Waziri mkuu wa Tanzania amaliza ziara yake nchini China

Waziri Mkuu wa Tanzania Bw Mizengo Pinda amemaliza ziara yake ya siku 9 nchini China. Katika ziara hiyo, waziri Pinda aliongozana na ujumbe mkubwa wa mawaziri, wafanyabiashara na maofisa wengi wa ngazi ya kati wa serikali na wabunge. Ziara ya Waziri Mkuu Pinda ni moja kati ya ziara zinazofanywa na viongozi wakubwa kati ya nchi hizi mbili, ikifuatia ziara iliyofanywa na Rais Xi Jinping nchini Tanzania mwezi Machi mwaka huu. Mara alipowasili mjini Beijing, Waziri Mkuu Pinda alikutana na mwenzake wa China Li Keqiang, na kusaini kumbukumbu ya maelewano na nyaraka za ushirikiano katika maeneo ya diplomasia, uchumi, teknolojia, utalii na kilimo. Baadaye alitembelea miji ya Guangzhou, Shenzhen na Chengdu, na kukutana na wakuu wa benki ya maendeleo ya China, makampuni ya serikali na makampuni binafsi.

Ziara ya Waziri Mkuu Pinda nchini China imefanyika wakati China na Tanzania zinajiandaa kuadhimisha miaka 50 tangu zianzishe uhusiano wa kibalozi. Kutokana na ratiba yake, mambo aliyozungumza wakati wa ziara yake, maofisa aliokutana nao na nyaraka za ushirikiano zilizosainiwa kati ya pande hizo mbili, kimsingi tunaweza kuona kuwa ziara hiyo inaonesha kulenga zaidi mambo ya uchumi. Mbali na kuwa ziara yake pia imethibitisha kile ambacho wengi tunakifahamu, ya kuwa China na Tanzania ni marafiki wakubwa wa tangu zamani, ziara hii pia imeonesha mambo yanayotakiwa kufanyiwa kazi ili kuhakikisha kuwa pande hizo mbili zinanufaika zaidi na ushirikiano mzuri uliopo.

Jambo moja kubwa lililoonekana ni kuwa, pamoja na kuwepo kwa uhusiano mzuri na wa muda mrefu wa kisiasa, bado kuna baadhi ya maeneo muhimu ya ushirikiano ambayo hayajafanyiwa kazi vya kutosha ili kuwezesha uwekezaji kutoka China uingie na kuchangia maendeleo ya Tanzania. Wakati wa mazungumzo yao, Waziri mkuu wa China Bw Li Keqiang aliitaka serikali ya Tanzania iweke urahisi kwa wawekezaji wa China wanaotaka kuwekeza nchini Tanzania. Hii inaonesha kuwa, kuna utayari kwa upande wawekezaji wa China kuwekeza Tanzania, lakini kwa pande wa Tanzania bado kuna ugumu fulani kwa wawekezaji wa China.

Mfano mzuri unaothibitisha hali hii ulitolewa na Mh Pinda alipokuwa mjini Shenzhen alipokutana na wakuu wa kampuni ya utalii ya CTS, (China Travel services). Waziri Mkuu Pinda alishangaa ni kwanini Kenya na Afrika Kusini zinapata watalii wengi zaidi kutoka China kuliko Tanzania, wakati Tanzania ambayo imekuwa na uhusiano mzuri na China kwa muda mrefu zaidi ya nchi hizo inapata watalii wachache. Jambo hili linaonesha dosari zilizopo nchini Tanzania, ambazo zinazofanya kuwe na ugumu kwa China kutoa mchango mkubwa zaidi kwa maendeleo ya nchi hiyo, na inayofanya matunda ya ushirikiano huo yasiwafikie haraka watu wa kawaida wa Tanzania.

Tukiangalia mfano huu wa sekta ya utalii, tunaweza kuona kuwa China imeziweka nchi nyingi za Afrika kwenye orodha ya nchi zinazoweza kupokea watalii kutoka China, na hii inaonesha utayari wa China katika kuingia kwenye ushirikiano wa kunufaisha na nchi za Afrika. Lakini nchi zenyewe zinazohitaji kupokea watalii, zina mazingira kadhaa yanayotakiwa kuboreshwa ili ziweze kupokea watalii kutoka China. Kwanza, bado kuna tatizo la kiuslama zinazowafanya wachina waogope kwenda kwenye nchi hizo, pili bado hakuna miundo mbinu ya kutosha yenye kiwango na gharama zinazofaa kwa watalii, na tatu, kusafiri kwenda katika baadhi ya nchi za Afrika ni vigumu, kuliko kusafiri kwenda Marekani au Amerika ya Kusini. Wakati fulani unatakiwa kuunganisha ndege tatu kwenda katika nchi ya Afrika kutoka China, wakati kwenda Marekani ambako ni mbali zaidi kuna ndege ya moja kwa moja, au Ulaya ambako umbali wake unafanana na ule wa Afrika hauhitaji kubadili ndege, kwani kuna ndge ya moja kwa moja. Kwa hiyo, kilichoonekana ni kuwa, kama Tanzania ikiboresha zaidi mazingira yake, urafiki uliopo kati yake na China, unaweza kuwa mali halisi inayoweza kuwa na manufaa makubwa kwa watu wake. Hata hivyo, mkuu wa Kampuni ya CTS amemwahidi waziri Mkuu wa Tanzania kuwa kampuni yake itajitahidi kuhimiza watalii elfu 10 kwenda Tanzania kila mwaka.

Jambo lingine lililonekana katika ziara ya waziri mkuu wa Tanzania ni kuwa, kwa mara ya kwanza kwenye historia ya uhusiano kati ya China na Tanzania, tumeanza kusikika zaidi sauti ya "ushirikiano wa kunufaishana", na sio ushirikiano wenye sura ya zamani wa "mtoaji msaada na mpokeaji msaada". Tukifuatilia yaliyomo kwenye kumbukumbu ya maelewano iliyosainiwa kati ya upande wa China na Tanzania, mambo yaliyomo ni pamoja na yanayohusu kilimo, sekta ya utalii, nishati na sayansi na teknolojia. Lakini waziri Mkuu wa Tanzania amesema wazi kuwa, Tanzania inapenda ipate fursa ya kuuza bidhaa zake hapa China, na ameiomba China ihimize wawekezaji wenye teknolojia kwenda Tanzania kuwekeza katika maeneo yatakayosaidia kuihimiza Tanzania kuuza mazao yake na bidhaa zake za kilimo nje ya nchi. Bidhaa alizoziwekea msisitizo ni tumbaku, korosho, pamba na mazao ya majini. Hizi ni bidhaa ambazo zinapatikana kwa wingi nchini Tanzania, na watu wengi wa kawaida wanalima bidhaa hizo, lakini tatizo kubwa linakuwa soko la bidhaa hizo. Bidhaa hizi zote zina soko kubwa hapa China, na kama Tanzania ikiweza kuuza bidhaa hizo nchini China basi watanzania wengi wanaojihusisha na shughuli hizo wataweza kunufaika.

Eneo lingine ambalo pia limeonesha mwelekeo huo, ni eneo la nishati. Pamoja na kuwa tayari China na Tanzania zinatekeleza mkataba wa uchumbaji na kuzalisha umeme kwa makaa ya mawe na gesi, moja kati ya mambo aliyofuatilia Mh Pinda katika ziara yake ni mradi wa kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo ambao unatarajiwa kujengwa katikati mwa Tanzania. Tatizo la nishati limekuwa ni moja kati ya matatizo makubwa yanayofanya uzalishaji nchini Tanzania uwe duni, na hata kukwamisha maendeleo ya viwanda vidogo vya usindikaji. Ni kwa sababu hiyo, katika miaka ya hivi karibuni, China na Tanzania zimejikita kwenye ushirikiano wa sekta ya nishati. Katika ziara hii, Mh Pinda alikutakana na Bw Xu Youliang, Makamu Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa ya Kundi la Daliang (China Daliang International Group) itakayojenga mradi mkubwa wa kuzalisha umeme kwa nishati ya gesi. Bw Xu amemwambia waziri mkuu kuwa, baada ya kampuni yake kukamilisha ujenzi wa mradi huo mwaka 2015, umeme wa megawati 150 utazalishwa. Lakini cha muhimu zaidi ni kuwa, kampuni hiyo pia imeahidi kuwa wakati inajenga mradi huo, itajenga barabara yenye urefu wa kilometa 17 kuelekea kwenye eneo la mradi, barabara ambayo pia itakuwa na manufaa ya kiuchumi kwa watu wa eneo hilo, na pia kutoa nafasi za ajira kwa wenyeji zaidi ya 1000 kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo na barabara. Utakapokamilika, mradi huo utakuwa ni mradi wa kipekee wa aina hiyo katika nchi za Afrika Mashariki.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company