
Ndugu zangu,
Katika simulizi hizi za Mzee Madiba, hakuna sehemu iliyonigusa zaidi kama hii niiandikayo sasa.
Kwa kumfuatilia Mandela kwenye simulizi zake na hususan kwa kupitia kitabu chake, hakika, najisikia ni kama mtu ninayemfahamu na niliyekutana nae. Hapana, sijapata kukutana wala kumwona moja kwa moja Nelson Mandela. Lakini, kupitia maandiko yake, najisikia ni kama mwanadamu niliyepata kukutana nae.
Naamini, hata kama maishani ningepata bahati ya kukutana na Mandela akiwa hai, basi, tungekuwa na ya kuongea kuhusiana na maudhui ya kwenye kitabu chake hiki; ' Long Walk to Freedom'.
Na tukio la kukamatwa kwake njiani akitokea Durban limenifanya nimwangalie Mandela kama mume na mzazi kama wengine. kama mume na mzazi, hisia alizokuwa nazo Mandela ni rahisi kuzielewa. Mandela ambaye, baada ya kuwa mbali na mkewe Winnie na wanawe kwa miezi mingi, hakusita kuelezea hisia zake, kwamba alitamani sana kurudi Johannesburg na kukutana na familia yake; mke wake mpenzi Winnie, na wanawe wapendwa pia . Ni Mandela baba, ambaye ndoto na matamanio yake hayo alijikuta yakikatishwa na Makechero wa Makaburu. Inahuzunisha sana.
Mara baada ya kukamatwa, Mandela alijiuliza maswali mengi. Na swali kuu ni hili; Ni nani aliyewapa taarifa polisi na kuwawezesha kumkamata?
Pale kituo cha polisi Mandela aliwaona polisi waliokuwa na furaha ya kukamatwa kwake. Mandela anasimulia;(P.T)
Kuwa muda wote akiwa na polisi hakukiri jambo lolote isipokuwa kusema anaitwa David Motsamayi. Na askari mmoja kwa jina la Truter na ambaye alimfahamu Mandela kabla alimwambia Mandela;
" Nelson, kwanini husemi ukweli? Unajua kwamba mimi nakujua. Na sote hapa tunajua wewe ni nani".
Mandela alimwambia askari yule, kuwa jina hilo la David ni jina la kupewa, na ndilo analosimama nalo kwa wakati huo. Mandela aliomba apatiwe Mwanasheria, ombi lake hilo lilikataliwa. Naye Mandela akakataa kutoa maelezo yake polisi.
Mandela anasimulia;
" Cecil na mimi tulifungiwa kwenye vyumba tofauti. Ni katika wakati huu nimeweza kutafakari zaidi hali yangu. Siku zote nimekuwa nikijua kuwa kuna siku naweza kukamatwa, lakini, wapigania ukombozi hujifunza pia kukana.
Na nikiwa kwenye chumba kile cha selo usiku ule, nikabaini, kuwa sikuwa tayari na uhalisia wa kukamatwa na kukiri. Nilijawa na hasira. Kwamba kuna mtu amewaambia polisi kuhusu mahali nilipo. Polisi walijua kuwa niko Durban, na kwamba ningerudi Johannesburg.
Mke wangu, Winnie, naye wamemsumbua sana, wakiamini kuwa ana taarifa zangu, na kuwa alijua lini ningerudi nyumbani. Najua Makachero wamekuwa wakimfuatilia ( Winnie) na hata kufika nyumbani na kupekua nyumba mara kadhaa. Nahisi walijua kuwa ningepanga kumtembelea Chifu Luthuli mara tu baada ya kurudi Afrika Kusini kutoka ziara yangu. Na walikuwa sahihi. Na nadhani walijua pia kuwa nilikuwa Durban.
Inaonekana ANC imevamiwa na ' Mapandikizi' watoa taarifa kwa Makachero." Anasimulia Mandela.
Hata hivyo, pamoja na kuzama kwenye fikra hizo. Mandela aliukubali ukweli, kuwa, kwa hali aliyokuwa nayo, kufikiri sana juu ya nani ' amemchoma' kwa Makachero ni kupoteza muda. Na kwa vile Mandela alichoka sana kimwili na kiakili, mara alijikuta akilala usingizi mzito.
Na Mandela anasimulia, kuwa walau usiku ule wa Agosti 5, 1962 hakuwa na sababu ya kuwa na mashaka kama polisi watamkamata au la. Polisi walikuwa wameshamkamata.
Na kulipokucha, siku ya pili yake, saa mbili na nusu asubuhi, Nelson Mandela akajikuta akiwa amesimamishwa kizimbani kwenye Mahakama ya Mwanzo. Na baadae akaingizwa kwenye 'Karandinga' kwa safari ya Johannesburg. Safari ya kwenda kwenye Mahakama ya juu na kusomewa mashtaka rasmi.
Ni nini kilitokea Mahakamani?
Jibu utalipata leo asubuhi.
0754 678 252
NA BLOGU YA MJENGWA.
