Polisi watanda Muhimbili kuwazuia ‘JKT’

Mmoja wa vijana wa waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) akiruka kutoka katika gari kwenye viwanja vya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jana wakati walipokwenda kumjulia hali kiongozi wao ambaye amelazwa. Inadaiwa kuwa kiongozi huyo, George Mgoba, alitekwa na kupigwa na watu wasiojulikana na baadaye kutupwa msituni. Picha na Salim Shao
Na Raymond Kaminyoge, Mwananchi
KWA UFUPI

Waingia hospitalini hapo saa 12 asubuhi wakiwa na magari matano, Mgoba awekewa ulinzi wodini.

Kwenye kitanda alicholazwa Mgoba kulikuwa na mlinzi aliyekuwa amevaa fulana ya njano, aliyekuwa amekaa kwenye kitanda cha mgonjwa huyo akisema anamlinda. Baada ya Mgoba kutakiwa kuzungumza na waandishi wa habari, alisema akipata kibali kutoka kwa mlinzi huyo angezungumza, lakini mlinzi huyo alisema yupo hapo kwa ajili ya kuangalia usalama wa Mgoba.Daktari wa Zamu, Salome Kasanga aliwaomba waandishi wa habari wasizungumze na mgonjwa huyo kwa sababu alikuwa anahitaji kupumzika.Baadaye jioni, mwandishi wa Mwanachi alishuhudia Mgoba akibisha na mlinzi huyo akisema anataka kuondoka kwenda kutibiwa hospitali binafsi kwa kuwa hana imani na tiba na ulinzi anaopata Muhimbili.

Dar es Salaam. Polisi wenye silaha na mabomu ya machozi pamoja na maofisa usalama, jana walitanda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kuzuia vijana waliopata mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wasimwone mwenyekiti wao, George Mgoba, aliyelazwa baada ya kutekwa na kuteswa na watu wasiojulikana.

Pamoja na hatua hiyo vijana wengine watatu akiwamo katibu wa wahitimu hao walikamatwa na polisi na walikuwa wanashikiliwa katika Kituo Kikuu jijini Dar es Salaam.


Mgoba Jumatatu iliyopita alitekwa, kuteswa na baadaye kutupwa kichakani katika eneo la Picha ya Ndege, Kibaha mkoani Pwani.

Kabla ya kufikishwa kwenye Hospitali ya Muhimbili, Mgoba alilazwa kwenye hospitali ya Tumbi Kibaha na baadaye alihamishiwa Hospitali ya Amana wilayani Ilala.

Jana, wahitimu hao wa JKT wanaokadiriwa kufikia 200 walifika katika lango la Hospitali ya Muhimbili saa 11.50 asubuhi na kujichanganya na watu wengine waliokuwa wakisubiri kuwaona wagonjwa wao.

Ilipofika saa 12.10 magari ya polisi matano kila moja likiwa na askari sita yalifika katika eneo hilo na kuingia ndani ya eneo la hospitali hiyo huku polisi waliovaa sare wakisimama kwenye lango hilo kulinda usalama.

Makachero wengine waliingia ndani na kwenda moja kwa moja kwenye jengo la Mwaisela, wodi namba sita ambako Mgoba amelazwa.

Ilipofika saa 7.00 mchana watu waliofika kuangalia wagonjwa waliruhusiwa kuingia ndani na baadhi ya wahitimu wachache walijichanganya kwenda kuangalia wagonjwa.

Wengine wakamatwa

Hata hivyo, habari zilizopatikana baadaye na kuthibitishwa na Kiwango zilisema kuwa aliyekamatwa ni katibu wa wahitimu hao, Linus Emmanuel na wenzake wawili, ambao walitiwa mbaroni wakati wakienda Muhimbili na wanashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki hakupatikana kuthibitisha kukamatwa kwa vijana hao, lakini Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Sa Salaam, Suleiman Kova alipoulizwa alisema yeye yuko ofisini, vijana wake wanafanya kazi wakikamilisha wangempeleka taarifa.


Msimbazi
Awali vijana hao walikusanyika katika viwanja vya Msimbazi tangu saa 3.30 ili kujadiliana hatma ya kiongozi wao, wakionekana kuwa makini na kila aliyefika katika uwanja huo kama hawamfahamu walihitaji utambulisho.

Makamu mwenyekiti Kiwango alisema kitendo kilichofanywa aliitaka serikali kuunda tume ili kuchunguza aliyemteka na kumtesa mwenyekiti wao.

“Hata kama mwenyekiti wetu alikuwa na makosa si angekamatwa na kufunguliwa mashtaka ni kwanini vitendo vya utekaji na utesaji vimekithiri nchini mwetu,” alihoji Kiwango.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company