CUF WAIBIPU UKAWA

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimetangaza Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, kuwa ni mmoja kati ya wanachama wa chama hicho, atakayewania nafasi ya Urais.

Pia chama hicho, kimetoa rasmi ratiba ya uchukuaji fomu na utaratibu wa kura ya maoni kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za uwakilishi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu wa udiwani, ubunge, uwakilishi na urais, na hadi ifikapo Aprili 25, chama hicho kitakuwa kimekamilisha uteuzi wa wagombea ubunge na uwakilishi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi wa chama hicho, Shaweji Mketo alisema kati ya wagombea waliojitokeza mpaka sasa kuwania nafasi hiyo ya urais ni Profesa Lipumba pekee.

“Kwa upande wangu mie kama Mkurugenzi wa Uchaguzi nina imani na Profesa Lipumba, kuwa atakuwa ndiye mgombea wetu wa urais tu kwa CUF bali hata kwa upande wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),” alisema Mketo


Alisema kwa mujibu wa makubaliano baina ya Ukawa, kila chama ni lazima kichague na kuweka wagombea katika nafasi na majimbo yote ikiwemo Urais na baadaye ndipo watakapochambua ni wagombea wangapi wabaki na akina nani waondoke na kwa nini.

Akizungumzia ratiba ya kuchukua fomu na kura ya maoni kwa wagombea wa chama hicho, alisema chama hicho kimeamua kujiandaa mapema kutafuta wagombea watakaokiwakilisha katika uchaguzi huo mkuu ambao pia watachujwa kupitia utaratibu wa kura za maoni.

Alisema kwa upande wa wanaotaka kuwania nafasi ya udiwani, fomu zitaanza kutolewa Machi Mosi hadi Machi 10, mwaka huu, na fomu hizo ambazo kila atakayezichukua atazilipia Sh 10,000 zitafikishwa kwa Katibu wa Kata Machi 11 hadi 13 mwaka huu kwa ajili ya utaratibu wa juu zaidi.

Kwa upande wa nafasi ya ubunge, alisema fomu hizo zitakazolipiwa Sh 50,000 zitaanza kutolewa nazo Machi Mosi hadi Machi 10, na Machi 15 hadi 30 mwaka huu, mikutano ya kata ya kura za maoni kwa nafasi ya udiwani itaanza kufanyika.

Mketo alisema kuanzia Machi 11 hadi 20, mwaka huu, Katibu wa kata wa chama hicho atazifikisha fomu za wagombea nafasi ya ubunge kwa Katibu wa wilaya na baada ya hapo maandalizi ya mikutano mikuu ya wilaya kwa ajili ya kura za maoni itaanza kuanzia Machi 31 hadi Aprili 4, mwaka huu.

Alisema kuanzia Aprili 5 hadi 15 mwaka huu, mikutano ya wilaya na majimbo ya kura ya maoni itafanyika na baada ya hapo Kurugenzi itafanya uchambuzi wa fomu za wagombea ubunge ili kuziwasilisha kwa Kamati ya Utendaji ya Taifa kuanzia Aprili 17 hadi 19, mwaka huu.

Aidha alisema kikao cha Kamati ya Taifa kwa ajili ya kuweka sifa za wagombea ubunge kinatarajiwa kufanyika kuanzia Aprili 20 hadi 21, mwaka huu, na kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kitafanyika kuanzia Aprili 22 hadi 23, mwaka huu.

Na kuanzia Aprili 24 hadi 25, mwaka huu, chama hicho kupitia Baraza Kuu la uongozi kitafanya uteuzi wa mwisho kwa wagombea wa ubunge na uwakilishi. Kuhusu ratiba ya kuchukua fomu kwa wagombea wa urais, alisema bado wanasubiri kikao cha pamoja cha Ukawa ambacho kitafanyika muda wowote kuanzia sasa, kitakachoweka taratibu za kuwatafuta wagombea urais.

Pamoja na hayo, Mketo alitupia lawama Jeshi la Polisi na kulituhumu kutumiwa vibaya na chama cha CCM, ambapo wanachama wake takribani nane waliopo mikoa ya Kusini wamekamatwa kwa tuhuma za ugaidi na hadi sasa hawajafikishwa mahakamani.

“Katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa chama chetu kilifanya vizuri katika maeneo yote ya kusini na kutokana na matokeo haya, tuna uhakika wa kufanya vizuri katika uchaguzi wa wabunge, sasa CCM wameona hivyo wanatumia polisi, kukamata viongozi wetu wanaoona ni tishio kwa kisingizio cha ugaidi,” alisisitiza.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company