PROFESA JAY APASUA ANGA MIKUMI

Stori: Sifael Paul-GPL
Katika harakati za kulinyakua Jimbo la Mikumi wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro kwa tiketi ya chama chake cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mwanamuziki mkongwe wa muziki wa Kizazi Kipya, Joseph Haule almaarufu Profesa Jay (pichani) ameendelea kupasua anga kwenye jimbo hilo akifungua matawi mapya na kuhamasisha watu kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.



Profesa Jay akiwa na Joseph Mbilinyi 'Sugu'.

Akizungumza na Uwazi Mizengwe ya Uchaguzi akiwa jimboni humo, Profesa Jay aliyejiunga na Chadema mwaka 2013 na kutangaza nia ya kugombea ubunge wa Jimbo la Mikumi mwaka huu, alisema kuwa amefanya kazi kubwa ya kuhamasisha watu wake huku akikumbana na changamoto mbalimbali ambazo aliahidi kuzitatua mara tu akiingia mjengoni.(P.T)

Profesa Jay alisema kuwa tayari Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) wanashikilia Halmashauri ya Mji Mdogo wa Mikumi huku wakiwa wamechukua viti vingi vya serikali za mtaa kutoka saba vya awali hadi 107 kwa sasa.

“Nimeshafungua matawi mengi sana ya Chadema hapa Mikumi. Nimefanya kazi kubwa ya ujenzi wa chama changu. Nashukuru napata sapoti kubwa kutoka kwa chama changu na wasanii wenzangu.

“Kwa kweli wananchi wangu wamenikubali sana, kila ninapofanya mikutano yangu mjini na vijijini wanajaa sana na kuniunga mkono. Wanasema mkombozi wao amepatikana,” alisema Profesa Jay aliyetoa nyimbo nyingi za harakati za kutetea jamii.

Alipoulizwa juu ya changamoto zinazolikabili jimbo hilo na namna ya kuzitatua, Profesa Jay alisema kuwa zipo nyingi ambazo tayari wananchi wamemfikishia na nyingine ameziona kwa kuwa analijua vizuri jimbo hilo ambalo ndiko alikozaliwa.

“Kuna matatizo mengi kwenye Jimbo la Mikumi. Kuna rasilimali nyingi hasa Mbuga ya Mikumi ambayo kama mapato yakisimamiwa jimbo lina utajiri wa kutosha.

“Kuna matatizo ya ardhi, mapigano ya wakulima na wafugaji, hakuna huduma ya afya, maji, barabara, ajira duni na mengine ambayo ndiyo nitaanza kuyapigania bungeni ili kuhakikisha wananchi wangu wanakuwa na maisha bora,” alisema Profesa Jay anayelitaka jimbo hilo lililo chini ya Mbunge Abdulsalaam Seleman Amer wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company