ULINZI WA IMARISHWA BUNGENI,MBWA KILA KONA

Na Habel Chidawali na Sharon Sauwa, Mwananchi
Dodoma. Ulinzi katika majengo na viunga vya Bunge umeimarishwa. Tangu jana idadi ya askari polisi imeongezeka.
Wanausalama hao wakiwa na farasi pamoja na mbwa, wamekuwa wakizunguka katika maeneo mbalimbali yanayozunguka eneo la Bunge. Kuimarishwa kwa ulinzi katika kipindi hiki cha Bunge la Katiba, kunatofautiana na ulinzi katika mikutano mingine ya Bunge. Hii ni mara ya kwanza kuwapo kwa ulinzi wa aina hii.
Upande wa Kaskazini mwa jengo la Bunge, ambako kuna Barabara ya Dodoma - Morogoro, askari wakiwa na mbwa na wengine silaha, walikuwa katika doria huku magari yaliyokuwa yamezoeleka kuegeshwa katika maeneo hayo yakitafutiwa sehemu nyingine hivyo kuacha eneo hilo wazi.


Jana asubuhi, wajumbe walipewa maelezo kuhusu utaratibu mzima katika kipindi chote watakachokuwapo bungeni ikiwa ni pamoja na jinsi watakavyoketi. Utaratibu huo umepangwa kwa kuzingatia herufi za mwanzo za majina ya wajumbe.


Mkuu wa Kitengo cha Uhasibu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, George Seni alisema wajumbe hao wameshalipwa posho ya kujikimu Sh80,000 kuanzia Februari 16 hadi Februari 28 mwaka huu na kwamba kuanzia Februari 28 mwaka huu, watalipwa kila wiki kupitia akaunti zao. Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema hakuna mjumbe atakayelipwa kama hatahudhuria.


Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Kitolina Kippa alisema kwamba wajumbe hao hawajaajiriwa. Hivyo hawatapata kiinua mgongo mwisho wa Bunge hilo.


Aliwatahadharisha wajumbe hao kuwa makini katika maeneo wanayolala... “Msiende katika maeneo yatakayohatarisha maisha yenu.”
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company