
Waziri wa Kenya anayehusika na Utalii, Biashara na Masuala ya Afrika Mashariki, Bi Phyllis Kandie amesema kuwa, serikali imeanza kupanga mikakati ya kujenga upya jumba la kibiashara la Westgate ambalo lilivamiwa na magaidi majuma kadhaa yaliyopita. Bi. Kandie amesema wafanyabiashara waliopoteza mali zao kwenye tukio la kigaidi kwenye jumba hilo pia watasaidiwa kuhuisha biashara zao.
Waziri huyo amesema kamati maalum itaundwa na itawajumuisha wadau wote wakiwemo wamiliki wa maduka yaliyokuwa Westgate pamoja na serikali ili kufikiria namna ya kufikia lengo lililokusudiwa. Jumba la Westgate liliharibiwa kabisa wakati wa mapambano kati ya maafisa wa usalama wa Kenya na magaidi walioliteka kwa siku nne mfululizo kuanzia Septemba 21. Maghorofa kadhaa ya juu kabisa yaliporomoka kutokana na kile kinachodaiwa ni makombora ya jeshi la Kenya ingawa serikali imedai magaidi ndio walioripua sehemu ya juu ya jumba hilo.www.hakileo.blogspot.com