
Tangazo mojawapo katika kuta za Kituo cha Afya Kilwa Masoko.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi limeingia lawamani baada ya kuruhusu baadhi ya matumizi yanayodaiwa kutowagusa wananchi wake moja kwa moja huku huduma nyingi muhimu zikitelekezwa kwa madai ya kukosekana kwa fedha.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE umebaini kuwa miongoni mwa matumizi yanayolalamikiwa na wananchi ni pamoja na ukarabati mkubwa wa nyumba ya mkurugenzi uliogharimu Sh. milioni 230 na nyingine mbili za watumishi wa halmashauri hiyo zilizogharimu jumla ya Sh. milioni 260.
Mbali na nyumba hizo ambazo kwa ujumla zimeigharimu halmashauri ya Kilwa Sh. milioni 490, baadhi ya wananchi wamekuwa pia wakilalamikia ujenzi wa banda la maonyesho la halmashauri hiyo lililopo Ngongo ambalo linadaiwa kutafuna Sh. milioni 200.
Baraza hilo pia limelalamikiwa kwa kuruhusu ununuzi wa jenereta kwenye ofisi za halmashauri hiyo uliogharimu Sh. milioni 46 huku likiishia kupanga fedha tu bila kusimamia utekelezaji wa ukarabati wa kituo cha afya cha Kilwa Masoko ambacho kiko katika hali mbaya na kuonekana kuwa ni kama jengo la ‘makazi ya popo’.
Sehemu ya fedha zinazotumiwa kutekeleza vipaumbele hivyo vyenye utata hutokana na tozo la kodi ya huduma ya gesi asilia (service levy) ambayo hulipwa kwa halmashauri hiyo kila baada ya robo ya mwaka wa fedha na wawekezaji, kampuni ya Pan African Energy (PAT) inayovuna gesi ya kuzalishia umeme katika Kisiwa cha Songosongo.
Aidha, hata bandari ya Kilwa Kivinje inayotegemewa kwa kiasi kikubwa na wananchi wa Kisiwa cha Songosongo kinachoiingizia halmashauri hiyo mamilioni ya fedha kutoka PAT, imeendelea kuwa katika hali mbaya kwa kukosa choo wala sehemu ya kupumzikia abiria.
Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wilayani humo wamesema kwa kiasi kikubwa, madiwani wao ndiyo wanaopaswa kulaumiwa kwa vile huishia tu kuzungumza kuhusu ukarabati wa kituo chao cha afya cha Masoko, lakini bila kusimamia utekelezaji wake kwa madai kwamba hakuna fedha.
“Hali ya kituo chetu cha afya (Masoko) ni mbaya sana. Ona mwenyewe... dari linaporomoka, paa linavuja, kuta zimechakaa na ukishikwa na haja ndiyo balaa. Choo hakifai kabisa na kwa bahati mbaya ndicho hicho kinachotumiwa pia na kina mama wanaojifungulia hapa,” alisema Agnes Alex ‘Mama Aaron’, mkazi wa Masoko aliyekuwa amemfikisha mtoto wake kituoni hapo ili atibiwe malaria.”
“Watumishi wa hiki kituo wanajitahidi, lakini jengo lenyewe limebaki kuwa gofu. Ni aibu kwa serikali kwa sababu hakipo mbali kutoka kwenye jengo la halmashauri yetu,” aliongeza.
Fatma Kassim ‘Mama Abdulrazak’, alisema viongozi wao wanapaswa kumuogopa Mungu kwa kutenga fedha kushughulikia kituo hicho cha afya kinachopaswa kuhudumia maelfu ya wakazi wa mji wao wa Masoko.
“Wodi ya wanaume ndo haifai kabisa... dari limeporomoka na mvua ikinyesha huwa ni balaa. Viongozi wetu wamuogope Mungu kwa kutumia fedha wanazopata kwenye gesi kukarabati kituo hiki,” ‘Mama Abdulrazak’ ambaye pia alimfikisha mwanawe kituoni hapo.
Mwajuma Yusuf (Mama Salma), alidai kuwa hali mbaya ya jengo na ukosefu wa vifaa katika kituo hicho huwalazimu watu wengi kwenda kufuata huduma katika hospitali (binafsi) za Bakwata na Arafa.
“Hapa hapafai. Pamekuwa gofu, lakini sisi tusiokuwa na uwezo hatuna namna, Alu (dawa za mseto) zinapatikana kuanzia tarehe 1 hadi 5 za mwanzo wa mwezi tu, sindano pia shida,” alisema Yusuf Nditu ambaye naye alifika kwenye kituo hicho kuumpeleka mwanawe aliyekuwa akisumbuliwa na homa.
Ismail Slim, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii ya Mji Mdogo wa Kilwa Masoko, anathibitisha kuwa hali ya kituo chao ni mbaya, lakini matumaini yao bado yapo kwenye Baraza la Madiwani.
“Kila mara huwa tunaambiwa kuna fedha zimeombwa kukarabati kituo hiki, lakini mwisho wa siku huwa hakuna kinachoonekana. Kuna wakati hata michoro ya jengo ilitolewa, lakini utekelezaji unaonekana kuwa mgumu kwa vile hakuna fedha. Kama ni uwezo wangu, ningeshauri madiwani watenge fedha walau kidogo kutoka kwenye hizi za gesi zinazoingia kila baada ya miezi mitatu ili ufanyike ukarabati mdogo na kuwasaidia wananchi wakati tukisubiri huo ukarabati mkubwa,” alisema Slim.
Selemani Said, mkazi wa kisiwa cha Songosongo alisema ni vyema halmashauri yao ikatumia sehemu ya fedha za gesi zinazolipwa na PATkuwajengea walau choo na sehemu ya kupumzikia katika Bandari ya Kilwa Kivinje inayotumiwa na watu wengi kufika kisiwani kwao kwani hali iliyopo sasa ni mbaya.
Uchunguzi zaidi uliofanywa na NIPASHE umebaini kuwa fedha zitokanazo na tozo la kodi ya huduma zilizolipwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa na PAT kuanzia Aprili 13, 2012 hadi k Desemba 2013 zilikuwa ni Sh. bilioni 1.549, achilia mbali Sh. milioni 200 zinazodaiwa kulipwa kimakosa katika manispaa moja nchini na uongozi wa Halmashauri ya Kilwa bado unazifuatilia.
Hata hivyo, fedha hizo za ‘service levy’ bado hazijasaidia maeneo kadhaa muhimu, ikiwa ni pamoja na kuboresha kituo hicho cha afya cha Masoko ambacho hutegemewa na wakazi zaidi ya 13,000, kwa mujibu wa ripoti ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 ambayo inaonyesha kuwa kati ya wakazi 13,601 wa Mji Mdogo wa Masoko, wanaume ni 6,462.
Aidha, mwandishi wa NIPASHE alithibitishiwa kuwa Sh. milioni 30 zilizopatikana kutoka katika ‘service levy’ ya gesi zilitumika kufanya ukarabati mkubwa wa nyumba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo ambayo kwa ujumla, gharama zake zinadaiwa kufikia Sh. milioni 230.
Nyumba hiyo iko katika eneo wanalokaa vigogo wengi wilayani humo liitwalo Jimbiza, barabara ya Hamjambo, jirani na Bahari ya Hindi na ilikarabatiwa kwa kuibomoa kabisa nyumba iliyokuwapo awali na kuijenga upya.
ITAENDELEA KESHO
*Habari hii imekamilika kwa ufadhili wa TMF
CHANZO: NIPASHE
