Wote twasherehekea, Maisha yake Mandela,
Maisha ya kiraia, Na alipokuwa jela,
Haya maisha murua, Alimjalia mola,
Maisha yake Mandela, Ni Urithi wa Dunia.
Aliishi kama mtu, Sio kama mungu mtu,
Hakutumia mtutu, Kuudhalilisha utu,
Alitumia mtutu, Kudai haki na utu,
Maisha yake Mandela, Ni Urithi wa Dunia.
Alidai ukombozi, Uhuru na haki pia,
Alipinga ubaguzi, Na mfumo dume pia,
Alikuwa kiongozi, Wa fikra na tabia,
Maisha yake Mandela, Ni Urithi wa Dunia.
Alikuwa na huruma, Kwa binadamu wenzake,
Ukweli aliusema, Akijenga hoja zake,
Raslimali za umma, Hakuzifanya za kwake,
Maisha yake Mandela, Ni urithi wa Dunia.
Usawa wa Binadamu, Ikawa imani yake,
Usikivu na nidhamu, Zikawa ni nguzo zake,
Woga pia Udhalimu, Vikawa miiko yake,
Maisha yake Mandela, Ni Urithi wa Dunia.
Mandela hakujikweza, Kwa maneno na tabia,
Mali hakulimbikiza, Na rushwa hakupokea,
Utu aliutukuza, Uovu alichukia,
Maisha yake Mandela, Ni Urithi wa Dunia.
Vita alivyoasisi, Ni vita vya ukombozi,
Kukomboa almasi, Na samaki wa Zambezi,
Vile vile kuziasi, Sera za ‘utandawizi’
Maisha yake Mandela, Ni urithi wa Dunia.
Nawausia vijana, Ishini kama Mandela,
Uchukieni utwana, Kama alivyo Mandela,
Ikibidi kupigana, Pigana kama Mandela,