Balozi Ali Karume akizungumza na wanachama wa CCM katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja jana. Picha na Mwinyi Sadallah Na Salma Said na Mwinyi Sadallah, |
Zanzibar. Mwanadiplomasia mashuhuri visiwani Zanzibar, Balozi Ali Karume ametangaza nia ya kuchukua fomu ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Balozi Karume alitangaza nia yake hiyo jana katika Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kati Unguja na kuahidi kuwa iwapo chama chake kitampitisha na kupata ridhaa ya kuingia Ikulu, atatoa uhuru wa kujieleza kwa wananchi wake na uhuru wa kuikosoa Serikali bila ya kuvunja sheria na katiba ya nchi.
Alitumia muda mwingi kuelezea historia na uzoefu wake wa uongozi ndani ya chama na Serikali na kuwataka Watanzania kutokurupuka kumchagua rais kama watataka maendeleo endelevu.
Balozi Karume alisema ameamua kugombea nafasi hiyo ya urais, baada ya kujipima na kuona ana sifa na uwezo wa kuliongoza Taifa la Tanzania na akawakumbusha wagombea wenzake umuhimu wa kuwa na kiongozi atakayeweza kujenga umoja na kudumisha amani miongoni mwa Watanzania.
“Ni wakati wa kufikiria na kutukuza utaifa wetu, badala ya Utanganyika na Uzanzibari,” alisema Balozi Karume katika mkutano wake huo uliochukua takriban saa moja na nusu.
Kwa mujibu wa Balozi Karume, urais unahitaji kiongozi mwenye sifa na uadilifu atakayepiga vita vitendo vya ubadhirifu na kukemea rushwa ili kujenga Taifa lenye kufuata misingi ya sheria na utawala bora.
“Uongozi si suala la majaribio, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuwa makini na watu ambao walishawahi kupewa uongozi na kushindwa kutokana na kukosa uadilifu,” alisema Balozi Karume.
Hata hivyo, alisema kwamba atahakikisha anaendeleza mipango yote ya maendeleo iliyoanzishwa na Rais Jakaya Kikwete na kukabiliana na kero mbalimbali zinazowakabili Watanzania hasa suala la umaskini, maradhi na elimu.
Vipaumbele vyake
Akizungumza katika shamrashamra za kutangaza nia hiyo, Balozi Karume alisema lengo lake ni kuwania nafasi hiyo ya juu serikalini ili kupokezana kijiti na kuendeleza mambo yote mazuri yaliyoanzishwa na mtangulizi wake, Rais Jakaya Kikwete.
Balozi Karume alitaja kipaumbele chake cha kwanza kuwa ni uhuru wa watu wote. “Kila mtu ana haki ya kuwa na uhuru wa kujiamulia mambo yake kuwa muumini wa dini au chama chochote cha siasa tena bila kubughudhiwa na mtu mwingine.
“Mkombozi wa mwananchi ni kuimarisha kilimo kwanza, elimu baadaye, huwezi kusoma huku ukiwa na njaa na hilo ndilo lengo nikipata ridhaa ya kuwa Rais wa Muungano” alisema Balozi Karume.Alisema Tanzania ili iweze kujenga uchumi imara, inahitaji kiongozi mwenye mbinu na uwezo wa kupambana na rushwa na ufisadi kwa vile ndiyo adui wakubwa wa maendeleo yake.
Alisema kuwa atahakikisha Watanzania wanapata uhuru wa kuchagua chama wanachotaka, uhuru wa kuabudu dini wanayotaka na kufanya biashara katika mazingira bora pamoja na kufungua milango ya uwekezaji yenye masilahi kwa Serikali na wananchi wake.
Alisema uhuru atakaousimamia pia utahusu uhuru wa kujituma na kufanya biashara bila kuwekewa vikwazo, kwani nayo ni haki ya msingi ya wananchi wa Tanzania.
“Uhuru wa kujituma ni muhimu sana kwa kila mtu siyo mtu anataka kuuza njugu wewe unamwambia huna leseni… leseni kwani anataka kuendesha gari? Mtu akitaka kuendesha gari ndiyo mdai leseni, lakini siyo kuuza njugu lazima watu wapewe uhuru wa kujituma,” alisema Balozi Karume.
Balozi alieleza kuwa atasimamia uhuru wa kuepukana na njaa kwa kusimamia uanzishwaji wa viwanda ili kusindika mazao na bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kuziongezea thamani.
Karume alitumia muda mwingi kuelezea historia ya nchi na CCM akieleza kuwa ni muhimu kwa wanachama hao kuwachagua viongozi wenye uelewa mzuri wa kimataifa na siyo watu ambao wanasindikiza na kutia aibu mbele ya mabalozi wa nchi za nje.
“Hatutaki mtu wa okay, sir au yes sir! Tunataka mgombea urais ambaye anaelewa mambo ya kidiplomasia na anajua kuzungumza na mataifa mbalimbali siyo anakwenda Ulaya anashindwa kuongea badala yake anaitikia tu yes sir,” alisema.
Balozi Karume amewataka wanachama wa CCM kuwachagua viongozi kwa vigezo vya uwezo na uadilifu na siyo kwa sababu wamekaa muda fulani katika matawi na mashina ya chama hicho tawala, huku akielezea jinsi gani wao walivyopikwa katika chama hicho.
Aidha, aliwapiga vijembe wenzake waliotangulia akisema wapo baadhi ya wagombea ambao wametangaza anataka kuunda Tanzania mpya jambo ambalo alisema haliwezekani kwani Tanzania ni hiyohiyo na haiwezi kuwa nyingine.
Alisema watu waliosema hawatakubali kilimo kwanza na badala yake watawekeza kwenye elimu wamekosea, kwani ingawa elimu ni muhimu, kilimo nacho bado ni muhimu pia.
Ilivyokuwa ukumbini
Balozi Karume aliwasili katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kati mkoani Unguja saa 9:45 jioni akiwa ameambatana na Zainabu Shamori ambaye amewahi kuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba na Kusini Unguja.Pia, Zainabu amewahi kuwa Naibu Waziri wa Afya, Zanzibar wakati wa uongozi wa Rais Amani Abeid Karume na aliwahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC).
Baada ya Balozi Karume kuwasili katika ukumbi huo alipokewa na wapambe wake ambao ni wanachama wa CCM na baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wakiimba na kushangilia kwa kupiga makofi muda wote.
Balozi huyo alipopanda jukwaani, kundi la watu waliokuwapo ukumbini ambao idadi yao haikufika 100, waliendelea kuimba na kushangilia kwa kupiga makofi. Hata hivyo, hapakuwapo na shamrashamra za ngoma.
Licha ya uchache wao, watu hao walionekana wenye furaha na kumshangilia Balozi Karume kwa kila neno alilokuwa akisema hasa pale alipoelezea namna atakavyopambana kuondoka rushwa na ufisadi unaoitafuta Serikali na kudhoofisha uchumi.
Huku akiendelea kushangiliwa, Balozi Karume alisema kwamba Rais mstaafu Karume, ambaye ni kaka yake, alisema kuwa katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu ni vizuri apatikane rais mwenye uzoefu wa kimataifa.
“Rais alisema ni vizuri apatikane rais ambaye atakuwa ametembea nchi mbalimbali ili ajue uzoefu wa mataifa mengine yanayofanya kazi,” alisema Balozi Karume.
Balozi huyo aliongeza kuwa uzoefu wa kimataifa ni sifa muhimu kutokana na kasi ya maendeleo ya kiuchumi inayoendelea duniani hivi sasa.
Katika mkutano huo wa Balozi Karume, hakuna viongozi maarufu waliopo madarakani au wastaafu waliomsindikiza kama ambavyo imekuwa kwa baadhi ya wanasiasa wanaotangaza nia ya kuwania nafasi ya kuteuliwa na vyama vyao kugombea urais.
Siyo mara ya kwanza
Balozi Karume aliwahi kugombea urais wa Zanzibar mwaka 2000, lakini alijitoa katika hatua za awali na kumwachia Rais Karume, pia mwaka 2005 na mwaka 2010, aligombea urais wa Tanzania Bara.
Wakati akiondoka ukumbini baada ya kutangaza nia jana, Balozi Karume alitumia muda mwingi kusalimia wanachama waliokuwapo ukumbini kwa kuwapa mikono.