Huyu hapa ndie Daktari feki wa Muhimbili

NA SAMSON FRIDOLIN

Kitano Mustafa Kitano (51) ambaye amekamatwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam jana akidaiwa kujifanya daktari akizungumza baada ya kuwekwa chini ya ulinzi.Picha/Omary Fungo
Mtu mmoja amekamatwa na maofisa usalama wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa tuhuma za kuwatapeli watu mbalimbali wakiwamo wagonjwa kwa kujifanya ni daktari.Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo jana, Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa MNH, Aminieli Eligaesha alisema kukamatwa kwa mtu huyo kunafuatia mtego uliowekwa na uongozi wa hospitali baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema juu ya vitendo vyake.

Alimtaja mtu huyo kwa jina la Kitano Mustafa Kitano, kwamba amekuwa akiendesha shughuli za kitapeli hospitalini hapo kwa muda mrefu huku akijidai kuwa ni daktari wa uzazi.

Alisema Februari 22, mwaka huu, Kitano alimpigia simu mkazi wa Kivule, jijini Dar es Salaam, Hussein Haji, na kumwambia kuwa kuna nafasi za kazi MNH na yeye (Kitano) atamuunganishia ili apate nafasi hiyo huku akimtajia vigezo kuwa awe na cheti cha kidato cha nne pamoja na leseni ya udereva, na kumtajia kiwango cha mshahara cha kazi hiyo kuwa ni Sh. 570,000 na posho ya Sh. 90,000 kwa siku.

Eligaesha alieleza kuwa Kitano alimwambia Haji kuwa MNH ina kitengo Kahama mkoani Shinyanga, ambacho kinashughulika na watu walioathirika na maji ya migodini, lakini Haji alimwambia hana elimu ya kidato cha nne, hata hivyo (Kitano) alimwambia amtumie namba ya cheti na Sh, 200,000 ili ampatie kazi hiyo.

Kwa mujibu wa Eligaesha, daktari huyo bandia amekuwa akionekana sana kwenye maeneo ya hospitali hiyo, huku watu wengi wakidhani kuwa ni daktari wa MNH.

Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa na vitu vinavyoashiria kuwa ni daktari zikiwamo kadi tatu za kliniki za MNH za wagonjwa mbalimbali, kitambulisho cha mtu aitwaye Peter Daniel wa Riki Hotel pamoja na vipimo vya kupimia mimba.

Aidha, kwenye simu yake ya mkononi zilikutwa namba nyingi za madaktari wa MNH pamoja na namba za wafanyakazi wa maabara, pamoja na wauguzi.

RAIS TMA ASIKITIKA
Rais wa Chama Cha Madaktari Tanzania (TMA), Dk. Primus Saidia, alisema ni jambo la kusikitisha kuona kuwa hata fani ya udaktari sasa imevamiwa na makanjanja na kuongeza kuwa hali hiyo ikiachiwa iendelee inaweza kuleta athari kubwa kwa wagonjwa na kwa fani ya udaktari.

Alisema hali hiyo inahatarisha afya za wananchi na kuwataka madaktari wanapomuona mtu na kumtilia shaka watoe taarifa haraka ili akamatwe mara moja badala ya kuendelea kuvichekea vitendo hivyo.

ALIYETAKA KUTAPELIWA ANENA
Kwa upande wake, Haji alisema Februari 21, mwaka huu saa 4:00 asubuhi alipigiwa simu na shemeji yake aliyemtaja kwa jina moja la Ally, ambaye alimweleza kuwa kuna rafiki yake amemwambia kuwa kuna kazi MNH na kumpa namba ya huyo mtu ili awasiliane naye.

Alisema baada ya kuwasiliana naye kwa kupitia namba hiyo, mtu huyo alijitambulisha kwa jina la Dk. Koba wa MNH na kumtajia vigezo vya kazi hiyo kuwa ni cheti cha kidato cha nne pamoja na leseni ya udereva, na kwamba kwa wakati huo alikuwa anataka awaite wajumbe wanaohusika na suala hilo la kazi akiwamo ofisa utawala ili wamjadili.

Alifafanua kuwa baadaye Dk. Koba alimwambia atoe Sh. 200,000 ili wampatie kazi hiyo, lakini yeye (Haji) akawaambia kuwa hana na ndipo akamwambia kuwa kesho yake aende huku akiwa amevaa vizuri kwani kazi hiyo inahitaji unadhifu. Baada ya kupewa maelekezo hayo ndipo alipoamua kumuuliza ofisa usalama mmoja wa MNH kama anamfahamu Dk. Koba.

Haji anasema kuwa askari huyo alimshauri waweke mtego, na ndipo akampigia tena na alipopokea alidai atampigia baadaye kwa kuwa wakati huo alikuwa kwenye kikao na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Alisema baadaye alipigiwa simu na Dk. Koba na kumwambia aende Muhimbili na baada ya kufika, askari walimtia mbaroni.

Mzee Hassan Madika, mkazi wa Mwananyamala, alisema anamfahamu mtu huyo kwa jina la Dk. Nyirabu kwa muda wa miaka mingi na kwamba alikutana naye hospitalini hapo alipokwenda kuomba nafasi ya kukutana na daktari wake wa moyo.

MTUHUMIWA AZUNGUMZA
Kitano alidai kuwa amebambikiziwa kesi na wala hafahamiani na Haji wala hajawahi kuonana naye na kwamba anashangaa kuambiwa kuwa alitaka kumtapeli kiasi hicho cha fedha.

Kitano alidai kuwa yeye ni ofisa tabibu kwa miaka mingi ambaye amewahi kufanya kazi kwenye hospitali mbalimbali zikiwamo Mwananyamala, Amana, Mnazi Mmoja na Temeke kabla ya kustaafu na kujiunga na Mkapa Foundation inayojihusisha na msuala ya Ukimwi.

Kitano aliendelea kudai kuwa kwa sasa anajihusisha na masuala ya Ukimwi na huenda MNH kila mara kwa ajili ya kuwaona wagonjwa wake.

WAFANYAKAZI WADUWAA
Wafanyakazi wengi wa MNH walijitokeza kwa wingi ili kumuona daktari bandia huku wengi wao wakionyesha mshangao kwa kuwa ni mtu ambaye wanadai amekuwa akionekana sana hospitalini hapo akiwa na watu mbailimbali wakiwamo wagonjwa wanaokwenda kutibiwa hospitalini hapo.

Kwa mujibu wa Eligaesha, mtu huyo ni daktari bandia wa nne kukamatwa hospitalini hapo.

CHANZO: NIPASHE
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company