Jeshi la Marekani linasema kuwa wanajeshi wake wane wamejeruhiwa Sudan Kusini pale ndege yao ilipopigwa risasi karibu na mji wa Bor, wakijaribu kuwahamisha raia wao.
Ndege kadha zililazimika kurudi Uganda.
Jeshi la serikali ya Sudan Kusini linajaribu kuukomboa mji wa Bor, kaskazini ya mji mkuu, Juba, kutoka wanajeshi walioasi na kujiunga na makamo wa rais wa zamani, Riek Machar ambaye aliuteka mji huo Jumatano.
Siku hiyo pia Marekani ilipeleka wanajeshi 45 kuwalinda raia na mali ya Marekani Sudan Kusini.
Kwa mujibu wa gazeti la taifa la Uganda, New Vision,ndege mbili za jeshi la Uganda pia yalinasa katika tukio hilo.
Pamekuwa na taarifa kwenye vyombo vya habari kutoka Sudan Kusini kwamba ndege za Uganda piya zimekuwa zikiisaidia serikali kuukomboa mji wa Bor kutoka kwa wanajeshi walioasi - taarifa ambazo zinakanushwa na nchi zote mbili.