
Ndugu zangu,
Tuanze na bashraf;
"Mandela anasimulia, kuwa alifungiwa kwenye selo (cell) ya peke yake. Na kwenye ukimya mkubwa, alianza kutafakari mikakati ya nini atakachofanya kesho yake. Ndipo akasikia sauti ya mtu akikohoa kwenye selo ya jirani.
Lakini, zaidi ya kukohoa, kulikuwa na cha ziada kwenye kukohoa kule. Ghafla Mandela alianza kuhusianisha kukohoa kule na mtu anayemfahamu mwenye kukohoa kwa namna hiyo. Mandela akabahatisha kwa kumwita mtu huyo kwa jina lake..." Endelea..
" Walter!" Aliita Mandela.
" Nelson, is that you!"- Nelson, ni wewe? Alijibu Walter kutoka upande wa pili wa ukuta unaotenganisha selo zao. Ni Walter Sithulu.
Hapo marafikia wawili hao wakaanza kicheko cha pamoja kilichochanganyika na hali ya kujisikia unafuu, kushangazwa, kukatishwa tamaa na kuwa na furaha.
Mandela akabaini, kuwa Walter naye alikamatwa mara tu baada ya yeye ( Mandela) kukamatwa. Wote wawili wakaamini kukumatwa kwao kulikuwa na mahusiano. Kwenye selo zile hakukuonekana kuwa mahala muafaka kwa wawili hao kukutana, lakini, usiku ule ulipita kwa Mandela kumpa taarifa nzima ya yeye ( Mandela) kukamatwa kwake. Mandela alimweleza Walter pia juu ya mkutano wake wa Durban.
Kulipokucha Mandela alifikishwa Mahakamani na kushtakiwa rasmi. Wapigananaji wenzake ndani ya ANC; Harold Wolpe na Joe Slovo nao walifika Mahakamani baada ya kusikia habari za kukamatwa kwa Mandela. Mandela alipata nafasi ya kuongea nao machache kwenye sakafu ya Mahakama.(P.T)
Mandela anasimulia, juu ya kumkumbuka Jaji wa Mahakama. Amekutana naye mara kadhaa kutokana na taaluma ya Mandela ya uanasheria. Mandela alipata kuwa Wakili wa Kujitegemea. Kwamba Mandela na Jaji huyo ni watu wenye kuheshimiana.
Mahakamani kulikuwa na idadi fulani ya wanasheria waendesha mashtaka ambao Mandela aliwafahamu. Baadhi yao Mandela aliwajua fika. Mandela alifikiri, kuwa ni ajabu kidogo kuwa mwanadamu unaweza kuingia katika jambo ambalo laweza kuonekana ni dogo. Kwamba, hapo Mandela alionekana kuwa ni mhalifu, mtu aliye kwenye namba moja ya orodha ya wenye kutafutwa kwa udi na uvumba na Serikali.
Sasa ni mhalifu aliyefungwa pingu na kuwa amekuwa akijificha kwa mwaka mmoja na zaidi, na bado, Jaji na wanasheria waendesha mashtaka wengine mahali hapo, ikiwamo baadhi ya waliokuja kushuhudia, wote wamemsalimia Mandela kwa namna ya kumheshimu, na pia kumsalimu kiweledi katika taaluma yao. kwao alikuwa Nelson Mandela mwanasheria, na sasa amefanywa kuwa mvunjifu wa sheria. Hayo yalimwongezea ari Mandela.
Na shauri lilipokuwa likiendeshwa, Jaji alionekana kuwa katika hali isiyo ya utulivu. Na wala hakumwangalia Mandela usoni. Na wanasheria wengine nao walionekana kufadhaishwa. Walijisikia hivyo si kwa vile ni Mwanasheria mwenzao kitaaluma aliyeletwa mbele yao. Bali, ni kwa vile Mandela alikuwa ni mtu wa kawaida anayeadhibiwa kutokana na imani na
mitazamo yake.
Mandela anasimulia, kuwa hakuwahi kuwa katika hali hiyo kabla. Hata hivyo, alilielewa jukumu alilotakiwa kulifanya mbele ya Mahakama kama mtu anayejitetea.
Kwamba yeye ( Mandela) alikuwa ishara ya haki mbele ya Mahakama ya wakandamizaji. Kwamba ni Mandela mwakilishi wa fikra kuu za Uhuru, Haki na Demokrasia katika jamii isiyoheshimu hayo.
Mandela anasema;
" I realized then and there that I could carry on the fight even within the fortress of the enemy."- Nelson Mandela. ( Long walk to Freedom, pg. 375-376)
Kwamba Mandela alibaini, kuwa angeweza kuendelea na mapambano hata ndani ya ngome ya adui.
Na Mandela alipoulizwa na Jaji wa Mahakama ataje jina la Wakili wake, naye alijibu;
" Mheshimiwa Jaji, nitajiwakilisha mwenyewe na Joe Slovo atakuwa mshauri wangu wa masuala ya kisheria".
Ni kwanini Mandela aliamua kujiwakilisha mwenyewe Mahakamani na si kumtumia Wakili?
Jibu utalipata leo kabla saa sita usiku.
0754 678 252
NA BLOGU YA MJENGWA.
