> Mbunge wa Hai , Freeman Mbowe akizungumza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Hai, Kilimanjaro jana mara baada ya kulipa faini ya shilingi milioni moja na kuachiwa huru ,hukumu iliyotokana na kutiwa hatiani kwa kosa la kumshambulia mwangalizi wa uchaguzi mwaka 2010. Picha na Dionis Nyato.
Na Daniel Mjema
KWA UFUPI
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Hai, Denis Mpelembwa. Mbowe, ambaye ni Mbunge wa Hai alilipa faini hiyo iliyochangwa chapchap na wabunge saba wa Chadema na wafuasi wa chama hicho waliokuwa mahakamani hapo.
Hai. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amehukumiwa kulipa faini ya Sh1 milioni au kwenda jela mwaka mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kumshambulia mwangalizi wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Hai, Denis Mpelembwa. Mbowe, ambaye ni Mbunge wa Hai alilipa faini hiyo iliyochangwa chapchap na wabunge saba wa Chadema na wafuasi wa chama hicho waliokuwa mahakamani hapo.
Wabunge waliochanga fedha hizo ni, Mustafa Akuney wa Mbulu Lucy Owenya, Grace Kiwelu, Cecilia Pareso, Joyce Mukya, Rose Kalili na Paulin Gekul wote wa Viti Maalumu.
Utata wa kupoteza sifa ya kugombea
Hukumu hiyo iliibua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii juu ya uwezekano wa kumzuia Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni kuwania tena ubunge au urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Hata hivyo, Mwanasheria, Alex Mgongolwa akinukuu Katiba ya Tanzania Ibara ya 67 (1)(c); 67(2) (c na d) alisema hukumu hiyo haiwezi kumzuia kugombea ubunge kwa sababu hakwenda jela na kosa lake halihusu kukosa utovu wa uaminifu, kukwepa kodi wala kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Suala hilo linafanana na lililotokea katika mchakato wa uteuzi wa wagombea urais mwaka 2005 wakati aliyekuwa mgombea urais wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila na mgombea mwenza wake, Saidi Soud Said walipowekewa pingamizi kutokana na kutumikia kifungo jela, Mtikila akitumikia mwaka mmoja kwa kosa la uchochezi, Said akitumikia chuo cha mafunzo kwa kosa la biashara ya vitambaa. Hata hivyo, pingamizi hilo lilitupwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Lewis Makame (marehemu) baada ya kusikiliza utetezi wa Mtikila na Said, kuwa makosa waliyofungwa kwayo hayakuwa ya kukwepa kodi, kukosa uaminifu wala kukiuka maadili ya viongozi wa umma.
Mashtaka
Mbowe alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya kumfanyia shambulio la kawaida, mwangalizi wa ndani wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 31, 2010, Nassir Yamin katika kituo cha kupigia kura kilichokuwa katika Zahanati ya Lambo.
Yamin alikuwa ni mwangalizi wa kutoka Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mpelembwa ambaye amehamishiwa Bukoba, alisema kitendo kilichofanywa na Mbowe hakikubaliki na kinapaswa kukemewa.
“Kitendo alichokifanya mshtakiwa akiwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema na Mbunge wa Jimbo la Hai ambaye alipaswa kuwa kioo cha jamii hakikubaliki na lazima kikemewe,” alisema.“Kwa hiyo hukumu ya Mahakama ni kwamba atalipa faini ya Sh1,000,000 au akishindwa kulipa atakwenda magereza kwa mwaka mmoja,” alisema hakimu huyo.
Ushahidi
Akichambua ushahidi uliomtia Mbowe hatiani, Hakimu huyo alisema Mahakama imeegemea ushahidi wa shahidi wa kwanza, Yamin na shahidi wa pili John Mushi aliyekuwa msimamizi wa kituo.
Alisema ushahidi huo ulieleza kuwa siku hiyo Mbowe aliingia katika Kituo cha Zahanati ya Lambo katika Jimbo la Hai na kuuliza uhalali wa mlalamikaji kuwapo kituoni hapo.
Mashahidi hao waliiambia Mahakama kuwa walimuona Mbowe akimkunja na kumtoa nje kwa nguvu mwangalizi huyo wa ndani na baadaye mbunge huyo kuondoka katika kituo hicho.
Alisema ushahidi wa mashahidi hao uliungwa mkono na shahidi wa nne wa mashtaka, ambaye ni daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Hai, aliyemtibu mlalamikaji na kujaza fomu PF3.
Alisema ushahidi wa daktari huyo unaonyesha kuwa mlalamikaji alikuwa na michubuko katika shavu lake moja na shingoni iliyotokana na kupigwa na kitu butu.
Hata hivyo, aliukataa ushahidi wa shahidi wa saba, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Shafii aliyekuwa mpelelezi mkuu kuwa Mbowe alikiri kufanya kosa hilo alipoandika maelezo ya onyo polisi.
Hakimu Mpelembwa alisema japokuwa upande wa mashtaka uliwasilisha maelezo hayo kama kielelezo lakini baada ya kuyapitia, hakuna mahali ambako Mbowe alikiri kufanya kosa hilo.
Utetezi wa Mbowe
Hakimu Mpelembwa alisema wakati akijitetea mahakamani, Mbowe alikanusha kufanya tukio hilo lakini alikiri kufika katika kituo hicho na kumtaka mwangalizi huyo kumwonyesha kitambulisho chake.
“Katika utetezi wake, mshtakiwa alikanusha kumpiga Nasir Yamin wala kumfanyia kitu chochote kibaya, bali alimwamuru atoke nje kwani hakuwamo kwenye orodha ya waangalizi iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.”Hakimu huyo alisema, Mbowe alieleza kuwa hakuwahi kuitwa polisi, bali alikwenda mwenyewe baada ya kusikia kwenye vyombo vya habari kuwa amefunguliwa kesi ya aina hiyo.
Sababu za kutiwa hatiani
Hakimu Mpelembwa alifafanua dhana ya kosa la shambulio kuwa ni kitendo chochote chenye nia ya kudhuru mtu mwingine au hata kujaribu tu kumdhuru au kumtia hofu.
“Kwa maana nyingine ni kitendo cha kumtia mtu mwingine hofu na ili kosa hilo litimie ni lazima mshtakiwa awe na nia isiyo halali kisheria ya kutaka kutenda kosa nililolianisha,” alisema.
Hata hivyo, hakimu huyo alisema shahidi wa kwanza (Yamin) na wa Pili (msimamizi) waliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa alimkunja na kumvuta nje mlalamikaji atoke nje ya kituo.
“Ushahidi wa Yamin na Mushi ni wa kuona kuwa mshtakiwa alimkunja na kumtoa nje mlalamikaji. Swali hapa ni je, kumvuta mtu na kumtoa nje kunapelekea kosa la shambulio?” alihoji.
Hakimu huyo alisema kwa tafsiri ya dhana nzima ya kosa la shambulio ni dhahiri kitendo alichokifanya mshtakiwa kinaangukia katika kosa hilo kwa mujibu wa sheria.
“Ushahidi wa shahidi wa kwanza na wa pili wa upande wa mashtaka unashabihiana na ushahidi wa daktari kwamba kulikuwa na michubuko. Kwa mantiki hiyo Mahakama inakubali ushahidi huo. Kutokana na Mahakama kukubali ushahidi wa mashahidi hao watatu, inakutia hatiani kwa kosa la shambulio kama ulivyoshtakiwa nalo.”
Mwendesha mashtaka, Inspekta Msaidizi wa Polisi, Feo Simon alisema ingawa hawana kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya mshtakiwa, aliiomba itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwake na kwa jamii.
Wakili wa Mbowe, Issa Rajabu aliyekuwa akisaidiana na Albert Msando, aliomba Mahakama impe adhabu ndogo mteja wake kwani hajawahi kutenda kosa lolote la jinai.
Hata hivyo, Hakimu Mpelembwa alisema kwa kutoa adhabu ya faini ya Sh1 milioni au kifungo cha mwaka mmoja jela amezingatia ombi la wakili wa Mbowe.
Baada ya hukumuHukumu hiyo iliyoanza saa sita mchana hadi saa 7.20 mchana, wafuasi wa Chadema waliokuwa wamefurika mahakamani hapo walitandika kanga chini na kuanza kuchangishana faini hiyo kazi ambayo ilisimamiwa na Kiwelu.
Wakati kazi hiyo ikiendelea, Mbowe aliendelea kushikiliwa ndani ya chumba cha Mahakama hadi wabunge hao walipokwenda Benki ya NMB, Tawi la Hai saa 7.40 mchana na kulipa faini hiyo na Mbowe kuachiwa saa nane mchana.
Mbowe azungumzia hukumu
Akizungumza nje ya chumba cha Mahakama hiyo, Mbowe aliwatoa hofu wanachama wa Chadema kwamba wasikatishwe tamaa na hukumu hiyo ambayo alisema alitegemea ingekuwa hivyo.
“Mnanipa pole ya nini? Kuna msiba hapa? Tupeane hongera. Sikutarajia cha tofauti na hiki kilichofanyika. Hakinivunji nguvu, bali kinaniimarisha katika mapambano,” alisema.
“Haki katika nchi hii itapiganiwa kwa watu wengine kuumia na wengine kuokoka. Nimesota mahakamani miaka mitano badala ya kufanya kazi ya wananchi. Hainivunji moyo,” alisema na kuongeza:
“Hainivunji moyo katika azma yangu ya kuikomboa nchi hii na ukombozi uko jirani. Mahakama ya nchi hii vimekuwa ni vyombo vya kutoa dhuluma kwa wananchi japo siyo mahakimu wote. Lakini iko siku Mahakama zitakuwa ni sehemu ya kutolea haki, kutenda haki na haki ionekane imetendeka. Mapambano yanaendelea na nawaomba msiwe wanyonge,” alisisitiza.
“Sitaki kuizungumzia Mahakama katika hatua ya sasa lakini ndani ya Mahakama kuna watu wanaotenda haki na ndani ya Mahakama kuna watu wasiotenda haki,” alisema Mbowe.
Alisema kesi hiyo haikustahili kuiendesha kwa miaka mitano na kwamba kodi za wananchi zinateketea pamoja na muda, akisema haiwezekani nchi ikaendeshwa katika utaratibu huo.
“Kama mimi mbunge, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, mtunga sheria wa nchi hii naweza kusoteshwa mahakamani miaka mitano, mwananchi wa kawaida atafanywaje?” alihoji Mbowe.
#USOPEN_VIGOGO CHALI
-
SIKU Safi kwa Muaustralia Nick Kyrgios baada ya ushindi dhidi Johnson na
kutinga raundi ya Pili.
- Rafael Nadal akimchapa Millman Seti Tatu zote mfululi...
5 years ago