
Serikali ya Rwanda imemzuia balozi wa Ufaransa nchini humo kuhudhuria shughuli ya miaka 20 ya kukumbuka mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Michel Flesch amesema kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda ilimpigia simu usiku wa jana na leo asubuhi kumfahamisha kuwa, hangeruhusiwa kushiriki kwenye shughuli hiyo iliyofanyika katika uwanja wa michezo wa Amahoro mjini Kigali. Hatua hiyo ya serikali ya Rwanda inatokana na mzozo wa hivi karibuni wa kidiplomasia kati ya nchi hiyo na Ufaransa kufuatia hatua ya Rais Paul Kagame ya kuituhumu tena Paris kuwa ilihusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Matamshi ya Rais Kagame kwenye mahojiano na gazeti la kila wiki la Jeune Afrique linalochapishwa mjini Paris, yalipelekea Ufaransa kuamua kwamba Waziri wake wa Sheria hatashiriki shughuli ya miaka 20 ya kukumbuka mauaji ya kimbari ya Rwanda na badala yake Paris ingewakilishwa na balozi wake mjini Kigali. Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda haijaelezea ni kwa nini imemzuia Balozi Michel Flesch kuhudhuria kumbukumbu za leo.