Serikali kuwakopa wakulima kwa miezi mitatu ni kichekesho


Lauden Mwambona
Hivi karibuni, wakulima wa mahindi mkoani Rukwa walipasua jipu kwa kuilalamikia Serikali kuhusu kitendo chake cha kuwakopa mahindi yao tangu Julai mwaka huu na hadi sasa haijawalipa.
Wakulima hao walitoa kauli zao kupitia vyombo vya habari, ambapo walilalamika kwa sauti za kukata tamaa kwa Serikali yao na kusisitiza kwamba wamechoka kuvumilia.
Ilielezwa kwamba Serikali kupitia Wakala wa Hifadhi ya Chakula cha Taifa iliwakopa wakulima lukuki wa mkoa huo tangu Juni, huku ikiwaahidi kuwalipa mapema Agosti.
Wakulima wa mkoa huo wanaidai Serikali zaidi ya Sh6 bilioni na mpaka sasa haijataja ni siku gani wakulima hao watalipwa.

Hali kadhalika wakulima wa zao hilo mkoani Ruvuma nao wametoa ya moyoni wakiilalamikia Serikali kwamba iliwakopa mahindi tangu Juni hadi sasa haijawalipa.

Meneja wa Wakala wa Hifadhi ya Chakula cha Taifa mkoani Ruvuma, Morgan Mwaipyana alikiri kwamba wakulima kudai zaidi ya Sh5 bilioni za mahindi waliyoikopesha Serikali.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu alisema Serikali ililazimika kuwakopa wakulima, baada ya mahindi yao kuwa mengi kuliko makisio ya manunuzi.
Alisema kwa miezi miwili waliweza kukusanya zaidi ya tani 55,000 za mahindi ya wakulima wakati malengo yalikuwa chini ya tani hizo.

Sawa, pamoja na mambo mengi ambayo wakulima wanailalamikia Serikali, lakini suala la Serikali kuwakopa wakulima mazao yao kwa muda mrefu halieleweki kabisa.

Je, ni nani ama mfanyakazi gani wa Serikali asiyetambua jasho la mkulima linavyotoka akiwa shambani mpaka anadiriki kuchelewesha fedha za mkulima?
Ni nani asiyejua jinsi wakulima wanavyodamka asubuhi mapema na kujiingiza kwenye udongo kwa siku nzima wakibugia vumbi ama tope, wakilowa mvua ama kupigwa na jua ili kupata mavuno?

Je, wafanyakazi wa Serikali wanaochelewesha fedha za wakulima hao wana nia gani kwa chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015?
Je, ni kweli tuamini kwamba mawakala wa kuiondoa Serikali ya CCM madarakani ni watendaji wa fedha wanaodaiwa kuunda mitandao ya uhujumu mipango ya maendeleo na kusababisha kero kwa wananchi?
Itawezekana wapi Serikali kuwakopa wakulima? Ni vigumu kuamini, lakini kama Serikali itaendelea na utaratibu wa kuwakopa wakulima, basi hiyo ni njia ya kutengeneza hoja ya msingi ya kwa wapinzani kuing’oa madarakani Serikali ya CCM.
Ikumbukwe kuwa wakulima wa mpunga Kilombero, Kyela, Mbarali wanalalamika kukosa soko, wanailalamikia Serikali, lakini pamoja na kwamba inayo majibu mazuri,
imekaa kimya jambo ambalo wakulima hao wanaamini wazi kwamba Serikali haiwajali wakulima.
Kwa miaka mingi kura za ndiyo kwa CCM zinatoka kwa wakulima, kutokana na wakazi wengi wa mijini kudai wameishajua ufisadi mwingi wa baadhi ya watumishi wa Serikali Kuu na halmashauri.
Hata hivyo, mimi naamini Serikali ni makini, hivyo suala la kuwalipa papo kwa papo wakulima wanapouza mazao yao ni jambo la lazima.
Natambua kwamba Serikali ina mpango wa kuanza kununua mazao mengine ya nafaka yakiwamo ya mtama, karanga, mpunga, ulezi na hata uwele kuanzia mwakani, lakini kama mpango utakuwa wa kuwakopa wakulima basi utasababisha fitina kubwa kati ya CCM na wananchi.
Ili kuepuka fitina hiyo, Serikali ya CCM haina budi kuwajali zaidi wakulima kuliko wanavyofikiria. Wakulima wasaidiwe kwa pembejeo na pia kamwe wasikopwe.
Je, ni kweli Waziri anayeshughulikia kilimo hajaliona hilo? Mbona Rais wa Bunge la Uswisi, Maja Graf aliyetembelea nchini hivi karibuni aliliona hilo na kuishauri Serikali kuwekeza zaidi kwa wakulima wadogo?
Graf alitoa ushauri huo alipotembelea wasindikaji wadogo wa mafuta ya alizeti mkoani Dodoma na kusisitiza kwamba uwekezaji wa katika ngazi za chini ni bora zaidi kwa sababu nguvu ya misaada inawafikia walengwa moja kwa moja.
Hata mimi najua wazi kwamba wakulima wakiuza mazao yao na kupata fedha, basi kasi ya maendeleo vijijini inaonekana kwani wananunua mabati na kujenga nyumba bora, huku wengine wakinunua majembe zaidi, ng’ombe na wengine kununua mavazi mapya.
Kwa hali hiyo ushauri wa Graf aliyefika nchini kwa mwaliko wa Ofisi ya Bunge ni jambo lililopashwa kushughulikiwa siku nyingi za nyuma.
Wafanyakazi Serikali hebu washeshimuni wakulima kwa kulipa madai yao haraka.
0767 338 897
CHANZO MWANANCHI MTANDAOBI.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company