Wanajeshi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakisherehekea baada ya kuchukua mji wa Rumangambo
Na
Victor Melkizedeck AbusoMjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa MONUSCO katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Martin Kobler ameliambilia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa kundi la waasi la M 23 sio tishio tena kijeshi Mashariki mwa nchi hiyo.
Kobler ameliambia Baraza hilo kuwa waasi wa M 23 wametoroka katika kambi zao za kijeshi na sasa wanajificha karibu na mpaka wa Rwanda baada ya kulemewa na wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakisaidiwa na wale wa Umoja wa Mataifa.
Mapigano kati ya waasi na majeshi ya serikali yalianza wiki iliyopita baada ya mazungumzo ya amani kuvunjika jijini Kampala Uganda na kufikia siku ya Jumatatu jeshi la serikali lilifanikiwa kuchukua miji ya Rutshuru, Kiwanja na Rumangambo yote ambayo hapo awali ilikuwa inathibitiwa na waasi hao kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Kurudishwa nyumba kwa waasi hao kwa mujibu wa mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini DRC ni ishara tosha waasi hao wamedhoofishwa kijeshi na huenda huu ndio ukawa mwisho wao.
Hata hivyo, waasi hao wa M 23 wanasema kuwa wamejiondoa katika ngome zao kwa muda tu ili kuuonesha ulimwengu kuwa wao hawataki vita kwa mujibu wa rais wa kundi hilo Betrand Bissimwa.
Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa Gerard Araud amesema kuwa baada ya waasi hao kudhoofishwa mazungumzo ya amani sasa yataendelea jijini Kampala ili kupata suluhu ya kudumu baada ya kusitishwa wiki iliyopita.
Wakaazi wa miji ya Rumangabo, Kiwanja, Rutshurum Buhumba na Kibumba wamekuwa wakisherehekea ushindi wa jeshi la serikali tangu mwishoni mwa wiki iliyopita.
Umoja wa Mataifa unasema kuwa zaidi ya watu 800,000 wamekimbia makwao baada ya kundi hilo la waasi kuanza Oparesheni zao Mashariki mwa nchi hiyo mwezi Aprili mwaka 2012.
Nchi za Rwanda na Uganda zimekanusha madai ya watalaam wa Umoja wa Mataifa kuwa wanawaunga mkono waasi hao wa M 23