Rais Kikwete Aongoza Maziko ya Sheikh Mkuu wa Tanzania Muft Issa Shaaban Simba

Rais Jakaya Kikwete jana jioni ameongoza maziko ya sheikh mkuu wa Tanzania Muft Issa Shaaban Simba aliyefariki jana katika hospitali ya TMJ jijini Dar es salaam.

Maziko hayo yalifanyika katika makaburi ya waisilamu ya nguzo nane mjini Shinyanga na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa Shinyanga wakiongozwa na mkuu wa mkoa huo Ally Nassoro Lufunga.

Mwili wa marehemu uliwasili nyumbani kwake majengo majira ya saa 9 na maziko kufanyika majira ya saa kumi baada ya ibada iliyofanyika katika msikiti wa Ijumaa wa Majengo ambao marehemu alikuwa sheikh wake.

Wakitoa salam za rambirambi , baadhi ya viongozi wa serikali waliohudhuria mazishi hayo walisema hakika taifa limepoteza kiongozi imara na shupavu ambaye alikuwa kiungo kikuu kati ya madhehebu mbalimbali ya dini na serikali kwa ujumla.

Mbali na Rais Kikwete viongozi wengine wa kitaifa waliopata fursa ya kusindikiza maziko ya sheikh mkuu ni pamoja na Waziri wa mambo ya nje na Ushirikiano wa kimataifa Bernard Membe, Mbunge wa Monduli Mh Edward Lowassa, Waziri mkuu mstaafu Fredrick Sumaye pamoja na viongozi wengine wa dini na serikali.

Nao baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu mjini shinyanga walisema kifo cha mufti Issa Simba ni pengo kubwa lisiloweza kizibika kwa haraka kwani alikuwa kiongozi mnyenyekevu na pia alikuwa mwalimu wa kufundisha na kuonya bila kubagua dini yoyote.

Wakati huohuo jijini Dar es salaam makamu wa rais wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal jana aliwaongoza waumini wa dini ya Kiislam, viongozi mbalimbali pamoja na watu wengine waliojitokeza katika swala ya kumuombea marehemu Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Shaaban Issa Bin Simba

Dkt Bilal alisema taifa limempoteza kiongozi muhimu sana wa kidini na katika jamii.

Akiongea katika swala hiyo iliyofanyika Makao Makuu ya Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Jijini Dar es Salaam, Dk. Bilal alimuelezea marehemu Mufti Shaaban Issa Bin Simba kama kiongozi aliyekuwa sura ya usuluhishi katika jamii yetu na alijenga mahusiano mazuri na serikali na katika jamii kwa ujumla.

Naye Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Hemed Jalala alimuelezea marehemu Mufti Shaaban Issa Bin Simba, kuwa alikuwa ni baba wa watanzania wote na wala hakukubali waishi kwa matabaka.

Mwili wa Mufti Shaaban Issa Bin Simba ulisafirishwa jana asubuhi kwa ndege kuelekea mkoani Shinyanga na maziko yake yakafanyika jioni hiyo hiyo nyumbani kwake Majengo, Shinyanga.

Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company