Karenzi Karake akamatwa Heathrow

Mkuu wa upelelezi nchini Rwanda,ambaye alikuwa anasakwa nchini Hispania kwa makosa ya uhalifu wa kivita,sasa amekamatwa mjini London.

Kitengo cha habari cha BBC cha BBC Newsnight, kimegundua kwamba askari wa kikosi cha Metropolitan walimkamata Karenzi Karake kwenye uwanja wa ndege wa Heathrow mnamo mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kikosi hicho cha askari wa Metropolitan tayari kimethibitisha kwamba Karenzi ambaye sasa ana umri wa miaka 54, amefikishwa katika mahakama moja ya Westminster baada ya kuwekwa kizuizini kwa hati ya kukamtwa ya umoja wa ulaya, na atasalia kizuizini mpaka mwishoni mwa wiki hii.

Karake alikuwa ni mkurugenzi mkuu wa usalama wa taifa wa Rwanda .Karake alipigana vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Rwanda mwaka 1990 hadi mwaka 1994 na baadaye alipata cheo cha kamanda msaidizi wa vikosi vya kulinda Amani vya umoja wa mataifa huko Darfur. Karake ni miongoni mwa makamanda walioko kwenye orodha ya makamanda wa Kinyarwanda wapatao 40 ,waliomo katika hati ya mashitaka iliyotolewa mwaka 2008 na kikosi cha uchunguzi cha Hispania kinachoongozwa na jaji Andreu Merelles.

Mahakama hiyo ya nchini Hispania inamtuhumu Karake, kwamba wakati alipokuwa kiongozi mkuu wa kijeshi wakati wa mauaji ya kimbari, aliamuru mauaji ya watu kadhaa. Lakini pia kiongozi huyo wa kijeshi anatuhumiwa pia kwa kuamuru mauaji ya raia watatu wa Hispania waliokuwa wakifanya kazi katika asasi moja ijulikanayo kama Medicos del Mundo nchini Rwanda.

Kukamatwa kwa Karake kuna uwezekano mkubwa wa kuiingiza serikali ya Uingereza katika mgogoro wa kidiplomasia na nchi ya Rwanda.

Inaarifiwa kwamba Mnamo mwaka 2013 Rwanda ilikuwa inashika namba 18 miongoni mwa nchi zinazopokea misaada ya kiwango cha hali ya juu kutoka Uingereza.

Karake ni wa kwanza kukamatwa miongoni mwa makamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la RPF kwa mashtaka yanayomkabili nje ya nchi yake. Wakili Jordi Palou-Loverdos, anayewakilisha watu 9 ambao wameuawa wenye asili ya Hispania ameiambia BBC, "Tunaamini kwa haki ya marehemu ninaowasimamia itatendeka na haraka Karenzi Karake atapelekwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili na huko atajitetea yeye mwenyewe.

Na tunaamini kwamba wanasiasa na wengine wenye mvuto na kesi yake hawataingilia kati na kuizorotesha kesi, haki,ukweli na fidia vitapatikana."
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company