PICHA HII IMENIHUZUNISHA SANA, TUNACHO CHA KUFANYA, TUFANYE SASA..Ni ukatili kwa mtoto Alibino aliyekatwa kiganja cha Mkono Jumamosi.


Ndugu zangu,

Imenihuzunisha sana. Imenisikitisha sana. Haya ya mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi yanachangiwa na kitu kimoja tu; Ushirikina.

Pichani ni mtoto Baraka Cosmas Rusambo mwenye umri wa miaka sita mwenye ulemavu wa ngozi (Albinism). Amekatwa mkono wa kulia katika tukio lilitokea Jumamosi usiku tarehe7 Machi kwenye kijiji cha Kiseta, wilayani Sumbawanga vijijini, mkoani Rukwa.

Nani anayafanya haya?

Ni watu wenye kuendekeza imani za kishirikina ndio wenye kupelekea aibu hii kwa nchi yetu.

Nini cha kufanya?

1. Mbali ya kuwasaka wahusika wa moja kwa moja. Tuna lazima pia ya kuangazia mazingira yenye kupelekea haya. Hapa kuna umuhimu sasa kwa vyombo vyenye mamlaka kuweka adhabu kali kwa vyombo vya habari vyenye kueneza taarifa zenye kuchochea wanajamii kuamini na kuendekeza ushirika. Vyombo vya habari vyenye kupigia debe mambo ya kishirikina vikutwe na adhabu kali vikithibitishwa kwa ushahidi. Katika hili , kuna vyombo vya habari, kupitia taarifa zake za mambo ya kishirikina redioni, kwenye runinga na magazetini vimetokeea kutengeneza faida ya kifedha huku jamii ikizidi kuangamia kwa kulowekwa kwenye dimbwi la ujinga. Katika kundi hili, wamo pia waandaaji wa filamu zenye maudhui ya kishirikina bila kutoa ujumbe wa kupambana na imani hizo, bali kuziamini. Badala, yake, vipewe nguvu na hamasa, vyombo vya habari vyenye kujibidiisha na kuielimisha jamii kuondokana na haya ya ushirikina na abrakadabra.

2. Vyombo vyenye mamlaka vianze kazi ya kuwasaka waganga wa kienyeji wenye kufanya kupiga ramli ambazo mara nyingi zimepelekea watu kuelekezwa kutafuta visivyowezekana bila kutoa roho za wanadamu wenzao.

3. Mamlaka husika, viangazie na kutoa adhabu hata kufungua nyumba za ibada, kwa baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini na wamiliki wa nyumba za ibada ambao nao hushiriki katika kuwaaminisha waumini wao juu ya haya ya ushirikina na abrakadabra. Tuifanye kazi hiyo sasa. Haya ni mapambano muhimu kwetu kwa sasa. Tushirikiane.

Maggid Mjengwa.

Dar es Salaam.

0754 678 252(P.T)
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company