Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Bi. Nkosazana Dlamini-Zuma amesema kura ya maoni inayoendelea katika eneo la Abyei si halali na amewataka wanaosimamia zoezi hilo kusitisha mara moja.
Kamati inayosimamia kura hiyo ya maoni imesema asilimia kubwa ya wakaazi tayari wamepiga kura. Msemaji wa kamati hiyo, Luke Biong amesema wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya serikali ya Sudan kuakhirisha zoezi hilo tangu mwaka 2011.
Bi Dlamini-Zuma amesema Umoja wa Afrika unafahamu fika matatizo ya watu wa Abyei hususan hali yao ya kuendelea kubakia gizani kuhusu hatima ya utambulisho wao lakini akasisitiza kuwa, kura ya maoni inaweza kuzirudisha vitani Sudan na Sudan Kusini. Serikali ya Sudan pia imesema haitambui zoezi hilo ambalo linatarajiwa kukamilishwa hapo kesho Jumanne.