Mbowe: Viongozi wa dini mjiepushe na fedha chafu


MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Freeman Mbowe, ametoa rai kwa viongozi wa dini nchini kuwa makini na watu aliodai kutumia nyumba za ibada kusafisha fedha chafu walizozipata kwa njia haramu ikiwemo ufisadi.
Amesema badala ya kuangalia kiwango kikubwa wa fedha wanazotoa, ni vema wakaenda mbali kwa kuangalia na uhalali na usafi wa kile wanachochangiwa.
Mbowe alisema hayo mwanzoni mwa wiki wakati alipoongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Usharika wa Sono, Kijiji cha Masama-Sono, wilayani Hai.
Jumla ya sh milioni 16 zilipatika katika harambee hiyo, huku Mbowe alichangia sh milioni nane kati ya hizo.
Kiongozi huyo wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, alisema kuwa kuna baadhi ya watu wamegeuza nyumba za ibada kuwa pango la walanguzi ambao hutoa michango ya fedha makanisani na misikitini kama njia ya kujisafisha na tuhuma zao za ufisadi.
“Kwanza napenda kuanza kwa kuwapongeza Watanzania wenzangu na waumini wa usharika huu wa Sono, kwa kuifanya kazi ya Mungu, mlipoamua kujenga jengo hili zuri kwa nguvu zenu wenyewe polepole tangu mwaka 1994 na sasa bado mnaendelea, mkiwa mmemaliza sehemu kubwa ya kazi hii muhimu.
“Katika hatua hii ningependa pia kutoa rai yangu kwa viongozi wetu wa dini nchini. Nitajengea hoja zangu kutokana na mahubiri ya Baba Askofu Kweka. Kwa siku za hivi karibuni kumeibuka tabia ya watu kugeuza nyumba za ibada kuwa ni soko au mapango ya walanguzi.
“Wengine wanajulikana wamepata fedha kwa dhuluma, wizi, rushwa na ufisadi mwingi, fedha ambazo zingenunua dawa hospitalini, kuboresha elimu yetu inayoporomoka na huduma nyingine muhimu.
“Na viongozi wa dini zote napenda kuwasihi, msiingie kwenye mtego wa kuangalia ukubwa wa michango inayotolewa na watu kwenye nyumba za ibada, bali muangalie usafi wa hicho kinachotolewa…msikubali mahali pa ibada kutumika kusafisha fedha chafu. Endeleeni kuwaombea wapate utakaso na kukiri dhambi zao,” alisisitiza Mbowe.
Alisema kuwa yeye na wenzake hawapambani na serikali kwa sababu hawana adabu, bali wameamua kuwa sauti ya watu wengi wanyonge wasiokuwa na sauti katika kupata haki na matumaini katika nchi yao.
Kwa upande wake, Askofu Mstaafu wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Erasto Kweka, alimshukuru Mbowe kwa kufika kwenye harambee hiyo huku akimwahidi kuwa wataendelea kumuombea ili kazi anazozifanya zilete matunda kwa Watanzania wote.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company