Kibanda aibwaga Serikali, Ni katika kesi ya uchochezi iliyomhusisha pia Makunga, Mwigamba

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemwachilia huru Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini, Absalom Kibanda, na wenzake waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kuandika na kuchapisha makala ya uchochezi kwenye gazeti la Tanzania Daima Jumatano.
Mbali ya Kibanda ambaye kwa sasa ni Mhariri Mtendaji wa magazeti ya New Habari Corporation (2006) Ltd, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya kihistoria ni Meneja Uendeshaji Biashara wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, Theophil Makunga, ambaye wakati anashitakiwa, alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mwananchi Communications Ltd.

Makunga alikuwa akitetewa na mawakili Isaya Matambo, Nyaronyo Kicheree, John Mhozya na Mabere Marando.

Mshitakiwa wa tatu ni Samson Mwigamba, ambaye ndiye aliyekuwa mwandishi wa makala hiyo iliyobeba kichwa cha habari: ‘Waraka maalumu kwa askari wote’, iliyochapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumatano la Novemba 30, mwaka 2011.

Hukumu ya kesi hiyo iliyovuta hisia za wengi na iliyokuwa ikisubiliwa kwa shauku kubwa na wadau wengi wa habari wa ndani na nje ya nchi, ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Waliarwande Lema.

Katika hukumu hiyo iliyochukua takriban saa mbili, Hakimu Lema alisema mtu yeyote aliyeisoma makala inayodaiwa kuwa ni ya uchochezi na mwenye akili timamu, hawezi kamwe kusema ni ya uchochezi, hivyo hakukuwa na sababu ya kufungua kesi ya uchochezi.

Kabla ya kusoma hukumu hiyo, Hakimu Lema alianza kwa kuishangaa serikali iliyofungua kesi hiyo kushindwa kuleta majumuisho ya mwisho kwa maandishi na hadi jana wakati anasoma hukumu hiyo upande wa utetezi tu ndio ulioleta majumuisho ya mwisho.

“Itakumbukwa kuwa Desemba mwaka jana washitakiwa walipomaliza kujitetea, mahakama hii ilitoa amri kwa pande zote kuleta majumuisho ya mwisho kwa maandishi lakini hadi hivi leo mahakama hii inavyotoa hukumu, upande wa utetezi tu ndio ulitekeleza amri ya kuleta majumuisho yao ya mwisho na kwa masikitiko makubwa upande wa Jamhuri haukutekeleza amri hiyo, yaani haujaleta majumuisho yao na umeshindwa hata kutoa sababu, lakini hilo halizuii mahakama kutoa hukumu yake,” alisema Lema na kusababisha watu kushikwa butwaa.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Lema alianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa hati ya mashitaka ilikuwa na jumla ya makosa mawili, kosa la kwanza likikuwa la kuandika makala ya uchochezi kinyume cha kifungu cha 32(1) (c) na 31 (1) (a) cha Sheria ya Magazeti sura ya 229 ya mwaka 2002.

Kosa hilo lilikuwa likimkabili mshitakiwa Kibanda na Mwigamba, ambapo walidaiwa kuwa Novemba 30 mwaka 2011, kwa makusudi waliandika makala hiyo iliyodaiwa na serikali kuwa ni ya uchochezi na ilikuwa na nia ovu ya kuhamasisha askari wasitii amri zinazotolewa na viongozi wao.

Kosa la pili ni la kuchapisha makala hiyo iliyodaiwa kuwa ni ya uchochezi ambalo lilikuwa likimkabili Makunga peke yake.

Katika kosa hilo, Makunga anadaiwa kuchapisha makala hiyo ya uchochezi kinyume cha sheria.

Ili kuthibitisha tuhuma hizo, alisema upande wa mashitaka ulileta mashahidi watatu na upande wa utetezi ulileta wanne.

Alisema katika kesi hiyo upande wa serikali umeshindwa kuleta ushahidi wa kuthibitisha pasipo kuacha shaka yoyote kwamba washitakiwa wametenda kosa.

Alisema upande wa mashitaka uliokuwa ukiongozwa na mawakili wa Serikali, Prosper Mwangamila na Elizabeth Kaganda umeleta ushahidi dhaifu na hafifu, ambao umeshindwa kuishawishi mahakama yake iwaone washitakiwa wote wana hatia katika kesi hiyo.

Alisisitiza kuwa utetezi wa serikali umeshindwa kuthibitisha madhara yaliyotokea baada ya makala hiyo kuchapishwa na madhara yenyewe ni kama kulikuwa na kundi la watu lilipanga kufanya vurugu, au kuna askari walikataa kutii amri za viongozi wao.

“Upande wa serikali umeshindwa kuleta ushahidi kuthibitisha kuwapo madhara yaliyojitokeza ndani ya majeshi baada ya makala kuchapishwa na kwa mujibu wa mashahidi wa upande wa Jamhuri ambao ni mlalamikaji wa kesi na mpelelezi wa kesi hiyo ofisa wa Polisi, David Hizza na Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza, George Mwambashi, waliieleza mahakama kuwa hakukuwa na madhara yoyote ndani ya majeshi yao yaliyosabishwa na makala hiyo kwani askari wengi walikuwa hawajaisoma.

“Ukilisoma shitaka la kwanza la kuandika makala ya uchochezi linalomkabili Mwigamba na Kibanda, na Mwigamba alivyojitetea na kueleza kuwa aliandika makala hiyo akiwa Arusha na kuituma katika chumba cha habari kinachochapisha gazeti la Tanzania Daima, upande wa Jamhuri umeshindwa kuleta ushahidi unaoonyesha makala hiyo kweli iliandikwa na Mwigamba, na alivyoiandika alikuwa na nia ovu ya kutaka ufanyike uasi ndani ya majeshi, pia umeshindwa kuonyesha Kibanda alishiriki vipi kuiandaa makala hiyo kwani Kibanda katika utetezi wake alieleza wakati makala hiyo inachapishwa na kuhaririwa alikuwa nje ya Dar e Salaam na hakuna ushahidi wa Jamhuri uliotolewa kupinga utetezi wa Kibanda,” alisema Hakimu Lema.

Alisema shahidi wa Jamhuri Hizza, katika ushahidi wake alidai yeye alipoisoma makala hiyo aliona ni ya uchochezi na akaenda kutoa taarifa kwa wakubwa wake, ambao nao waliisoma na kuiona ni ya uchochezi, hivyo wakamtaka Hizza awe mpelelezi wa kesi.

Hakimu Lema alisema Hizza alimuita Kibanda katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na kumhoji na kisha akawa shahidi katika kesi hiyo, lakini cha kustaajabisha shahidi huyo ameshindwa kuleta mahakamani maelezo aliyomhoji Kibanda akiwa polisi na badala yake shahidi huyo akaeleza mahakama kuwa eti Jeshi la Polisi wameamua kukaa na maelezo hayo kwa manufaa yao.

“Kisheria pale mtu zaidi ya mmoja anaposhitakiwa kwa kosa moja, lazima upande wa Jamhuri ulete ushahidi unaoonyesha kila mshitakiwa alishiriki vipi kutenda kosa hilo lakini katika kesi hii upande wa Jamhuri umeshindwa kufanya hivyo,” alisema Hakimu Lema.

Akilichambua kosa la pili la kuchapisha makala ya uchochezi lililokuwa likimkabili Makunga peke yake, Hakimu Lema alisema upande wa serikali umeshindwa kuleta ushahidi wa moja kwa moja unaoonyesha Makunga ndiye aliyechapisha makala hiyo.

Aliongeza kuwa kwa bahati mbaya shahidi wa Jamhuri ambaye ni Msajili wa Magazeti, Rafael Hokororo, katika ushahidi wake alioutoa mahakamani hapo, alishindwa kusema kuwa makala hiyo ni ya uchochezi na hakuwahi kumuita Mhariri Mtendaji wa gazeti la Tanzania Daima (Kibanda), lililochapisha makala hiyo kumhoji kutokana na makala hiyo ya uchochezi.

“Mimi kama hakimu ni maoni yangu kuwa washitakiwa walishitakiwa kwa hisia tu na hisia zinakatazwa kumfungulia mtu kesi mahakamani …kwani hata huyu mpelelezi wa kesi hii Hizza alipaswa alete ushahidi unaoonyesha nani aliandika makala, nani alihariri makala hiyo na ni nani aliichapisha makala hiyo…mtu mwenye akili timamu ambaye aliisoma makala hiyo hawezi kusema makala hiyo ni ya uchochezi wala kuwafungulia washitakiwa hao kesi ya uchochezi mahakamani,” alisema Hakimu Lema.

Aidha, alisema mwandishi wa makala hiyo Mwigamba aliandika kwa nia njema tu ya kuwakumbusha askari majukumu yao na alikuwa akiitumia haki yake ya kutoa maoni iliyoainishwa kwenye Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Alisisitiza kuwa makala ya Mwigamba ilikuwa na nia njema ya kuwakumbusha askari wa majeshi ya Tanzania kutenda kazi zao kwa kufuata haki na kuheshimu haki za watu wengine za kushiriki maandamano.

Huku akisikilizwa kwa makini na umati wa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi, Hakimu Lema alisema Mwigamba aliandika makala hiyo kwa sababu alikuwa akikemea mauaji yaliyofanywa na polisi Januari 5, mwaka 2011 jijini Arusha ambapo polisi iliwaua watu watatu waliokuwa wakishiriki maandamano yaliyokuwa yameandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

“Hivyo nawaachilia huru washitakiwa wote chini ya kifungu cha 235 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002,” alisema Hakimu Lema na kuibua shangwe.

Akizungumza nje ya viwanja vya mahakama, Kibanda alisema kwanza anamshukuru Mungu kwa kushinda kesi hiyo ambayo imemsumbua kwa miaka miwili.

Alisema hukumu hiyo imeonyesha wazi kuwa kumbe ni kweli mahakama zetu zinatoa haki na kuwashukuru wanahabari na wadau wa habari waliokuwa naye bega kwa bega wakati wa kesi hiyo.

Naye wakili wa Kibanda, Nyaronyo Kicheere, alisema kesi hiyo ni ushindi kwa tasnia ya habari na kwamba waandishi wa habari wana haki ya kuandika makala za kuwakosoa askari wa majeshi yetu kwani ni kodi zetu ndizo zinazowalipa mishahara.

Naye Meneja Maadili wa Baraza la Habari (MCT), Allan Lawa, alieleza kuwa hukumu hiyo ni ushahidi tosha wa vita ya uhuru wa habari inayopiganwa na vyombo vya habari nchini, ambayo imeainishwa wazi kwenye Ibara ya 18 ya Katiba ya nchi.

Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari walifurika mahakamani hapo tangu asubuhi, wengine wakisali kwa imani zao na baada ya Hakimu Lema kutoa hukumu yake na kuwaachilia huru waandishi hao walikumbatiana kwa furaha na kumshukuru Mungu na kumpongeza Hakimu Lema kwa kutoa hukumu ambayo imerejesha faraja na amani kwa tasnia ya waandishi wa habari hapa nchini.

Itakumbukwa kuwa Mwigamba, Kibanda na Makunga walifikishwa mahakamani kwa siku tofauti.

Mwigamba alifikishwa mahakamani hapo mara ya kwanza Desemba 8, mwaka 2011, Kibanda alifikishwa Desemba 20, mwaka 2011 na Makunga alifikishwa Machi 6, mwaka 2012 na washitakiwa wote walikanusha mashitaka.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company