
Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian akiwa mjini BanguiAFP PHOTO/FRED DUFOUR
Na Flora Martin Mwano
Umoja wa Mataifa umesema kuwa watu zaidi ya mia sita wameuawa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati na wengine zaidi ya mia moja na hamsini na tisa wamesalia kama wakimbizi kwa kipindi cha wiki moja kutokana na mapigano baina ya Wakristo na Waislamu.
Msemaji wa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, Adrian Edwards amesema watu 450 wameuawa katika mji mkuu wa nchi hiyo Bangui na wengine 160 wameuawa katika maeneo mengine ya nchi hiyo.
Takwimu hizo zinakuja wakati Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian akizuru mjini Bangui siku ya ijumaa na kukutana na wanajeshi wa Ufaransa pamoja na viongozi wa serikali ya mpito.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki-moon ametoa wito kwa viongozi wa dini wa wa kimila nchini humo kujituma kama mabalozi wa amani ili kusaidia jitihada za kukomesha umwagaji damu unaoshuhudiwa hivi sasa.
Wakati huo huo mashirika ya misaada ya kibinadamu yameomba Umoja wa Mataifa kuongeza misaada zaidi kwa waathirika wa mapigano hayo mjini Bangui.
