Zitto azidi kuwakaang'a CCM, Chadema



Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali Zitto Kabwe akisisitiza jambo wakati wajumbe wa kamati hiyo walipofanya kikao na watendaji wa Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Katibu wa kamati hiyo, Michael Kadebe. Picha na Michael Jamson
Na Beatrice Moses na Fidelis Butahe, Mwananchi
Zitto juzi alikaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa Serikali ilitoa kiasi cha Sh67.7 bilioni kama ruzuku kwa vyama tisa vya siasa tangu mwaka 2009, lakini vyama hivyo havijawahi kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa hesabu zake kwa msajili kama sheria inavyoagiza.

Dar es Salaam. Wakati Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe akisisitiza kuwa hesabu za Chadema ni miongoni mwa ambazo hazijakaguliwa, chama hicho kimeishutumu kamati hiyo kwa kuagiza kusitishwa kwa ruzuku kwa vyama vya siasa na kusema hatua hiyo ni ubabe.


Wakati Chadema wakitoa kauli hiyo, jana Zitto alisema vyama vya siasa tisa vikiwamo Chadema, CCM na CUF vinatakiwa kufika mbele ya PAC Oktoba 25 mwaka huu, kwa ajili ya kujieleza na kwamba chama kitakachokaidi, sheria za Bunge zinaeleza wazi, kwamba wahusika wanaweza kufungwa jela siku saba.


Chadema kilisema kuwa PAC kabla ya kuchukua hatua, ilipaswa kuwapa nafasi ya kuwasikiliza viongozi wa vyama husika, kumhoji Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Msajili wa vyama vya Siasa ambao wameshindwa kutimiza wajibu wa kukagua hesabu hizo kwa miaka minne.


Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Anthony Komu alisema jana kuwa, uamuzi wa PAC utaviathiri vyama kwani bajeti zake zimezingatia kuwapo kwa ruzuku.


“Kuna vyama ambavyo vinategemea ruzuku kulipa mishahara ya wafanyakazi wake, Chadema ingawa tuna vyanzo vingine vya mapato, tunaitegemea kukamilisha bajeti yetu kwa fedha za ruzuku ambazo zinatusaidia kwa asilimia 45. Ni tabia mbaya kuchukua uamuzi kwa kibabe na kuhukumu kabla ya kutusikiliza siyo haki hata kidogo,” alisema Komu.


Alitetea chama chake kwamba kimekuwa na utaratibu wa kuwasilisha hesabu zilizokaguliwa ambapo alitoa ushahidi wa barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya April 16, 2012 ikithibitisha kwamba hesabu zao zipo sawa baada ya kuziwasilisha katika ofisi hiyo.


“Chadema tunataka ukaguzi wa hesabu usijikite katika fedha za ruzuku pekee bali katika vyanzo vyote vya mapato ya vyama, tatizo CAG alitueleza kwamba anakabiliwa na upungufu wa rasilimali watu kwa hiyo PAC walipaswa kuliangalia tatizo hilo na kutafuta ufumbuzi,” alisema Komu.


Zitto juzi alikaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa Serikali ilitoa kiasi cha Sh67.7 bilioni kama ruzuku kwa vyama tisa vya siasa tangu mwaka 2009, lakini vyama hivyo havijawahi kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa hesabu zake kwa msajili kama sheria inavyoagiza.


Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini (Chadema), aliamuru Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kusimamisha utoaji wa ruzuku hadi hapo vitakapowasilisha ripoti ya ukaguzi na makatibu wake wakuu kuhojiwa.


Miongoni mwa vyama vilivyotajwa ni APPT-Maendeleo lakini jana Rais Mtendaji wa Chama hicho, Peter Mziray alisema chama chake hakijawahi kupewa kiasi cha Sh217 milioni kama inavyodaiwa na PAC.


Mziray alikiri walianza kupata ruzuku 2009 ila inasema ilikuwa kidogo kiasi cha Sh 50,000 kwa mwezi na baadae kupanda Sh 275,000 kwa mwezi.


Alisema kiasi walichopata kuanzia mwaka 2009 ni kiasi cha Sh12 milioni tu. “APPT-Maendeleo haina uwakilishi bungeni kwa hiyo haiwezi kupata kiasi hicho kikubwa cha fedha,” alisema Mziray.
Zitto akaza kamba
Jana Zitto alivitaka Chadema, CUF na CCM kuacha kupiga kelele katika vyombo vya habari na badala yake viwasilishe taarifa za ukaguzi wa matumizi yake katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.


“Vyama hivi visilete ujanja ujanja, hizi ni fedha za umma lazima zikaguliwe. Tatizo la CCM, CUF na Chadema wanahusisha suala la kuwasilisha taarifa za ukaguzi na nafasi yangu ya Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, sifanyi kazi kwa niaba ya Chadema mimi nafuata sheria za Bunge na katika hili sitacheka na mtu,” alisema Zitto jana wakati akizungumza na wanahabari katika ofisi ndogo za bunge, Dar es Salaam.


Zitto alisema Kanuni za Bunge zinataka ukaguzi wa hesabu ya serikali huku akionya kuwa sio sahihi kwa vyama hivyo kulichukulia suala hilo kama jambo binafsi. Alisema chama husika kikishakaguliwa na ofisi ya CAG, na taarifa husika hupigwa muhuri wa ofisi hiyo ya mkaguzi.


Zitto alisema vyama hivyo vinatakiwa kuichukua taarifa hiyo na kuipeleka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye hutangaza taarifa hiyo katika gazeti la Serikali ili ijulikane wazi mapato ya vyama husika.


“Hilo ndio halijafanyika, waulizeni hao CCM, CUF na Chadema lini wamekaguliwa na kama wamekaguliwa mbona taarifa zao hazipo katika ofisi ya msajili, sisi tunatambua taarifa za ukaguzi wa vyama ambazo zipo ofisi ya msajili,” alisema Zitto na kuongeza:


“CCM na Chadema ndiyo wana kelele zaidi, hatuwezi kusimamia Serikali wakati sisi wenyewe ni wachafu, najua kila mtu alikuwa akiogopa kueleza ukweli kuhusu ukaguzi kwa vyama vya siasa, kuanzia CAG, Mwenyekiti aliyepita wa PAC hadi Msajili wa vyama.”

Alisema ruzuku za vyama hivyo ilitakiwa kusimamishwa tangu miaka mitatu iliyopita, kwa maelezo kuwa Sheria ya Vyama vya Siasa Ibara ya 14(4) inaeleza kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama ina uwezo wa kufungia ruzuku ya chama fulani, mpaka hapo kitakapowasilisha hesabu zake.

“Katika hili CAG na Msajili wa Vyama kila mtu atabeba mzigo wake, inaonekana kulikuwa na kuogopana lakini mimi nimekuwa Mwenyekiti wa PAC hivi karibuni lazima nisimamie sheria na hiyo ndiyo kawaida yangu,” alisema Zitto.
Msajili anena
Msajili wa Vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi alizungumza na gazeti dada la The Citizen juzi na kufafanua kuwa ofisi yake itayafanyia kazi maoni ya PAC na kuongeza kuwa uamuzi wowote utakaotolewa utafanyika kwa mujibu wa sheria za ofisi yake.

Alisema kuwa alipitia maoni yaliyotolewa na Zitto kuhusu vyama kufungiwa kupewa ruzuku na kwamba atayafanyia kazi licha ya kuwa pia alitoa maoni binafsi kuhusu suala hilo.

Alisema hawezi kuchukua hatua za haraka kuchukua hatua za kuvifungia vyama hivyo mpaka atakapokutana na Makatibu Wakuu wa vyama hivyo ambavyo vimetajwa na Zitto kwamba havijawasilisha ukaguzi wao.


“Nataka kuzungumza nao ili nijue kwanini wameshindwa kuwasilisha ukaguzi kabla ya kuamua kuchukua hatua za kisheria” alisema.

Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company