Mwenyekiti wa muda Bunge la Katiba kuchaguliwa leo

NA WAANDISHI WETU

Katibu wa Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania,Dk.Thomas Kashililah
Wajumbe wa Bunge la Katiba, leo watamchagua mwenyekiti wa muda atakayesimamia uandaaji na upitishaji wa kanuni na michakato mbalimbali, ikiwamo uchaguzi wa mwenyekiti na makamu wake wa kudumu wa Bunge hilo.Mwenyekiti wa kudumu wa Bunge hilo na makamu wake, pamoja na mambo mengine, watakuwa na jukumu la kusimamia majadiliano katika Bunge hilo, ambalo litapitisha Rasimu ya Katiba Mpya.

Katibu wa Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania, Dk. Thomas Kashililah, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jana. Alisema uchaguzi huo utafanyika kuanzia saa 8:00 mchana.

“Kikao cha kesho (leo) asubuhi hakitakuwa na mwenyekiti, kwa hiyo kitaongozwa na makatibu wa Bunge na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, baadaye sisi tutarajie jina la mtu akatakayekaa kwenye kiti kuongoza mchakato wa kumpata mwenyekiti wa muda,” alisema Dk. Kashililah.

“Sisi ni wasimamizi wa uchaguzi, hivyo tutaendelea kuwa wasimamizi wa uchaguzi…uchaguzi wa mwenyekiti na makamu wake tunasubiri kanuni zitakazopitishwa na wajumbe.”

“Ili zitungwe ni lazima wachaguliwe mwenyekiti na makamu wake wachaguliwe na wajumbe wenyewe…kesho (leo) makatibu tumepewa dhamana ya kuongoza kikao kwanza tu.”

Kesho na Alhamisi kutakuwa na kikao cha kazi ya kuandaa Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalum itakayofanyika nje ya Bunge na Ijumaa kutakuwa na kikoa cha azimio la kuridhia Kanuni za Bunge na uchaguzi wa mwenyekiti wa kudumu na makamu wake.

Wote wataapa kiapo pamoja na wajumbe wa Bunge Maalumu Jumamosi.Jumapili hadi Jumatatu asubuhi na jioni yake ufunguzi rasmi.

Dk. Kashililah alisema vituo vyote vya televisheni vinaruhusiwa kuwasilisha maombi ya kurusha matangazo ya vikao vya Bunge moja kwa moja baada ya kukamilisha taratibu za kufanya hivyo.
CHANZO: NIPASHE
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company