Burundi: utawala umekubali mapendekezo ya AU kwa masharti

Askari polisi ikimkamata mmoja kati ya waandamanaji wakati maandamano dhidi ya muhula wa tatu wa rais Nkurunziza, Bujumbura, mwanzoni mwa mwezi Juni.
REUTERS/Goran Tomasevic
Na RFI

Baada ya siku nne za kutafakari kwa kina, serikali ya Burundi imejibu kuhusu tangazo la mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika uliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, mkutano ambao ulijadili mgogoro nchini humo.

Serikali haijakataa mapendekezo ya Umoja wa Afrika, lakini imesema mapendekezo hayo inayakubali kwa masharti.

Serikali ya Burundi imesema iko tayari kushirikiana na waangalizi wa haki za binadamu, lakini pia na wataalamu wa kijeshi ambao watasimamia zoezi la kuwapokonya silaha wanamgambo nchini Burundi. Lakini utawala umetoa masharti ya kupelekwa kwa timu hizo za Umoja wa Afrika.

" Tunasema kwamba tuko tayari kufanya kazi na Umoja wa Afrika. Lakini watueleze wataalam hao wa kijeshi ni kutoka nchi gani, idadi yao, na majukumu yao. Kila kitu kitategemea na msimamo ambao Umoja wa Afrika utaonyesha katika kazi hiyo ", amesema waziri wa mambo ya nje wa Burundi, Aimé Alain Nyamitwe.

Itakuwa vigumu katika mazingira haya, kupeleka waangalizi na wataalamu wengine ndani ya wiki mbili zilizotolewa na Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika. Waziri wa mambo ya nje wa Burundi anaona kuwa umuhimu katika kesi hii ni kwamba " serikali ya Bujumbura imeonyesha nia yake ya kupokea ujumbe wa aina hiyo."

Pamoja na uwazi huu, serikali ya Bujumbura imetupilia mbali uwezekano wowote wa kuketi kwenye meza ya mazungumzo na upinzani pamoja na mashrika ya kiraia kuhusu suala tata la muhula wa tatu wa rais Pierre Nkurunziza. Suala la muhula wa tatu ndio chanzo ya mgogoro wa Burundi. Hata hivyo tangazo la Baraza la Amani na Usalamala Umoja wa Afrika halijataja suala la muhula wa tatu, amesema Aimé Alain Nyamitwe.

Waziri wa mambo ya nje wa Burundi Aimé Alain Nyamitwe pia amesema suala la kalenda ya uchaguzi halipaswi kuzungumziwa, wakati ambapo Umoja wa afrika unataka itolewe kwa makubaliano ya wadau wote katika mchakato wa uchaguzi nchini Burundi.

Itafahamika kwamba Jumatau wiki hii, Ikulu ya rais ilifutilia mbali mapendekezo ya Umoja wa Afrika na kusema kwamba haitotekeleza pendekezo hata moja.

Wakati huo huo Ubelgiji umeomba jumuiya ya kimataifa kuwachukulia vikwazo viongozi ambao wanakwamisha mazungumzo ya kisisa nchini Burundi.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company