisha kuwekwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Kahama kwa saa kadhaa, kwa madai ya kuwazuia kufanya kazi.

Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita wakati maofisa hao walipokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kuwatafuta watu wanaoharibu mazao ya misitu katika eneo hilo kinyume cha utaratibu.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kudhaminiwa jana, Njige alisema kuwa alifikwa na kadhia hiyo alipojaribu kuwazuia maofisa hao kutowanyanyasa wananchi na kuwadhulumu mali zao.

Kwa mujibu wa Njige, msimamo wake huo wa kutaka taratibu za uendeshaji misako ya mazao ya misitu zifuatwe ulisababisha akamatwe na kuanza kumshambulia kwa kipigo na kujeruhiwa.

“Mimi nilikuwa msibani, lakini nilipata taarifa kutoka kwa baadhi ya wananchi kwamba kuna maofisa Maliasili wanaendesha msako wa kukamata mbao, mkaa na samani za ndani, zikiwamo meza, vitanda, flemu za milango na madirisha, kitu ambacho si cha kawaida.

“Nilipofika katika eneo hilo nikajaribu kuwasihi maofisa hao wasitishe msako wao, lakini sikusikilizwa, badala yake walinikamata na kuanza kunishambulia kwa kipigo na wananchi walipochachamaa risasi zilifyatuliwa hewani ili kuwatawanya,” alieleza.

Alisema baadaye maofisa hao walimbeba kwenye gari la halmashauri ya wilaya walilokuwa nalo na kumpeleka wilayani, ambapo walimfikisha katika Kituo Kikuu cha Polisi na kuwekwa mahabusu hadi alipodhaminiwa saa 3:30 usiku.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangalla, alisema hakuwa na taarifa za tukio hilo.www.hakileo.blogspot.com






Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company