Siasa noma mbio za urais sumaye aitisha ccm

MBIO za urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), zimezidi kuibua mambo mapya, baada ya
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, kudai
atachukua uamuzi mgumu kama chama chake
kitateua mgombea urais asiye na sifa.
Akizungumza Radio Tumaini, mjini Dar es Salaam
jana asubuhi, Sumaye alisema kama CCM itafanya
mambo ya ajabu kwa kuteua mgombea
asiyekubalika wala kuwa na sifa za kiongozi
mwadilifu, atafungua ukurasa mpya.
"Nitachukua uamuzi mgumu kama CCM watateua
mgombea ambaye hana sifa ya kuwaongoza
Watanzania, nitachukua uamuzi mgumu,
haiwezekani tukaongozwa na watu wanaotoa
fedha nyingi kila kukicha.
"CCM wakifanya mambo ya ajabu kwa kuchukua
mtu ambaye ametoa fedha, nitatafuta njia
nyingine," alisema.
Alisema hata siku moja hatakuwa na kinyongo
kama atateuliwa mtu safi na mwenye moyo
mweupe wa kusaidia Watanzania.
Alipoulizwa swali kama atagombea urais, alisema
"Mimi sisemi kama nagombea, nakwambia muda
ukifika nitasema tu, kwa wakati huu naomba
tuendelee kutulia kwanza.
"Muda ukifika nitaamua nini cha kufanya, unajua
unapotaka kuchukua uamuzi huu kuna mambo
mazito ambayo unapaswa kuyatafakari kwa
undani zaidi.
"Miongoni mwa mambo haya, ni kusaidia
Watanzania kutoka walipo ili wapige hatua moja
mbele zaidi, kuachana na tabia ya mtu mmoja
kujitajirisha kupita kiasi," alisema Sumaye.
Alisema kama Watanzania wakimhitaji ili
awasadie, atakuwa tayari kufanya hivyo.
"Muda ukiwadia na Watanzania wakisema
wananihitaji, basi nami nitakuwa tayari
kuwasaidia...jukumu hili linahitaji mtu mwenye
busara sana," alisema Sumaye.
Alipoulizwa kuhusiana na hali ya CCM kwa sasa,
alisema kuna tofauti kubwa katia ya CCM ya
mwaka 1977 na ya sasa ambayo imekuwa
ikikumbwa na matukio mengi.
Akitoa mfano, alisema: "Hivi sasa ukitaka
kugombea lazima uwe na fedha, haya ni mambo
machafu ambayo CCM yetu ya miaka ya 77
haikuwapo kabisa.
"Nalisema hili kutoka moyoni mwangu,
nimekuwa mbunge na mjumbe wa NEC kwa
miaka 20, sijawahi kutoa rushwa wala kupokea.
"Ukiona watu hao wanatoa rushwa, ujue moja,
hawana uwezo wa kuongoza wananchi wao na
ndani ya mioyo yao hawana dhamira safi zaidi ya
kutanguliza maslahi yao.
"Nikikuhonga leo ujue sina nia njema,
sitakuhudumia pindi nitakapoingia madarakani,
nitaanza kwanza kutafuta namna ya kurudisha
fedha zangu... hii ni vita ambayo CCM tunapaswa
kuipinga kwa nguvu zote," alisema Sumaye.
MUUNDO WA SERIKALI
Akizungumzia muundo wa Serikali, alisema yeye
ni muumini wa muundo wa serikali mbili siku
zote na atendelea kusimamia ukweli huo.
"Haiwezekani ndani ya taifa hili tukawa na
serikali tatu, hivi Rais wa Jamhuri ambaye
anamiliki mali nyingi, akisema anamnyima Rais
wa Tanganyika misaada nini kitatokea... huu ndio
mwanzo wa kuondoa utulivu wetu, tuwe makini,
tutaparanganyika," alisema Sumaye.
RUSHWA
Kuhusu rushwa, alisema wakati wa utawala wa
awamu ya tatu, chini ya Rais mstaafu Benjamin
Mkapa, walipambana vya kutosha, ikiwa ni
pamoja na kuondoa kipengele cha takrima.
"Tumepambana vya kutosha dhidi ya rushwa,
hata takrima tulihakikisha inaondolewa wakati
ule baada ya kubaini uchaguzi wa serikali za
mitaa ambao ulijumuisha madiwani, ndiko hali
hiyo ilikuwa imejikita.
"Nakumbuka enzi za utawala wangu, niliagiza
idara zote za serikali mikoani na wilayani
kukutana kwa saa moja kujadiliana masuala ya
rushwa na ugonjwa wa Ukimwi," alisema Sumaye.
MAWAZIRI MIZIGO
Akizungumzia utendaji kazi wa awamu yake,
Sumaye alisema ndani ya Baraza la Mawaziri
hakukuwa na mawaziri mizigo.
"Sikuwa na mawaziri mizigo kwenye utawala
wangu, utaona hata umma kwa sehemu kubwa
unakiri tulifanya kazi nzuri.
"Nakwambia ukiwa na mizigo unapaswa kuitua
haraka sana kabla ya watu hawajakuona," alisema
Sumaye.
WAPINZANI
Kuhusu vyama upinzani, Sumaye alisema
vimekuwa na mchango mkubwa wa kuimarisha
serikali katika utekelezaji wa mambo muhimu.
"Siku zote nimekuwa muumini mkuu wa
upinzani, wamekuwa kiungo muhimu, natamani
kuona wanaingia kwa wingi kwenye Bunge letu,
michango yao mizuri...nawaomba waendelee hivi
hivi wasirudi nyuma," alisema Sumaye.
MBOWE
Kuhusu kauli ya Mwenyekiti wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman
Mbowe, kwamba Katiba itapatikana kwa ngumi,
Sumaye alisema kauli hiyo si nzuri, kwa sababu
amani ikitoweka, si CCM wala CHADEMA
watakaopona.
"Nimemsikia akiruka na helikopta zake huko
mikoani na kusema atatumia nguvu, hivi jamani
leo amani ikitoweka, CCM na CHADEMA
watapona?" Alihoji Sumaye. www.hakileo.blogspot.com
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company