Hali ya kibinadamu katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui inaripotiwa kuwa mbaya na baadhi ya ripoti zinasema kuwa, mji huo unakaribia kukumbwa na maafa ya kibinadamu.Taarifa zaidi zinasema kuwa, raia 30 elfu wameomba hifadhi katika Uwanja wa Ndege wa Bangui huku vikosi vya jeshi la Ufaransa vilivyoko nchini humo vikishindwa kurejesha amani. Asasi zisizo za kiserikali zinatahadharisha kwamba, mji huo unakaribia kukumbwa na maafa ya kibinadamu kutokana na kukosekana huduma muhimu kwa ajili ya mahitaji ya mwanadamu. Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limemuandikia barua Valerie Amos, Naibu Katibu Mkuu wa UN anayehusika na misaada ya kibinadamu likimtaka atume misaada ya kibinadamu katika mji wa Bangui.
Wakati huo huo, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani vikali machafuko na mapigano ya kikaumu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na kutoa wito wa kusitishwa mauaji nchini humo. Profesa Ekmeleddin Ihsanoglu, Katibu Mkuu wa OIC ameyataka makundi yanayopigana katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kuhitimisha mapigano na yaweka chini silaha na hivyo kutoa fursa ya kurejeshwa amani na utulivu nchini humo.
