Magazeti mengi si Kigezo Sahihi cha Uhuru wa Habari (2)



Hivyo, ni vizuiri kuelewa kuwa chombo cha habari hakiwezi kuwa huru kwa sababu tu kinamilikiwa na mtu au kampuni binafsi. Mara nyingi chombo kama hicho huwa kinatekeleza matakwa na kinawakilisha masilahi ya kibiashara ya mmiliki wake badala ya kuwakilisha mahitaji ya wasomaji au wasikilizaji au watazamaji wake.
Kwani mara ngapi tunawaona waandishi au hata wahariri wakitumiwa kama chombo, kwa masilahi ya mmiliki ambaye ndiye mwamuzi wa mwisho, hata kama haonekani asilani katika chumba cha habari.
Ndiyo maana mwanasheria na msomi maarufu, Profesa Issa Shivji amewasihi wanahabari wapiganie uhuru wa kweli katika kazi zao. Amesema tusikubali weledi wetu kuingiliwa na watawala, wamiliki au wafadhili.


Anasema ni kawaida kwa watawala kukwepa suala la uwazi kwa sababu hupenda mambo yao yawe ya siri. Ndiyo maana mara nyingi hujaribu kuminya na kudhibiti usambazaji wa habari zinazowahusu.


Hujaribu kuwavutia wanahabari upande wao kwa kuwapa vishawishi na motisha, yaani “ulaji.” Ndipo utasikia ghafla mwanahabari “mtiifu” hupandishwa cheo na kuwa mkurugenzi au mkuu wa shirika.


Na pale isipowezekana, utasikia gazeti limepigwa marufuku au mwanahabari ameshushwa cheo au amehamishiwa mahali ambako itamuwia vigumu kuendelea na kazi ya kufichua maovu ya wakuu. Hizi ni mbinu zinazoweza kutumiwa siyo tu katika vyombo vya habari vya serikali bali hata vile vinavyomilikiwa na wafanyabishara ambao wana masilahi yao ya kibiashara.


Mhariri hataruhusiwa kufichua mradi mbovu wa madini iwapo kampuni ya madini inatoa matangazo makubwa au inashirikiana na mmiliki wa magazeti.


Hizi ni ajenda za siri zilizo katika vyombo vya habari.
Ndiyo maana Profesa Shivji anaangalia suala zima la uhuru wa uhariri ambao ni msingi wa uhuru wa habari. Chini ya suala hili la uhuru wa uhariri ni muhimu kwa mhariri au mwandishi kutoingiliwa na mwajiri katika weledi wake. Ni muhimu pia mhariri asiyumbishwe na mfadhili au mwekezaji. Lengo lake liwe kutumikia masilahi ya wasomaji au wasikilizaji, badala ya maslahi ya wawekezaji. Kwani mwekezaji hawezi kuwa mweledi. Lengo lake ni kutengeneza faida.
Ndipo Baraza la Habari Tanzania (MCT) likaamua kutoa Azimio la Dar es Salaam kuhusu uwajibikaji na uhuru wa uhariri (DEFIR). Wanahabari, wamiliki wa vyombo vya habari na wananchi kwa ujumla waliombwa wajitokeze na kuuridhia waraka huu kwa kuweka saini zao.

DEFIR haizungumzii tu uhuru wa habari bali pia wajibu na jukumu la wanahabari katika kuulinda uhuru huu kwa niaba ya wananchi.

Ni kwa sababu uhuru huu si mali ya mwana habari kuandika atakalo, bali ni uhuru wa mwananchi kutoa na kupata habari. Mwana habari ana wajibu wa kuhakikisha kuwa mwananchi mmoja mmoja na kwa ujumla wao wana haki hiyo ya kimsingi.
Bila shaka, DEFIR inaunga mkono umuhimu wa kuwa na vyombo binafsi vya habari. Lakini papo hapo inatahadharisha kuwa vyombo hivyo vinaweza vikahodhiwa na watu wachache kwa faida yao. Hapo vyombo hivyo vitakuwa si tofauti na vile vinavyomilikiwa na dola kwa faida yake.
Kwa maneno mengi, vyombo vya habari kuhodhiwa si jambo zuri, bila ya kujali ni nani anayehodhi vyombo hivyo. Njia bora ni kwa vyombo hivyo kumilikiwa na kuendeshwa na wanahabari na wadau wenyewe kupitia ushirika wao.
Uhuru wa uhariri unaweza ukahatarishwa sio tu na wamiliki binafsi, bali pia na dola, wanasiasa, viongozi, wafadhili, wawekezaji na wana diplomasia. Tofauti ni kuwa wakati dola inatumia vyombo vyake vya ukandamizaji kama polisi, mahakama na Usalama wa Taifa, wengine hutumia nguvu za fedha ili kudhibiti uhuru wa tahariri.
Haya yanaonekana zaidi katika nchi zetu zinazotegemea wafadhili au wahisani kwa kila jambo, kuanzia uchimbaji wa vyoo katika shule za msingi hadi kuitisha warsha za wanahabari na semina elekezi kwa vigogo.
Mara nyingi hao wanaofadhili watajaribu kusukuma mbele ajenga zao. Ubalozi unaotoa msaada wa kompyuta kwa chumba cha habari ni nadra kuandikwa au kutangazwa vibaya. Ifikapo hapo chumba cha habari kinakuwa kimepoteza uhuru wake wa uhariri.
Kuna ushawishi mwengine katika vyumba vya habari.
Huu unatokana na utandawazi wa mataifa makuu ambayo yanadhibiti habari zinazoenezwa ulimwenguni. Udhibiti huu unatokana na mataifa babe kwa kupitia kampuni zao za kimataifa ambazo zinahodhi habari duniani.
Ndiyo maana, ukiangalia habari zinazoingia katika vyumba vyetu vya habari utaona kuwa sehemu kubwa inatokana na vyanzo vikubwa viwili au vitatu. Hapa ndipo wanahabari na wahariri wetu wanapaswa kutumia weledi na kuepukana na kasumba kutoka mataifa ya Kaskazini. Tusikubali kuwa watumwa wa mawazo na badala yake tufanye uchambuzi wetu wenyewe.
DEFIR kwa hiyo ni chombo muhimu sana katika tasnia ya uandishi. Inapaswa kuungwa mkono na waandishi na wadau wote ili kuhakikisha kuwa uandishi na uhariri katika nchi yetu hautiwi kabali na wachache kwa masilahi yao.
CHANZO; MWANANCHI MTANDAONI www.hakileo.blogspot.com
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company