
Eneo la Donetsk lililoko mashariki mwa Ukraine limejitangazia uhuru wiki kadhaa baada ya eneo la Crimea kujitenga na nchi hiyo. Wanaharakati wanaounga mkono serikali ya Russia wamevamia makao makuu ya mji wa Donetsk na kutangaza kwamba mji huo umejitenga na Ukraine na kwa sasa unaitwa ‘Jamhuri ya Watu wa Donetsk’.
Hatua hiyo imepingwa na serikali ya Ukraine ambapo rais wa muda, Oleksander Turchinov, amesema mji huo bado ni sehemu ya nchi yake. Turchinov ameituhumu serikali ya Russia kuwa inachoche harakati za kujitenga na kusema kuwa Moscow inapanga kuteka ardhi yote ya Ukraine kupitia njia hiyo. Inahofiwa kwamba, Donetsk huenda ikaamua kujiunga na Russia kama ilivyokuwa katika kesi ya Crimea.
Tayari wanaharakati wanaohusika wamesema wataandaa kura ya maoni ili watu wa Donetsk waamue iwapo watajiunga na Russia au wataendelea kuwa sehemu ya Ukraine.