Makamu wa Rais Zanzibar amuunga mkono Membe

‪Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.‬
Na Julius Mathias, Mwananchi

Dar es Salaam. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema atakuwa bega kwa bega na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe katika mbio zake za kuwania urais.

Membe, ambaye amekuwa akizungumzia kutangaza nia kuwania urais kama “kusubiri kuoteshwa”, ameshasema siku ikifika atachukua fomu lakini anatarajia kutangaza rasmi mpango wake jimboni kwake Mtama, sasa anaungwa mkono na mmoja kati ya viongozi wa juu wa Serikali na CCM kutoka Zanzibar ambayo ina nafasi ya pekee katika kuamua mgombea urais wa chama hicho.

Balozi Iddi ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje tangu mwaka 2006, alitoa msimamo huo wa kwanza kwa kiongozi wa juu wa Serikali jana jijini Dar es Salaam wakati akifunga mkutano wa siku tatu wa mabalozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali, akimwakilisha Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein aliyeshindwa kuhudhuria kutokana na msiba wa dada yake.

“Namtakia Membe safari njema na ninamuahidi kuwa tutakuwa naye bega kwa bega katika safari hii ngumu kwake,” alisema Balozi Idi bila ya kutaja neno urais.

Kauli ya makamu huyo wa Rais ilikuja baada ya Membe, ambaye amesema wakati ukifika atachukua fomu za kugombea urais, kuwaaga mabaozi hao kabla ya kumkaribisha mgeni huyo rasmi.

Katika hotuba yake ya mwisho kwa mabalozi hao, Membe aliweka wazi kuwa hatarudi tena bungeni akiwa waziri baada ya kuongoza wizara hiyo kwa takriban miaka minane.

Alirejea kauli yake ambayo amekuwa akiitoa mara kwa mara kuwa ameamua kuondoka wizarani hapo ili kujaribu nafasi kubwa zaidi katika siasa na kuwakaribisha bungeni mjini Dodoma ili wasikilize hotuba ya bajeti yake ya mwisho.

“Njooni msikilize bajeti yangu ya mwisho kama waziri kwani sitarajii tena kuingia bungeni kama waziri labda kwa nafasi nyingine ambayo ni ngumu sana,” alisema Membe akiwaaga mabalozi 36.

Waziri huyo pia alitumia nafasi hiyo kuwaomba mabalozi hao kuitangaza Tanzania nje, huku akitahadharisha kuhusu mabadiliko ya kisiasa yanayoendelea kutokea katika baadhi ya mataifa barani Afrika.
Alisema nchini Madagascar, Bunge limepiga kura ya kutokuwa na imani na rais na kuilazimu Mahakama ya Katiba kufanya uamuzi kuhusu suala hilo.

“Rais (Hery) Rajaonarimampianina amepigiwa kura 121 kati ya 125. Sitarajii kama kama Mahakama itaamua tofauti na matakwa ya Bunge. Hukumu inatarajiwa kutolewa leo (jana) baada ya kura hizo kupigwa jana (juzi),” alisema Waziri Membe.

Pamoja na kumuunga mkono Membe, Balozi Iddi aliwataka mabalozi hao kutumia vyema nafasi walizonazo katika kuitangaza Tanzania ili nchi inufaike na fursa za kiuchumi zilizopo huko walipo.Membe, ambaye amekuwa akizungumzia kutangaza nia kuwania urais kama “kusubiri kuoteshwa”, ameshasema siku ikifika atachukua fomu lakini anatarajia kutangaza rasmi mpango wake jimboni kwake Mtama, sasa anaungwa mkono na mmoja kati ya viongozi wa juu wa Serikali na CCM kutoka Zanzibar ambayo ina nafasi ya pekee katika kuamua mgombea urais wa chama hicho.

“Amani na utulivu ni rasilimali muhimu katika kuvutia wawekezaji. Zanzibar ipo tayari kusikiliza maoni yenu juu ya nini cha kufanya ili kuitangaza zaidi kimataifa,” alisema.

Kaimu kiongozi wa mabalozi wa Tanzania, John Kijazi, akitoa neno kwa niaba ya wenzake, alisema mkutano huo umekuwa wa mafanikio na wamepata maazimio kadhaa wanayokwenda kuyatekeleza katika nchi wanakofanya kazi.

Aliitaka Serikali kuwawezesha ili kutekeleza majukumu hayo kwa ufanisi na kwa wakati ili kuleta tija. Aliwatakia kila la heri viongozi hao wawili wanaotoka katika jamii ya wanadiplomasia nchini katika harakati zao za kisiasa.

“Tunawatakia kila la heri katika nafasi mbalimbali mnazogombea. Kwa mfano wako, Balozi (Iddi) natarajia kuwa mwaka huu kutakuwa na utitiri wa wanadiplomasia watakaojiunga nawe,” alisema Balozi Kijazi.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company