KUMEKUCHA;Kanda ya Ziwa waanzisha ‘genge’ kuratibu mgombea wao wa urais

Mwandishi Wetu      Mwanza NA RAIA MWEMA
BAADHI ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kanda ya Ziwa, wameandaa mkakati kuhakikisha Rais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, anatoka katika kanda hiyo, huku zikielezwa sababu nne zilizowasukuma kuwa na mtazamo huo wa kikanda.

Mgombea anadaiwa kuwa Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ambaye ni kutoka Kanda ya Ziwa. Magufuli anadaiwa na wafuasi wake hao kuwa amejizolea umaarufu miongoni mwa wananchi kutokana na utendaji wake wa kazi na wapo wanaodai amekubali kuwania nafasi hiyo ingawa bado hajaweka hadharani.

Taarifa zaidi ambazo bado hazijathibitishwa na Waziri Magufuli zinadai kwamba amekubaliana na masharti ya kundi hilo la kikanda.
Hata hivyo, kundi hilo limepata pigo baada ya aliyekuwa mwenyekiti wake katika kuratibu na kuwaweka pamoja wadau muhimu wa kundi hilo, Clement Mabina, kuuawa na wananchi wenye hasira mwanzoni mwa wiki iliyopita.

Katika kikao kilichofanyika kwenye moja ya hoteli zilizoko eneo la Capripoint jijini Mwanza asubuhi ya siku ya maziko ya aliyekuwa diwani wa Kisesa na Mwenyekiti wa zamani wa CCM, Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina, kilichowakutanisha mawaziri Samuel Sitta, Steven Wassira na John Magufuli, mikakati mipya ya kuendeleza harakati hizo baada ya Mabina kuuawa, iliazimiwa.

Mabina aliteuliwa kushika nafasi hiyo ya uratibu kwa sababu mbalimbali, moja ikiwa ni kutokuwa na uongozi katika chama na hivyo kumuwezesha kufanya mizunguko bila ya kushtukiwa au kusababisha maswali kutoka kwa viongozi wa juu wa chama.

Katika kutekeleza mkakati huo, baadhi ya viongozi wa Kanda ya Ziwa ambao tayari walikuwa wakionyesha nia ya kuwania urais mwaka 2015, wamefikiwa na kamati hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Mabina, ikielezwa kwamba wengi walikubali kumuunga mkono mgombea wao.

“Waziri Steven Wassira ni kweli alitangaza nia kwa wajumbe wa NEC mkoani kwake na alianza kupata uungwaji mkono katika baadhi ya mikoa na hata huko Zanzibar, lakini walimfuata na kumweleza kwa nguvu yake pekee, hawezi kumudu na ana vikwazo vingi kwa hiyo wakamwomba awaunge mkono na amekubali wako pamoja,” kilidai chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya kamati hiyo ya uratibu.

Wassira anadaiwa kukatishwa tamaa kuendelea na dhamira yake hiyo kwa sababu zinazodaiwa kuwa ni kutokuwa na vigezo vya kumudu nguvu ya upinzani, hasa kwa kuwa alikwipata kuwa mpinzani na kukisema vibaya Chama cha Mapinduzi kwa wananchi.

Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja naye anadaiwa kujiunga katika harakati hizo na hata kuahirisha harakati zake za awali za kutaka kuwania nafasi hiyo kwa msukumo wake binafsi.

Kambi hiyo ambayo imepata uungwaji mkono mpaka katika mikoa ya Tabora na Kigoma ambako wanasiasa machachari wa mikoa hiyo wamekubali kuiungana mkono ili kudhibiti kasi ya kundi lolote wanalodhani ni tishio dhidi ya malengo yao.

Moja ya sababu ya kupata nguvu kwa kambi hiyo ya Kanda ya Ziwa inatajwa kuwa ni kutokana na minyukano ya kisiasa ndani ya CCM, kiasi kwamba baadhi ya makada wake hawako tayari kuona kundi jingine likifanikiwa na hivyo kuwa tayari kuungana na kundi lolote lile ilimradi linaweza kukwamisha juhudi za kundi jingine.

Mbinu zinazotumiwa na kundi hilo kwa sasa ni kwa baadhi ya wafuasi wa kambi hiyo kutangaza kuwania nafasi ya urais na kuanza harakati za kuomba kura kwa wajumbe wa NEC na mkutano mkuu, lakini nyuma ya mkakati huo yupo mgombea maalumu wa kanda hiyo, ambaye anatakiwa lakini amezuiliwa asizungumzie masuala hayo ili atakapojitokeza wakati muafaka kuwe na nguvu kubwa na mvuto.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kanda hiyo iko katika mazungumzo ya kuungana na wenzao wa Nyanda za Juu Kusini ili wawe na nguvu ya pamoja katika kuamua nani anakuwa mgombea wa CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao.

“Lakini pia wana mpango mbadala, kama ikifika hatua mgombea wao anashindwa kupenya wataingia katika makubaliano na kanda anakotoka mgombea mwenye nguvu, ili aweze kubeba agenda zao na tayari yako mazungumzo na kanda ya Nyanda ya Juu Kusini na yanaendelea vizuri,” kinaeleza chanzo chetu cha habari ndani ya kamati hiyo ya urais wa kikanda.

Kanda ya Ziwa ambayo inatajwa kuwa na turufu muhimu ya kuamua mshindi katika vikao vya chama kutokana na idadi ya wajumbe wake, wameibua mambo manne ambayo wanataka kuyasimamisi kikamilifu.

Mambo hayo ni pamoja na kuwa na chuo kikuu cha umma katika Kanda ya Ziwa, kuifanya Mwanza mji muhimu kiuchumi katika ukanda wa maziwa makuu hasa katika kuboresha uwanja wake wa ndege na kuwa na nafasi muhimu katika vyombo vya uamuzi, ikiwamo Kamati Kuu ya CCM.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company