Wakaazi wa Mashariki mwa DRC wakikimbia makwao
Wataalam wa Umoja wa Mataifa wanazuru Rwanda siku kadhaa baada ya Marekani kuiwekea serikali ya Kigali vikwazo kutokana na waasi wa M 23 Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuwatumia watoto katika jeshi lake, waasi ambao Rwanda inatuhumiwa kuwaunga mkono.
Rais Paul Kagame anakutana na wataalam hao ambao pia walizuru mji wa Goma kuthathmini hali ya usalama Mashariki mwa nchi hiyo, kipindi hiki Kigali ikiendelea kukanusha madai ya kuwaunga mkono waasi wa M 23 au kujihusisha na machafuko nchini DRC.
Wiki iliyopita, serikali ya Marekani ilitangaza kuiwekea vikwazo serikali ya Kigali kwa kusitisha mafunzo na ufadhili wa jeshi lake baada ya ripoti ya umoja wa Mataifa kuonesha kuwa Kigali imeedelea kuwaunga mkono waasi wa M 23 wanaotumia watoto katika jeshi lake.
Tuhuma za utumizi wa watoto katika jeshi la M 23 zimekanushwa vikali na kiongozi wa kundi hilo Betrand Bissimwa ambaye ameiambia RFI Kiswahili kuwa sheria zao haziruhusu watoto kutumiwa katika jeshi lake na madai hayo hayo hayana msingi.
Katika hatua nyingine, Umoja wa Mataifa unasema utulivu Mashariki mwa DRC unaweza kupatikana tu kupitia mazungumzo ya kisiasa wala sio matumizi ya nguvu.
Alexis Lamek, Naibu Balozi wa Ufaransa katika Umoja huo amesema kuwa mazungumzo ndio njia ya pekee kwa sababu waasi wa M 23 tayari walikuwa wamejumuishwa katika jeshi la serikali mwaka 2009 baada ya muafaka wa amani.
UN inasema mazungumzo ya amani yanayoendelea jijini Kampala ni muhimu sana na ni sharti yamepewe nafasi na suluhu lipatikane ili amani irejee Mashariki mwa DRC.
Mazungumzo hayo kati ya waasi wa M 23 na wajumbe wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamekuwa yakiendelea kwa wiki kadhaa na hadi sasa hakuna muafaka wowote uliopatikana.
Mwezi uliopita, Marais wa Kanda ya Maziwa Makuu walikutana jijini Kampala na kuwapa wajumbe kutoka pande zote mbili wiki mbili kupata suluhu ambalo hadi sasa bado halijapatikana.
Hata hivyo, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tayari imetoa orodha ya baadhi ya waasi wa M 23 watakaojumuishwa katika jeshi la serikali au kupewa msamaha ikiwa suluhu litapatiana.
Makabiliano kati ya waasi wa M 23 na jeshi la serikali yamesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na wengine kukimbia makwao. wwwhakileo.blogspotcom
