Katuni.
Wakati fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2015 zilitarajiwa kumalizika jana usiku kwa fainali baina ya Ivory Coast na Ghana, vyombo vya habari vya Ulaya vimekuwa vikiyashambulia mashindano hayo kwa matukio mabaya yaliyojitokeza nchini Guinea ya Ikweta ambako yamefanyika kwa dharura.
AFCON 2015 imefanyika kwa dharura nchini Guinea ya Ikweta baada ya kujitoa katika dakika za mwisho kwa waliokuwa wenyeji Morocco wakihofia kuingizwa nchini mwao kwa ugonjwa wa ebola.
Refa wa Mauritania, Rajindraparsad Seechurn, alifungiwa miezi sita kwa kuchezesha chini ya kiwango mechi ya robo-fainali iliyojaa vurugu baina ya wenyeji Guinea ya Ikweta dhidi ya Tunisia.
Wenyeji walipewa penalti ya utata katika dakika ya mwisho wakati wakiwa nyuma kwa bao 1-0. Wakasawazisha kupitia penalti hiyo na mechi ikaingia katika dakika 30 za nyongeza ambako wenyeji walipata goli la ushindi na kutinga nusu-fainali.
Wachezaji wa Tunisia walimzonga refa huyo na kutaka kumpiga kabla ya kuokolewa na walinzi wa uwanja. Kutokana na makosa yake, refa huyo alifungiwa miezi sita na shirikisho la soka barani Afrika (CAF).
Wenyeji katika nusu fainali walionekana kusahau kwamba walifika katika hatua hiyo kwa mbeleko na wakafanya mechi yao ya nusu-fainali isimame kwa zaidi ya dakika 30 kutokana na vurugu za mashabiki.
Huku wakiwa nyuma kwa magoli 3-0, katika dakika ya 82, mashabiki wa Guinea ya Ikweta walianza kurusha chupa uwanjani kuwapiga nazo wachezaji na pia kuwapiga mashabiki wa Ghana, ambao walilazimika kuondoka majukwaani na kuingia kwenye dimba la kuchezea wakisimama nyuma ya goli mojawapo uwanjani humo.
Mashabiki wapatao 36 walijeruhiwa huku wengine wakiumizwa vibaya. Helikopta ya polisi ililazimika kuja kusambaratisha mashabiki majukwaani.
Ni kweli kwamba hayo ni matukio ambayo hamna mpendasoka wa ukweli anayetaka kuona yanatokea kwenye viwanja vya soka. Na ni kweli pia kwamba ni matukio yanayotupaka tope Waafrika.
Lakini si sahihi kwa wachambuzi wa Ulaya kuyaita matukio hayo kuwa ni “soka la Afrika”.
Waafrika hatupaswi kukatishwa tamaa na kauli hizi za kibaguzi kwa sababu matukio ya vurugu uwanjani, marefa kuchezesha chini ya kiwango na kuwapa wapinzani penalti za utata yako dunia nzima. Siyo “soka la Afrika”.
Kwenye ligi kubwa na maarufu kama England, kila siku tumekuwa tukishuhudia matukio ya marefa kuibeba timu fulani kama vile kutoa penalti zinazotokana na wachezaji kujiangusha ndani ya boksi.
Mashabiki wa nchi kama za Urusi na nyingine za Ulaya ni kawaida kuingia uwanjani, kurusha mafataki uwanjani wakati mechi ikiendelea, kupigana na kadhalika. Iweje yanapotokea Afrika yaitwe ni “soka la Afrika”? Ni kauli za kibaguzi ambazo hazipaswi kuwafanya Waafrika kujisikia vibaya baada ya fainali tamu za AFCON ambazo tumeshuhudia mambo ya kukumbukwa kutoka kwa mastaa wetu wakubwa wanaong’aa huko huko kwao wanaojaribu kutubagua.
Goli kali la kutokea pembeni mwa uwanja la winga wa Ghana, Christian Atsu, katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Guinea wakati wa mechi yao ya robo fainali; goli la shuti la ‘roketi’ la Yaya Toure wa Ivory Coast katika ushindi wa 3-1 wa nusu-fainali dhidi ya DRC na chenga kali ya Wilfried Bony katika mechi ya Kundi D iliyoisha kwa sare ya 1-1 dhidi ya Mali, ni kati ya mambo mengi matamu ya kujivunia katika fainali za Afrika mwaka huu. Hilo ndiyo “soka la Afrika”.
Lakini pia, Guinea ya Ikweta wanapaswa kupongezwa kwa kuokoa mashindano hayo ambayo yalikuwa hatarini pengine kutofanyika kabisa mwaka huu. Ndani ya miezi miwili tu Guinea ya Ikweta waliweza kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha fainali hizo za kila baada ya miaka miwili zinafanyika.
Walikarabati miundombinu haraka na kuhakikisha kila kitu kinakuwa katika mstari kwa ajili ya kupokea maelefu ya mashabiki kwa ajili ya fainali hizo huku tahadhari ya ebola ikipewa kipaumbele. Hoteli zilikarabatiwa, viwanja vya mazoezi vilikarabatiwa huku nyasi mpya zikisafirishwa kwa ndege kutoka Ulaya na kupandwa kwenye viwanja vinne vilivyotumika kwa fainali hizo.
Zilikuwa ni juhudi kubwa za kujivunia, ukiacha ukorofi wa mashabiki wachache vichwamaji wasiojua uungwana wa soka walioanza kurusha chupa za maji uwanjani.
Kulikuwa na mengi ya kujifunza AFCON 2015.
CHANZO: NIPASHE
TAIFA STARS HAZARANI
-
Kaimu kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Etiene Ndairagije ametangaza
kikosi cha timu ya taifa chenye wachezaji 30 ambao wanajiaandaa na mchezo
wa kuwania ...
5 years ago